Unending Love -44

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.

Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…K

umbukumbu za Jafet zikawa zimerejea upya ndani ya kichwa cha Anna, akaanza kulia kwa uchungu na kukimbilia kwenye hosteli aliyokuwa anaishi, akajifungia.

“Naendelea kukuomba msamaha Jafet, nilitamani ningekuwa karibu tushangilie pamoja ushindi huu lakini nasikitika kwamba nipo mbali, hayakuwa malengo yangu kuondoka na kukuacha kwenye hali hiyo, bado nakupenda mwenzio,” alisema Anna huku akiwa analia.

Muda mfupi baadaye, mama yake alimpigia Anna simu kwa lengo la kutaka kumpongeza kufuatia matokeo mazuri ya kidato cha sita aliyokuwa anayapata lakini akashangaa mwanaye akipokea simu huku akiwa analia.

“Unalia nini Anna, una tatizo?”

“Jafet mama.”

“Jafet amefanya nini?”

“Bila yeye nisingefaulu kwa kiwango cha juu namna hii. Kwa nini leo nimlipe ubaya mtu aliyeyabadilisha maisha yangu kwenye kila sehemu? Ameokoa maisha yangu kwa kunipa figo yake moja, amenisaidia pia kufaulu mtihani wangu wa kidato cha sita, naumia mama,” alisema Anna huku akiwa analia lakini kauli hiyo ilionesha kumchefua mno mama yake, akakata simu muda huohuo.

“Mume wangu, huyu mtoto amerogwa nini?”

“Vipi kwani?”

“Mimi nampigia simu kutaka kumpongeza kwa kufaulu yeye anaanza kunililia huku akimtaja huyo mshenzi wake.”

“Nani, Jafet?”

“Ndiyo, na nisivyompenda huyo Jafet hajui tu, yaani hata nikisikia jina lake nahisi kutapika. Anataka kuharibu maisha ya binti yetu, kwani sisi tumemlea ili aje kuolewa na maskini?” alisema mama yake Anna kwa dharau, japokuwa baba yake hakuwa anafurahishwa na hali hiyo, hakuwa na cha kusema zaidi ya kumuunga mkono mkewe.

***

“Mbona unalia mwanangu wakati matokeo yametoka na umefaulu vizuri? Kuna tatizo?”

“Nalia kwa furaha mama, nimefurahi sana kufaulu,” Jafet alidanganya kwani kiukweli kilichokuwa kinamliza ilikuwa ni kumbukumbu za Anna. Alijisikia vibaya sana kuona amefanya kila kitu, ikiwemo kuhatarisha mpaka uhai wake kwa sababu ya kumsaidia mtu ambaye leo anamgeuka na kuwa mwiba mkali kwenye moyo wake.

Japokuwa alimdanganya mama yake, mwanamke huyo aliweza kuelewa kilichokuwa kinamsumbua mwanaye. Kwa mara nyingine akatumia muda huo kuendelea kumjenga mwanaye kisaikolojia kwani ilionesha ameshindwa kukabiliana na kilichotokea.

Siku hiyo ilipita, maisha yakaendelea kusonga mbele lakini bado haikuwa kazi nyepesi kwa Jafet kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Ule uchangamfu na ucheshi wake vilipotea kabisa, muda wote akawa ni mtu wa kujiinamia na kujifungia peke yake chumbani kwake.

Hata muda wa maandalizi ya kujiunga na chuo kikuu ulipowadia, japokuwa alikuwa na sifa na vigezo vyote vya kupata nafasi chuo kikuu, hakuonesha kuwa na morali hata kidogo. Hakujishughulisha na chochote. Kwake maisha yalipoteza kabisa maana, akawa yupoyupo tu.

“Kwa hiyo kwa sababu huyo msichana wako amekukimbia ndiyo unaona hakuna hata sababu ya kuendelea kusoma tena? Unajua kabisa jinsi familia yetu ilivyo maskini, wewe ndiyo tegemeo letu na siku zote tumekuwa tukikuombea ili siku moja uje kubadilisha maisha ya hapa nyumbani, kwa nini unataka kutuangusha mwanangu?” mama Jafet alikuwa akizungumza na mwanaye jioni moja baada ya kupata chakula cha usiku.

Badala ya kujibu, Jafet alianza kulia kwa uchungu, mama yake akaendelea kumbembeleza na kumwambia kuwa anatakiwa kuwa makini kwani anavyoendelea kutumia muda mrefu kulia na kuhuzunika, anaweza kujisababishia madhara mengine makubwa zaidi.

“Wewe unajua kabisa kwamba tangu ufanyiwe upasuaji wa kutoa figo hata muda mrefu haujapita, sasa unavyokesha ukilia unataka tukupoteze na wewe?” alisema mama yake Jafet.

Alipotoa kauli hiyo, ni kama alimroga mwanaye huyo kwani siku moja baadaye, Jafet alianza kulalamikia maumivu makali ya kifua kwa ndani, hali iliyozua taharuki kubwa kwenye familia yake kwani walikuwa wanajua nini kitafuatia.

Kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo maumivu yalivyozidi kuwa makali kwa Jafet, ikafika mahali akawa hawezi kufanya chochote zaidi ya kushinda akiwa amelala huku akiugulia maumivu makali.

“Mume wangu, inabidi tuwapigie simu wazazi wa yule msichana ili watusaidie kumpeleka mtoto wetu hospitali kwani wao ndiyo waliosababisha awe hivi,” mama yake Jafet alikuwa akizungumza na mumewe.

Kutokana na matatizo yaliyokuwa yanamsumbua mtoto wao, baba yake Jafet ambaye alikuwa akifahamika kwa ulevi, alipunguza sana kwenda kulewa, muda mwingi akawa anashinda nyumbani na mkewe kwa ajili ya kumuangalia Jafet. Pale alipokuwa akizidiwa sana na kiu ya pombe, alikuwa akiwatuma wanaye waende kumnunulia.

Wazo lililotolewa na mkewe, wote waliliona kuwa la msingi sana, kwa kuwa hakuna aliyekuwa na simu kati yao, ilibidi watumie simu ndogo ya Jafet. Wakachukua namba ya simu waliyoachiwa na baba yake Anna na kujaribu kumpigia. Hata hivyo, simu ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.

Hata baada ya kujaribu kwa zaidi ya mara sita, bado majibu yalikuwa yaleyale, simu ilikuwa ikiita tu mpaka inakata bila kupokelewa.

“Sasa tutafanyaje na hali ya mtoto inazidi kuwa mbaya?” alihoji mama yake Jafet huku akianza kulengwalengwa na machozi, hakuna aliyekuwa na majibu ya nini cha kufanya.

***

“Mbona unaonesha kuwa na mawazo sana Anna jamani,” William alisema kwa sauti ya upole baada ya kumkuta msichana huyo mrembo akiwa amejiinamia kwenye ngazi za kuingilia kwenye hosteli aliyokuwa anaishi chuoni hapo, akionesha kuwa na mawazo yaliyopitiliza, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu kutokana na kulia kwa muda mrefu.

Ikabidi Anna avunge kwamba hakukuwa na chochote japokuwa uso wake ulikuwa ukionesha kila kitu. William akamshika mkono Anna na kumuinua pale alipokuwa amekaa, akamuomba wakanyooshe miguu kwenye bustani nzuri za maua chuoni hapo, Anna akakubali huku kijana huyo akijitahidi kadiri ya uwezo wake kumchangamsha.


Loading...

Toa comment