Unending Love (Penzi Lisiloisha)-56
Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.
Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.
Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna anaanza kuona dalili zisizo za kawaida. Anapoenda kupima anagundulika ni mjamzito lakini kijana huyo anaonesha kukasirishwa na hali hiyo, anataka wakautoe ujauzito huo.
Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila Jafet kujua chochote lakini akiwa anaelekea uwanja wa ndege, anakutana na Jafet katika mazingira ambayo hakuyategemea. Hata hivyo, Jafet anakataa kumuonesha ushirikiano kama mwenyewe alivyotegemea.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Bado akilini mwake, Anna aliendelea kubabaika kufikia uamuzi wa kurudi nyumbani kwao, Mwanza au kuahirisha safari na kujaribu kwa mara nyingine kutafuta nafasi ya kuzungumza na Jafet. Mpaka wanawasili uwanja wa ndege, bado Anna hakuwa na majibu kama aendelee na safari au arudi kwenda kuzungumza na Jafet.
Hata hivyo, alipofikiria ujauzito aliokuwa nao, alijikuta akikosa cha kufanya zaidi ya kurudi nyumbani kwao Mwanza.
“Nisamehe Jafet! Ni kweli nilikukosea lakini nahitaji msamaha wako, bado nakupenda mwenzio,” Anna alijisemea mwenyewe akiwa ndani ya teksi. Hakuwa na habari kwamba tayari ameshafika mwisho wa safari yake mpaka dereva wa teksi hiyo alipomzindua kutoka kwenye lindi la mawazo machungu.
“Dada hapa si ndiyo uwanja wa ndege? Au sikukusikia vizuri unakoenda?”
“Ooh! Samahani kaka yangu, niko mbali sana kimawazo,” alisema Anna huku akifungua pochi yake ndogo na kutoa nauli, akamlipa dereva huyo ambaye alimsaidia kuteremsha mizigo yake na kuisogeza mpaka kwenye jengo kubwa la uwanja wa ndege.
Huku akionesha kuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake, Anna alianza kuburuza begi lake kuelekea kwenye ofisi za shirika la ndege aliyopanga kusafiri nayo, akahakikishiwa kwamba amewekewa nafasi kama alivyoomba kisha baada ya hapo akajipanga kwenye foleni sambamba na abiria wengine kwa ajili ya ukaguzi.
Muda mfupi baadaye, tayari Anna alikuwa ameshakaguliwa, akaingia ndani ya ukumbi maalum uwanjani hapo na kuungana na abiria wengine kusubiri ndege ya kuelekea Mwanza.
Akiwa ndani ya ukumbi huo, Anna aliendelea kutokwa na machozi kwa wingi kama mtu aliyepokea taarifa za msiba. Hakutaka kuamini kwamba ndani ya kipindi kifupi tu maisha yake yalikuwa yameharibika kiasi hicho na kupoteza kabisa mwelekeo. Kilichozidi kumchanganya kichwa chake ilikuwa ni ujauzito aliokuwa nao na jinsi atakavyoenda kuwaeleza wazazi wake.
Taswira za tukio la kukutana na Jafet ana kwa ana katika mazingira ambayo hakuyategemea kabisa na kilichofuatia baada ya kukutana naye, zilikuwa zikijirudia ndani ya kichwa cha Anna mithili ya mkanda wa video wa kusisimua.
Kila alipomfikiria msichana mrembo aliyekuwa akisumbuana na Jafet, akionesha kumpenda sana kiasi cha kumuonea wivu uliopindukia, alijikuta akiumia sana ndani ya moyo wake. Alitamani siku zirudi nyuma ili arekebishe makosa yaliyotokea kwani Jafet hakustahili kulipwa ubaya kiasi hicho, hasa kutokana na ukweli kwamba alijitolea maisha yake ili kumuokoa Anna.
“Mama ndiyo amesababisha yote haya! Yeye ndiyo chanzo cha yote, sikubali,” alisema Anna kwa sauti ya juu, hali iliyowashangaza abiria wengine waliokuwa wamekaa naye jirani.
“Vipi binti kuna tatizo?” mzee wa makamo aliyekuwa amekaa pembeni yake, alimuuliza Anna huku akiwa amemkodolea macho.
“Hamna, kawaida tu mzee,” alisema Anna huku akijifuta machozi ambayo yalikuwa yameulowanisha kabisa uso wake. Muda mfupi baadaye, sauti ya mhudumu wa uwanja huo ilisikika kwenye vipaza sauti ikiwataarifu abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri kuelekea Mwanza, kuanza kujiandaa kuelekea kwenye ndege, tayari kwa safari.
Anna akaungana na abiria wengine na kupita kwenye geti la pili kisha wakapanda kwenye basi maalum uwanjani hapo lililowapeleka mpaka jirani kabisa na ndege, wakateremka na kupanda ngazi za kuingia kwenye ndege. Anna akaenda mpaka kwenye siti yake na kutulia, mawazo mengi yakawa yanaendelea kukisumbua kichwa chake.
Wakati abiria wengine wakiendelea kuingia ndani ya ndege na kwenda kukaa kwenye siti zao, simu ya Anna ilianza kuita mfululizo, akafungua pochi yake ndogo na kuitoa, akawa anatazama namba ya mpigaji, hakuwa mwingine bali William.
Kwa yote aliyofanyiwa na kijana huyo, Anna hakuwa hata na hamu ya kuzungumza naye kwani aliona kama amemharibia kabisa maisha yake wakati hana mapenzi ya kweli kutoka ndani ya moyo wake. Simu iliita mpaka ilipokata, Anna akaamua kuizima kabisa kwani hakutaka kabisa kuzungumza na William.
Muda mfupi baadaye, safari ilianza, ndege ikapaa na kuiacha ardhi ya Dar es Salaam, ikawa inapasua mawingu kuelekea jijini Mwanza. Takribani dakika hamsini baadaye, sauti ya mhudumu wa ndege hiyo aliwataarifu abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Dakika kadhaa baadaye, ndege tayari ilikuwa imeshatua na kusimama mbele ya jengo la uwanja huo, abiria wakaanza kuteremka, akiwemo Anna ambaye kutokana na kulia kwa muda mrefu, macho yake yalikuwa yamevimba na kubadilika rangi na kuwa mekundu.
Kwa kuwa hakuwa amempa taarifa mtu yeyote kuhusu safari yake hiyo, hakukuwa na mtu wa kumpokea uwanjani hapo, akatoka na kukodi teksi iliyompeleka mpaka nyumbani kwao, Capri Point. Alipofika getini kwao, alimuelekeza dereva kusimama, akamlipa fedha zake na kushuka, akatembea kinyonge na kwenda kugonga geti.
Mlinzi aliyemfungulia alikuwa mtu wa kwanza kugundua kwamba Anna hakuwa sawa, akajaribu kumdadisi kama alikuwa anaumwa lakini msichana huyo alikataa kutoa ushirikiano wowote, akaingia ndani ambako alipokelewa na mama yake aliyeonesha kushtushwa na ujio wa ghafla wa binti yake, akaacha kila alichokuwa anakifanya na kumsogelea Anna, akimtazama kwa macho yaliyojaa udadisi.
Kitendo cha kumuona mama yake mbele yake, kilimfanya Anna aanze kuangua kilio mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba, mama yake akamkumbatia na kuanza kumbembeleza huku akimsihi atulie na kumueleza kilichomtokea.
Baada ya mama yake Anna kutumia dakika kadhaa kumtuliza binti yake huyo, hatimaye Anna alitulia na kuanza kueleza kilichomsibu.
“Mungu wangu! Anna umepata ujauzito?”
“Ni bahati mbaya mama, sikuwa nimepanga.”
“Mhusika ni nani?”
“William.”
“Unasemaaa? Haiwezekani, nasema haiwezekani,” alisema mama yake Anna huku akizunguka huku na kule ndani ya sebule yao ya kifahari kama mwendawazimu. Taarifa hizo zilimchanganya mno.
JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS


