The House of Favourite Newspapers

Unending Love-68

2

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet akaletwe ili amueleze kilichokuwa ndani ya moyo wake. Hali hiyo inasababisha baba yake Anna afunge safari mpaka jijini Dar es Salaam kumfuata Jafet.

Anampeleka kwa wazazi wake ambao baada ya mvutano mkubwa wanamruhusu. Hatimaye wanaondoka pamoja jijini Mwanza mpaka Dar es Salaam wakiwa njiani kuelekea India. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Muda umeisha Jafet,” alisema baba yake Anna, kauli hiyo ndiyo ikamzindua kutoka kwenye hali aliyokuwa nayo, akajitoa kwenye mikono ya Suleikha na kumbusu kwenye midomo yake kisha akamalizia kwenye paji lake la uso. Akaondoka na kumuacha Suleikha akiendelea kulia kwa uchungu. Waliingia kwenye teksi na safari ya kuelekea uwanja wa ndege ikaanza.

Njia nzima Jafet alionesha kuwa na mawazo lukuki. Hakuna aliyemsemesha mwenzake, safari iliendelea kimyakimya mpaka walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakateremka kwenye teksi na kuingia kwenye jengo kubwa uwanjani hapo ambapo walijipanga kwenye foleni kama abiria wengine.

Baada ya shughuli za ukaguzi kukamilika, waliingia mpaka ndani ambapo walifanyiwa ukaguzi wa mara ya pili na kwenda kwenye chumba maalum cha abiria, wakaungana na abiria wengine wengi waliokuwa wakisafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani.

“Unaonekana kuwa na mawazo sana Jafet, nini kinachokusumbua?”
“Aah! Kawaida tu,” alisema Jafet huku akijitahidi kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
“Unajua ukishazaliwa mwanaume ujue kuna mitihani mingi sana hapa duniani inakusubiri na ili kusonga mbele ni lazima uipitie yote, huna haja ya kuogopa chochote, jiamini kwa sababu maisha ya Anna yapo mikononi mwako.

“Nakuombea kwa Mungu akupe busara katika kipindi hiki kigumu, najua jinsi unavyojikuta kwenye wakati mgumu wa kuamua ukiwafikiria Anna na Suleikha lakini naamini haya yote yatapita na maisha yataendelea kama kawaida,” alisema baba yake Anna huku akimpigapiga kijana huyo mgongoni.

Jafet alishusha pumzi ndefu na kumtazama baba yake Anna usoni, alichokizungumza ni kama alikuwa ameona kilichokuwa kinaendelea ndani ya nafsi yake. Ni kweli alikuwa kwenye wakati mgumu sana na hakuelewa moyo wake unampenda nani hasa.

Ni kweli kwamba alikuwa akijisikia amani sana ndani ya moyo wake anapokuwa na Suleikha na yeye ndiye aliyemtoa kwenye hali ya huzuni aliyodumu nayo kwa kipindi kirefu tangu alipotendwa na Anna.

Hata hivyo, alikuwa haelewi kwa sababu gani anaposikia habari za matatizo ya Anna zinamgusa sana moyo wake na kumfanya atamani hata angekuwa na uwezo wa ziada ili aweze kumponya kutoka kwenye maradhi yaliyokuwa yanamtesa.

“Umenielewa Jafet!”
“Nimekuelewa baba,” alisema Jafet huku akitingisha kichwa. Sauti ya mhudumu wa uwanja huo ndiyo iliyowazindua wawili hao kutoka kwenye mazungumzo. Mhudumu huyo wa uwanjani hapo, alikuwa akiwataarifu abiria waliokuwa wakitegemea kusafiri na ndege ya Qatar Airways kuelekea nchini India kwa kupitia Doha, Qatar, kuanza kujiandaa kuelekea kwenye ndege.

Jafet na baba yake Anna waliinuka na kuongozana na abiria wengine mpaka upande ndege zilipokuwa zinaegeshwa, wakaingia kwenye basi maalum la uwanjani hapo lililowapeleka mpaka kwenye ngazi za kuingilia kwenye ndege, wakateremka kwenye basi na kupanda ngazi za kuelekea ndani ya ndege.

Dakika kadhaa baadaye, ndege ilianza kuondoka uwanjani hapo, ikaongeza kasi na muungurumo wa injini ukazidi kuwa mkubwa, hatimaye ikapaa na kupotelea mawinguni.

Baada ya safari ndefu iliyochukua zaidi ya saa nane, hatimaye waliwasili nchini India na bila kupoteza muda, baada ya taratibu zote za kiusalama kukamilika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji, Jafet na baba yake Anna walitoka na kukodi teksi iliyowapeleka mpaka Hospitali ya Apollo alikokuwa amelazwa Anna.

Kitendo cha kumuona mumewe amerejea, tena akiwa ameongozana na Jafet, kilimfanya mama yake Anna ashindwe kuyazuia machozi ya furaha kumtoka. Akamkimbilia mumewe na kumkumbatia kwa nguvu huku akimbusu kwenye paji lake la uso kwa hisia kali, machozi mengi yakiendelea kumtoka.

“Ahsante kwa kukubali kuja, Mungu atakulipa kwa haya yote unayotufanyia,” alisema mama yake Anna wakati akipeana mkono na Jafet aliyemwamkia kwa adabu.
“Mwanangu yuko wapi?”

“Ameingia kwenye Dialysis saa tatu zilizopita, nafikiri atakuwa anakaribia kutoka,” alisema mama yake Anna huku akiendelea kumkumbatia mumewe na kumbusu. Furaha aliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki. Uwepo wa Jafet eneo hilo ulimhakikishia kwamba mwanaye atakuwa salama.

Kwa kuwa muda ulikuwa haujafika wa Anna kutoka kwenye tiba ya Dialysis, ambapo mzunguko wake wa damu ulikuwa ukiunganishwa kwenye mashine maalum iliyokuwa inafanya kazi sawa na figo, ilibidi baba yake Anna aondoke na Jafet hospitalini hapo na kumpeleka kwenye hoteli aliyokuwa amemkodia chumba.

“Pumzika kidogo nitakuja kukuchukua muda si mrefu,” alisema baba yake Anna, akatoka na kumuacha Jafet akijiandaa kwenda kuoga ili kupunguza uchovu wa safari. Baada ya kumaliza kuoga, alijitupa kitandani na kupumzika huku mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa chake.

Alikumbuka maneno ya baba yake Anna ya kumtaka kujitahidi kumuonesha mapenzi Anna hata kama walikuwa na tofauti kati yao. Kumbukumbu za mambo mazuri waliyowahi kuyafanya pamoja zikawa zinajirudia ndani ya kichwa chake kama mkanda wa video. Kumbukumbu hizo ziligota siku aliyokuwa anamsubiri Anna Uwanja wa Ndege wa Mwanza na katika hali ambayo hakuitegemea, akamuona akitoka akiwa amekumbatiana kimahaba na mwanaume mwingine.

“No! It can’t be! Why did you leave me in a time when i was in need of you the most?” (Hapana! Haiwezekani! Kwa nini uliniacha katika kipindi nilichokuwa nakuhitaji sana?) Jafet alijikuta akitamka kwa sauti na kusimama, akawa anazunguka huku na kule ndani ya chumba hicho.

Mlango uliokuwa unagongwa ndiyo uliomzindua kutoka kwenye hali hiyo, harakaharaka akaenda kufungua na kukutana uso kwa uso na baba yake Anna.

“Ameshatoka, twende,” alisema. Bila kupoteza muda waliongozana mpaka hospitalini ambapo Anna hakuyaamini macho yake kumuona Jafet mbele ya macho yake. Jafet akamsogelea pale kitandani na wawili hao wakakumbatiana kwa nguvu huku machozi yakimtoka kila mmoja.

“Nisaidie niinuke hapa kitandani tukakae nje, nina mazungumzo muhimu sana na wewe,” alisema Anna, Jafet akawageukia wazazi wa msichana huyo ambao walitingisha vichwa vyao kumkubalia. Akamsaidia kuinuka na wakatembea taratibu mpaka nje ya wodi hiyo, wakakaa kwenye benchi huku ukimya ukiwa umetawala kati yao.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

2 Comments
  1. mwanaidy ramso says

    ai see japhet akirudiana na anna itakuwa pw sana kwan hakuna binadamu aliyekamilika na anna anampenda japhet sana

  2. dorah fredy says

    MMmmmmmmh sijui ila jafet usimwache Sulekhi

Leave A Reply