The House of Favourite Newspapers

Unending Love 43

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.

Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona.

Je, nini kitafuatia?

 SONGA NAYO…

Walifanya kila kilichowezekana ili mradi mwisho wa siku kijana wao aweze kupona na kuwa kwenye hali yake ya kawaida. Hawakutaka kumuona akiumwa tena, kwao, Jafet alikuwa kila kitu. Hawakuwa na hela lakini kitendo cha kuwa mgonjwa, hawakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima wafanye chochote kinachowezekana ili kuyaokoa maisha yake.

Tayari walikuwa ndani ya gari kuelekea katika Hospitali ya Bugando, ndani ya daladala, kila mmoja alikuwa kimya, walionekana kuwa na mawazo, mioyo yao ilibeba majonzi makubwa, walisali mioyoni mwao ili Mungu aonekane katika afya ya kijana wao.

Safari iliendelea kama kawaida, walipofika Mwanza Mjini, moja kwa moja wakaunganisha kuelekea katika hospitali hiyo. Walipofika, wakafuata taratibu zote na hatimaye Jafet kuchukuliwa na kupelekwa katika chumba cha vipimo, kama walivyoambiwa katika hospitali waliyotoka, hata hapo waliambiwa vilevile kwamba kijana wao alikuwa na matatizo makubwa ya ugonjwa wa figo.

“Mtaweza kumtibu?” aliuliza mama Jafet.

“Hakuna tatizo, cha msingi malipo yawepo,” alijibu daktari.

Mara baada ya kulipia gharama walizotakiwa kulipia, matibabu yakaanza rasmi. Hakukuwa na mtu aliyeondoka kurudi nyumbani, walitaka kufuatilia hatua kwa hatua mpaka pale ambapo madaktari wangemaliza matibabu yao.

Mama Jafet hakuweza kuvumilia, alimpenda sana kijana wake, kitendo cha kuwa kwenye hali mbaya namna hiyo ilimfanya muda wote kutokwa na machozi ya uchungu, alijisikia maumivu makubwa moyoni mwake, wakati mwingine alisikia sauti moyoni ikimwambia kwamba mtoto wake hatoweza kupona, hiyo ilikuwa safari yake ya mwisho, angekufa.

“Hawezi kufa, Jafet hawezi kufa,” alijikuta akisema mama Jafet huku akilia.

“Kuna nini tena?” aliuliza mume wake.

“Ni mawazo, nasikia sauti ikinitisha kwamba Jafet atakufa,” alijibu mama Jafet.

“Hawezi kufa, Mungu atamponya,” alisema baba Jafet.

Hicho ndicho kilichoendelea, baada ya saa tisa, madaktari wakawa wamekwishamaliza kumfanyia upasuaji hivyo kutoa muda wa saa mbili kwa ajili ya mapumziko. Kila walichoambiwa walikifanya, baada ya kukatika saa mbili, wakaruhusiwa kwenda kumuona kijana wao, kila mmoja uso wake ukajawa na tabasamu pana.

Baada ya wiki mbili, Jafet akawa mzima wa afya. Alitakiwa kusafiri kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na Chuo cha Muhimbili kwa ajili ya kuanza masomo ya kitabibu.

Kwa kuwa hakuwa na fedha, akaanza kufuatilia mkopo katika Bodi ya Mikopo kwa wanachuo na baada ya mwezi mmoja, akafanikiwa kupata mkopo hivyo kuanza safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, sehemu ambayo hakuwahi kufika zaidi ya kusikia kutoka kwa watu tu.

*****

Usiku, William hakulala, kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi juu ya msichana Anna, alimpenda mno na alikuwa tayari kwa kila kitu. Kitendo cha msichana huyo kumkatalia kiliuumiza moyo wake, muda mwingi akawa mtu wa kujilaumu kwa kitendo chake cha kumfuata msichana huyo na kumtongoza.

Kwa upande wa Anna, bado moyo wake ulikuwa kwa Jafet, alimkumbuka mpenzi wake huyo, alimpenda zaidi ya mwanaume yeyote lakini kwa jinsi William alivyokuwa akizidisha ukaribu naye, akajikuta akianza kutekwa kimapenzi taratibu.

“Sitaki, sitaki kumsaliti Jafet,” alisema Anna huku akijitahidi kujiongelesha ili mawazo juu ya William ambayo yalianza kumuingia yaweze kumtoka.

Hiyo haikusaidia, maneno yake hayakusaidia kitu chochote kile, hakutaka kumuingiza mwanaume yeyote moyoni mwake lakini kitendo cha kuwa karibu na William, akajikuta akianza kumpenda mvulana huyo.

Siku iliyofuata, mtu wa kwanza kabisa kumfuata alikuwa William, mvulana huyo alifika mahali hapo na kumchukua kisha kuelekea sehemu maalumu ya kukaa kwa wanachuo na kuanza kuzungumza naye kama ilivyokuwa siku nyingine. Siku hiyo William hakutaka kugusia kitu chochote kuhusu mapenzi, alijitahidi kujikaza ili mradi tu asimlize msichana huyo.

“Anna, nashindwa kuvumilia,” alisema William, alikuwa akimwangalia msichana huyo usoni.

“Kwa nini?”

“Kwa jinsi ninavyokupenda…” alijibu William.

Hakuweza kuvumilia, moyo wake ulimsumbua na mwisho wa siku kujikuta akimwambia Anna jinsi alivyokuwa akimpenda. Siku hiyo alitumia uwezo wake wote kuzungumza na msichana huyo, alimshika mkono na kuuminyaminya kama njia mojawapo ya kuweka msisitizo juu ya kile alichokuwa akikizungumza.

Anna akaanza kumuelewa, hisia za kimapenzi zikaanza kumkamata kiasi kwamba kuna kipindi alishindwa kuongea zaidi ya kutoa miguno ya mahaba tu. William hakuacha, aliendelea kuzungumza huku akiubinyabinya mkono ule, Anna akashindwa kuvumilia, maneno aliyoongea William yakamuingia na hapohapo akajikuta akijisogeza karibu na William, kilichofuata, wakaanza kubusiana kimahaba, hakukuwa na mtu aliyeogopa macho ya watu waliokuwa wakipita.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply