Unending Love -58
Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.
Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.
Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.
Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inaanza. Upande wa pili, Suleikha anazidi kumganda Jafet kama ruba.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Japokuwa mwenyewe hakuwa ameamua kuanzisha rasmi uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo, Suleikha alionesha kumpenda mno Jafet. Hakujali uzuri wa kipekee aliokuwa amejaliwa, japokuwa wanaume wengi chuoni hapo walikuwa wakimtongoza, mwenyewe aliamua kuwa karibu na Jafet akiamini lazima ipo siku atakubali kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi.
Kila Jafet alipokuwepo, lazima Suleikha alikuwa pembeni yake, ndani ya kipindi kifupi tu tangu walipokutana, tayari watu wengi walikuwa na uhakika kwamba wawili hao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi.
“Mbona leo unaonekana kuwa na mawazo sana? Nini kinachokusumbua Jafet?” Suleikha alimuuliza Jafet kwa sauti ya upole wakiwa wamekaa kantini baada ya kugundua kwamba hakuwa kwenye hali yake ya kawaida.
“Kuna jambo linanisumbua sana ndani ya kichwa changu Suleikha.”
“Mimi si nipo jamani, kwa nini usiniambie kinachokusumbua? Naweza kukusaidia japo kwa ushauri Jafet, please talk to me! (Tafadhali zungumza na mimi).”
“Hapana Suleikha, nitakuwa nakubebesha mzigo mzito usiostahili,” alisema Jafet huku akigeukia pembeni lakini Suleikha hakutaka kumuelewa, akamsogelea na kuendelea kumsihi amueleze kilichokuwa kinamsumbua.
“Ni stori ndefu kidogo Suleikha,” alisema Jafet huku akikaa vizuri kwenye kiti pale kantini. Akaanza kumsimulia msichana huyo kuanzia siku ya kwanza alipokutana na Anna, kipindi hicho akiwa mwanafunzi wa sekondari.
Alimueleza kila kitu kilichofuatia, jinsi alivyojikuta akiangukia kwenye penzi zito la msichana huyo bila kujali kwamba walikuwa wakitoka kwenye familia mbili tofauti, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri wakati Jafet akitokea kwenye familia ya kifukara kupindukia.
Aliendelea kumueleza jinsi alivyoamua kuvunja kiapo chake cha kwenda kusomea upadri mara baada ya kukutana na msichana huyo, jinsi mapenzi yao yalivyoshamiri mpaka msichana huyo alivyoanza kusumbuliwa na figo.
“Nilifikia hatua ya kumtolea figo yangu moja, hapa unaponiona nina figo moja ndiyo maana kuna kipindi nilikuwa naumwa sana, lakini hayo yote yeye na familia yake hawakujali,” alisema Jafet na alipofikia hatua hiyo, alishindwa kuzuia hisia zake, machozi mengi yakawa yanamtoka na kulowanisha uso wake.
“Pole, usilie Jafet, jikaze! Kila jambo linakuja kwa sababu maalum,”
alisema Suleikha kwa upole, Jafet akajifuta machozi na baada ya dakika kadhaa, aliendelea kuelezea kilichofuatia.
Alieleza jinsi Anna alivyoondoka na kwenda kusoma nje ya nchi bila hata kumuaga na jinsi Jafet alivyoumia siku aliyosikia kwamba anarejea nyumbani na kwenda kumpokea uwanja wa ndege.
“Nikiwa namsubiri kwa hamu baada ya kutoonana kwa muda mrefu, sikuamini macho yangu kumuona anatoka uwanja wa ndege akiwa amekumbatiana kimahaba na mwanaume mwingine, siwezi kuelezea maumivu niliyoyahisi na kuanzia siku hiyo nikajiapiza kwamba siwezi tena kurudiana na Anna, hata iweje,” alisema Jafet, akajiinamia kwa dakika kadhaa huku machozi yakiendelea kumtoka.
“Sasa huku Dar amefuata nini na kwa nini alikuwa anakupigia magoti barabarani huku akilia?”
“Anasema anahitaji kuzungumza na mimi, nikamkatalia na kumwambia hakuna chochote anachoweza kuzungumza na mimi, sitaki hata kumuona.”
“Pole sana Jafet, nipo kwa ajili yako na naahidi nitakuwa pembeni yako katika kipindi hiki kigumu unachopitia kwa sababu nakupenda kuliko kitu kingine chochote chini ya jua,” alisema Suleikha na kumkumbatia Jafet kwa nguvu huku naye machozi yakimtoka.
Walibaki wamekumbatia kwa zaidi ya dakika tatu huku ukimya ukiwa umetawala kati yao, mapigo ya moyo ya kila mmoja yakawa yanasikika vizuri kwa mwenzake.
“Kwa hali uliyonayo, naomba jioni ya leo nikuoneshe kitu kingine tofauti kabisa, naamini utafurahi,” alisema Suleikha huku akijitoa kwenye kifua cha Jafet, kijana huyo akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na alichokuwa anakisema msichana huyo mrembo.
Suleikha alienda kwenye meza ya wahudumu na kuagiza chakula kwani licha ya kufika muda mrefu uliopita, bado hawakuwa wameagiza chakula. Muda mfupi baadaye, chakula kililetwa mezani walipokuwa wamekaa, akaanza kumbembeleza Jafet kula kwani alionesha kupoteza kabisa hamu ya kula.
Jafet alikula kwa shida kisha baada ya hapo, Suleikha akamshika mkono na kumuinua, wakaondoka taratibu mpaka sehemu palipokuwa pakiuzwa vinywaji, nje kidogo ya eneo la chuo.
“Umeshawahi kunywa ‘wine’?”
“Hapana, sijawahi, vipi kwani.”
“Nataka leo unywe japo kidogo kwa ajili yangu.”
“Hapana Suleikha, si nimeshakwambia mwenzio nina figo moja? Siwezi kuhatarisha afya yangu, utanisamehe kwa hilo.”
“Kwani nani alikwambia ukiwa na figo moja hutakiwi kunywa? Unakuwa utafikiri siyo daktari bwana! Mhudumu tuletee Red Cape chupa moja na glasi mbili,” alisema Suleikha, muda mfupi baadaye mhudumu akawaletea chupa kubwa ya mvinyo mwekundu na glasi mbili. Akawamiminia na kuwakaribisha.
“Wala haileweshi sana, kunywa upunguze mawazo, utajisikia vizuri usijali,” alisema Suleikha, akanyanyua glasi yake na kugongesheana ‘cheers’ na Jafet, wakaanza kunywa taratibu.
Kwa kuwa Jafet hakuwahi hata mara moja kunywa pombe maishani mwake, alipomaliza glasi moja tu, tayari alianza kuonesha kuchangamka kuliko kawaida. Ule msongo mkubwa wa mawazo uliokuwa ukimsumbua, uliyeyuka kama barafu iyeyukavyo juani, tabasamu pana likaupamba uso wake.
“Hivi Jafet, ukiniangalia mimi na huyo Anna wako nani mzuri zaidi?”
“Wewe ni mrembo zaidi Suleikha. Unajua kabla sijakufahamu nilikuwa naamini hakuna mwanamke mrembo kama Anna lakini kumbe nilikuwa najidanganya,” alisema Jafet huku akionesha kuanza kukolea kwa kilevi.
“Mbona hujawahi kunisifia hata mara moja? Halafu kama kweli mimi ni mzuri, mbona hujawahi kuniambia kama unanipenda? Au sikuvutii?” alisema Suleikha kwa sauti ya upole, akamsogelea Jafet pale alipokuwa amekaa na kumkumbatia huku akimwagia mvua ya mabusu, Jafet akawa anachekacheka tu mwenyewe, tofauti na siku nyingine zote ambapo msichana huyo alikuwa kila akijaribu kumbusu, alikuwa anamtoa mwilini mwake.
“Unajua Suleikha mimi naogopa kuingia tena kwenye uhusiano wa kimapenzi. Nilimpenda sana Anna lakini kwa alichonifanyia, naona kama wanawake wote mpo sawa.”
“Mimi niko tofauti Jafet, nakuhakikishia hutajuta kunifahamu,” alisema Suleikha na kuendelea kumfanyia Jafet vituko vya hapa na pale. Akamwambia kwamba amemfurahisha sana kwa kitendo chake cha kukubali kunywa wine, akamtaka waongozane pamoja mpaka kwenye hosteli aliyokuwa anaishi msichana huyo.
“Kufanya nini tena muda huu? Huoni tayari ni usiku?”
“Nataka nikakupe zawadi ambayo nimeitunza kwa muda mrefu. Sikupanga kumpa mtu yeyote kwa sasa lakini naamini wewe ndiye unayestahili kupewa, nimekufuatilia kwa kina na nimejiridhisha kwamba unastahili,” alisema Suleikha huku na yeye akionesha kuchangamka baada ya mvinyo kumkolea kichwani. Akamshika mkono Jafet na kuondoka naye huku akimvuta, kila mtu akawa anawashangaa.
Walienda moja kwa moja mpaka hosteli, wakapitiliza mpaka kwenye chumba alichokuwa anaishi Suleikha, akamkalisha Jafet juu ya kitanda kisha akaenda kufunga mlango kwa funguo, Jafet akawa ametulia kama kondoo anayesubiri kuchinjwa.
“Unajua kwa nini nimekuleta huku?” alisema Suleikha huku akimsogelea Jafet pale alipokuwa amekaa kwa mwendo wa maringo utafikiri mwanamitindo wa kimataifa, Naomi Campell. Jafet hakujibu kitu zaidi ya kutingisha kichwa huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Suleikha akamvamia mwilini na kumkumbatia kimahaba, kufumba na kufumbua wakagusanisha ndimi zao mithili ya njiwa anayemlisha kinda wake.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.
Comments are closed.