The House of Favourite Newspapers

Unending Love 51

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.

Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa karibu na sasa William amemlewesha Anna kwa lengo la kufanya naye mapenzi.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Alipomaliza boksi la pili, Anna alionesha kulewa chakari kiasi cha kulala na kuegamia meza, William akaachia tabasamu pana kwenye uso wake. Hakutaka kupoteza muda, akamuinua na kumkokota mpaka kwenye gari lake, harakaharaka wakaondoka eneo hilo kuelekea nyumbani kwa kina William.

Baada ya kuwasili nyumbani kwao, harakaharaka William alimkokota Anna mpaka ndani. Tofauti na makubaliano yao kwamba kila mmoja alale kwenye chumba chake, William alimpeleka Anna chumbani kwake, akatumia nafasi hiyo kutimiza azma yake.

Anna alikuja kushtuka usiku wa manane na kujikuta akiwa amelala mtupu, bila nguo hata moja, akashtuka mno kwani haikuwa kawaida yake. Alikurupuka pale kitandani na kutaka kuamka lakini maumivu makali katikati ya miguu yake, yalimfanya arudi pale kitandani.

Alipopeleka mkono kwenye ngome yake, hakuamini macho yake baada ya kukuta hali isiyo ya kawaida ikimaanisha kwamba William alikuwa amefanikisha malengo yake ya kufanya naye mapenzi.

“Mungu wangu,” alisema huku akijikokota na kuwasha taa, akapigwa na butwaa kumuona William naye akiwa amelala fofofo kitandani pale, akiwa kama alivyozaliwa.

“William! William, umefanya nini, umefanya niniiiii?” alisema Anna kwa sauti ya juu huku akimtingisha William kwa nguvu, kijana huyo akazinduka usingizini kichovu na kuinuka.

“Kwa nini umenifanyia hivi? Kwa niniii?” alisema Anna huku akianza kuangua kilio kwa nguvu, William akakosa cha kujibu zaidi ya kujiinamia. Anna aliendelea kulia kwa sauti ya juu bila kujali kwamba tayari ilikuwa ni usiku wa manane, ikabidi William aanze kumbembeleza.

Licha ya kutumia kila aina ya ushawishi kumtuliza, Anna hakutulia, akatoka na kwenda kujifungia kwenye chumba alichotengewa. Huku nyuma, ilibidi William abadilishe mashuka kwani yale ya awali yalikuwa hayatamaniki.

Miongoni mwa mambo yaliyomshangaza sana William usiku huo, ni kugundua kuwa licha ya urembo aliokuwa amejaliwa, Anna hakuwa akimjua mwanaume mpaka umri huo, moyoni akawa anajipongeza kwa ushindi alioupata.

Hakulala kabisa, muda wote akawa amejiinamia huku akiendelea kulia, hakuna kitu ambacho kilimfanya ajisikie vibaya kama kuingiliwa kimwili bila ridhaa yake. Kingine alimlaumu sana William kwa kitendo chake cha kumnywesha pombe huku akimdanganya kuwa ni juisi.

Kesho yake kulipopambazuka, William aliwahi kuamka na kuandaa kifungua kinywa, akaenda kwenye mlango wa chumba cha Anna na kuanza kugonga kwa upole na kumbembeleza afungue. Hata hivyo, Anna hakuwa mwepesi wa kufungua mlango, baada ya kumbembeleza sana, hatimaye alifungua.

Kwa kuwa William alikuwa anayajua makosa yake, William aliamua kujishusha kwa kila kitu, akampeleka mpaka sebuleni na kumkaribisha kifungua kinywa. Japokuwa Anna alikuwa na chuki kali ndani ya moyo wake kutokana na alichofanyiwa, kitendo cha William kuonesha kujutia kosa alilolifanya na kwa jinsi alivyokuwa anamjali, taratibu alijikuta akianza kumsamehe.

Siku hiyo ilipita huku William akiendelea na juhudi zake za kumbembeleza Anna, kesho yake ilibidi ampeleke kwenye Kisiwa cha Mbudya kilichopo kwenye Bahari ya Hindi, kilometa kadhaa kutoka Dar es Salaam, kama alivyomuahidi, akiamini kwa atakayoyaona huku, yatamfurahisha kiasi cha kumfanya asahau yote yaliyotokea.

Walitoka mpaka kwenye Hoteli ya Sea Cliff ambapo William alilipia gharama zote na safari ya kuelekea kwenye kisiwa hicho ikaanza. Walipelekwa na boti maalum mpaka kwenye kisiwa hicho ambapo walitumia muda mrefu kufurahi pamoja, wakicheza kwenye boti ndogo mfano wa pikipiki mpaka jioni ambapo walirejeshwa kwenye Hoteli ya Sea Cliff.

“Leo nataka tusirudi nyumbani, nataka tulale hapahapa hotelini,” alisema William, wazo ambalo Anna alilikubali lakini kwa sharti moja kwamba kila mmoja alale kwenye chumba chake, William akakubaliana naye bila kinyongo chochote.

“Naomba ninunulie tena ile pombe ya kwenye boksi kama jana, ila leo sitaki kulewa,” alisema Anna, wazo ambalo lilimfurahisha mno William kwani aliamini itakuwa rahisi kumshawishi Anna akubali walale tena kitanda kimoja.

Baada ya kula chakula cha jioni, wawili hao walikaa sehemu tulivu ndani ya hoteli hiyo ya kifahari, wakawa wanapiga stori za hapa na pale huku wakiendelea kupata vinywaji taratibu. Baada ya kumaliza mvinyo uliokuwa kwenye boksi, Anna alichangamka mno, zile aibu za kikekike alizokuwa nazo awali ziliyeyuka kabisa.

Hata William alipotaka kumbusu, alimruhusu bila tatizo, wakawa wanaendelea kufanyiana vituko vya kimahaba vya hapa na pale. Muda wa kulala ulipofika, William alimuomba Anna ambaye tayari kilevi kilishakolea kichwani wakalale pamoja. Kama alivyokuwa amehisi mwanzo, japokuwa Anna mwanzoni alileta ubishi, alipoendelea kumbembeleza, alikubali na kwa mara nyingine, wawili hao wakafanya mapenzi, safari hii Anna akiwa ameridhia mwenyewe.

Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

 

Leave A Reply