The House of Favourite Newspapers

Uongo unasaidia kudumisha penzi?

0

Womanwithmobilephone.jpgKWA wale walioguswa na mada ya wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa kisemacho ‘Unampenda mtu wa mtu ili iweje’ nawashukuru kwa kunitumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) za pongezi. Nina hakika mlipata elimu kupitia mada ile na sasa karibuni tupate elimu mpya yenye kichwa cha habari hapo juu.

Ukichunguza kwa makini kwa kizazi cha sasa utagundua, wanaume wengi wanaamini katika uongo. Wanaamini kwamba mwanamke ni mtu wa kudanganywa. Ukimueleza ukweli ni tatizo hivyo ni bora umwambie uongo ili mambo yaende.

Kwamba, mwanamke ukimwambia ukweli, kama hujampata basi huwezi kumpata na hata kama akiwa tayari ni wako, penzi haliwezi kudumu. Yaani kama unataka penzi lidumu, kamwe usimueleze mpenzi wako ukweli.

Wanaume wanaofikiri hivyo huwa wanakuwa na hoja zao. Ukiwaambia wakupe mifano, watakupa mifano lukuki ya wenzao ambao waliongea ukweli kwa wanawake wao na kujikuta wakiangukia pua. Hata wanawake pia, wapo ambao wana ‘ugonjwa’ huo.

Mwanamke anaamini kwamba ili adumu na mwanaume, asimueleze ukweli. Asimpe siri ya maisha yake. Eti atakuwa amempa silaha ya kumnyanyasa. Anaamini kwamba akimueleza ukweli mwanaume wake basi ni rahisi kukosa vitu fulanifulani ikiwemo fedha na mahitaji mengine.

Hapo ndipo uongo unapohalalishwa kwa pande zote mbili. Mbaya zaidi kila mmoja anajipa uhalali wa uongo. Mwanaume anaamini kwamba uongo ni mali yake lakini mpenzi wake hapaswi kuwa muongo. Vivyo hivyo kwa mwanamke, anaamini uongo ni halali yake hivyo mwanaume anapaswa kuzungumza ukweli.

Kila mmoja anataka adanganye yeye lakini akigundua mwenzake anamdanganya ni tatizo. Anasahau kabisa kwamba yeye pia huwa anadanganya. Mwanaume anabadilisha maana ya uongo kwamba ule wa kwake una manufaa lakini wa mwenzake anauona hauna manufaa.

Ndugu zangu hapo kwanza tunapaswa kuelewa kwamba uongo una madhara zaidi kuliko ukweli. Unaweza kudumu kwenye uongo kwa muda mrefu lakini siku mwenzako akibaini kwamba ulikuwa unamdanganya, mtagombana.

Kugombana huko kunaweza kukawa kwa kawaida au mnaweza kufikia hatua ya kuachana kabisa. Kwa nini usimueleze ukweli? Utaficha makucha hadi lini? Kama mtu umeshamchunguza kwamba anapenda watu wa aina f’lani na wewe huna hizo sifa, kwa nini umuongopee?

Kwa nini umfurahishe kwa uongo wakati nafsi yako inajua ukweli? Uongo siku zote huwa haumfanyi mtu kuwa huru. Muda wote utakuwa na shaka. Utaishi kwa kupangilia maneno kila siku. Eti unaishi kwa shaka kuhofia kwamba mambo yasije yakabumburuka muda wowote si kitu kizuri.

Eti utakuwa mtu wa kujihami. Kwamba hata unapozungumza jambo mahali lazima uwe na uhakika kwamba unaozungumza nao hawana mawasiliano na mpenzi wako? Maisha gani hayo. Ili muwe na maisha marefu katika uhusiano, kila mmoja anapaswa kuwa mkweli.

Mwanaume unatakiwa kuwa mkweli. Unatakiwa kuchagua mwanamke ambaye atakubaliana na ukweli. Mueleze ukweli ili akubaliane nao. Hakuna haja ya kudanganya. Utadanganya mpaka lini? Ni rahisi kudumu kwenye ukweli kuliko uongo. Njia ya muongo siku zote ni fupi.

Ukitumia uongo ili kukamilisha uhusiano wako ni dhahiri hata huyo anayekubaliana na uongo naye si mtu sahihi. Maana ungemfuata bila kumuonesha uongo, asingekubali. Mwanamke naye anapaswa kuwa mkweli ili kujenga imani kwa mpenzi wake.

Mkiwa wakweli mtasomana vizuri tabia zenu. Mtajuana hali zenu. Mtapanga mipango mizuri ya kufikia kilele cha mafanikio ya uhusiano wenu. Ni matumaini yangu wapenzi wa safu hii mtakuwa mmenielewa.

Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

Leave A Reply