Unending Love, 48
Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno.
Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.
Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa lakini licha ya wema wake huo, wazazi wa Anna wanaonesha kutomkubali Jafet hasa baada ya kugundua kuwa alikuwa akitokea familia maskini.Kwa njama za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.
Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona na kujikuta akipata matatizo ya figo yake moja iliyosalia. Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa karibu.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Muda mfupi baadaye, sauti ya mhudumu wa uwanja huo wa ndege ilisikika ikiwataarifu watu wote kwamba ndege iliyokuwa ikitarajiwa kuwasili kutoka jijini Dar es Salaam, tayari imeshawasili jijini Mwanza na muda wowote itatua kwenye uwanja huo. Watu wote wakasimama na kuanza kujipanga, tayari kwa kuwapokea ndugu zao.
Dakika saba baadaye, lango kubwa la kutokea uwanjani hapo lilifunguliwa na abiria wakaanza kutoka, mapigo ya moyo ya Jafet yakawa yanaamuenda mbio kuliko kawaida, akiwa na shauku kubwa ya kumuona Anna.
Katika hali ambayo hakuitegemea, alishtuka mno kumuona Anna akitoka kwenye lango la kutokea, akiwa amekumbatiwa na kijana mmoja ambaye kwa kumtazama alikuwa akifanana sana na Wamarekani weusi kuanzia jinsi alivyokuwa amevaa na alivyokuwa anatembea.
Kwa jinsi alivyokuwa amemshika Anna kiuno, bila hata kuuliza, Jafet alijua kuwa lazima wawili hao ni wapenzi, akajikuta mwili wote ukiishiwa nguvu, kwa mbali akaanza kuhisi kizunguzungu, hali iliyosababisha atafute sehemu na kukaa ili asije akaanguka.
Pale alipokaa, aliweza kuendelea kuona kila kilichokuwa kinaendelea, alimuona jinsi Anna alivyokuwa na furaha kuungana tena na ndugu zake, akawa anakumbatiana nao mmoja baada ya mwingine huku pia akitumia muda huo kumtambulisha kijana wa kisasa aliyekuwa ameongozana naye.
Japokuwa Jafet alikuwa mbali, kwa jinsi alivyokuwa anamtazama Anna akimtambulisha kijana huyo, alielewa moja kwa moja kwamba lazima alikuwa akiwaambia ndugu zake kwamba huyo ndiyo mume wake mtarajiwa.
Akajikuta akishindwa kujizuia, machozi yakawa yanamtoka na kuulowanisha uso wake. Alijilaumu sana kwa uamuzi aliouchukua wa kufika uwanjani hapo kwani badala ya kuutibu moyo wake, alikuwa amejiongezea matatizo maradufu.
Aliendelea kuwatazama Anna na ndugu zake pamoja na yule mvulana ambaye kila alipojifananisha naye, aligundua kwamba mwenzake alikuwa amemzidi vitu vingi mno. Kwa kumtazama tu, alionesha kutokea kwenye familia bora tofauti kabisa na yeye, akazidi kuumia kwenye moyo wake.
“Kwa nini unanifanyia hivi Anna? Nimekukosea nini kustahili adhabu kali kiasi hiki?” Jafet alijisemea kwa sauti ya chini huku akiendelea kulia kwa kwikwi. Hali aliyokuwa akiihisi ndani ya moyo wake ilikuwa mbaya mno.
Baada ya mapokezi hayo ya kifalme, Jafet akiwa palepale alipokaa, aliwaona wote wakielekea kwenye magari mawili ya familia hiyo yaliyokuwa yamepaki kwenye maegesho uwanjani hapo, wakaingia na kuondoka kwa kasi, Jafet akawa anaendelea kulia kwa uchungu, kiasi cha kuwafanya watu waliokuwa jirani naye wapigwe na butwaa kwani ungeweza kuhisi amepokea taarifa za msiba.
***
Baada ya kutoka uwanja wa ndege, msafara wa mapokezi ya Anna ulienda moja kwa moja mpaka Capri Point, nyumbani kwao ambapo walimkuta baba yake akiwa amesharejea kutoka kazini kwa ajili ya kumpokea mwanaye huyo. Wakafanya sherehe ndogo ya kumkaribisha Anna nyumbani ambapo aliitumia nafasi hiyo kumtambulisha rasmi William kama rafiki yake kipenzi.
Wazazi wake walifurahi sana kumfahamu, wakazidi kumpenda hasa baada ya kutambulishwa kuwa ni mtoto wa balozi wa Tanzania nchini Marekani. Wakaubariki urafiki wao na kumsisitiza Anna kutulia kwani tayari alishampata mtu sahihi.
“Huyu ndiyo mnayeendana mwanangu, usifanye makosa kama kipindi kile,” alisema mama yake Anna, wazo lililoungwa mkono na wote. Anna na William wakakaa nyumbani hapo kwa siku tatu ambapo baadaye, William aliomba ridhaa ya kuondoka na Anna kuelekea nyumbani kwao, jijini Dar es Salaam kwa siku kadhaa kisha watarejea tena Mwanza.
Kwa jinsi Anna na William walivyoonesha kushibana, wazazi wake hawakuwa na kipingamizi, wawili hao wakajiandaa kisha wakaianza safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, kwenye makazi mengine ya familia ya akina William. Walisafiri kwa ndege na muda mfupi baadaye tayari walikuwa wameshawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kwa kuwa tayari William alishatoa taarifa kwa wafanyakazi wao, walikuta tayari kuna gari linawasubiri uwanja wa ndege ambalo liliwachukua hadi Masaki, ilipo nyumba ya kifahari ya familia hiyo ambayo huwa wanaitumia wakija Tanzania.
Japokuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Anna kufika jijini Dar es Salaam, safari hii alikuwa huru zaidi kwani alikuwa na mtu anayeifahamu vyema mitaa ya jiji hilo ambaye naye aliahidi kumtembeza kila sehemu aliyokuwa anaitaka.
“Nataka mpaka likizo ikiisha niwe nimeshafika kila sehemu maarufu hapa Dar,” alisema Anna wakiwa wamepumzika kwenye bustani ya maua, nje ya jumba la kifahari la akina William.
***
Kutokana na jinsi Jafet alivyoumizwa na kitendo cha kumuona Anna akiwa na mwanaume mwingine, aliamua kutafuta sehemu tulivu, akaenda kukaa kwenye mawe makubwa pembezoni mwa Ziwa Victoria na kuendelea kutafakari kilichotokea huku machozi yakiendelea kuulowanisha uso wake.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.