The House of Favourite Newspapers

UPANDE WA MASHTAKA WAAMRIWA KUTOA MAJIBU KESI YA VIGOGO WA UTHAMINI MADINI

Vigogo wawili wa uthamini wa madini ya Almasi wa Serikali wanaotuhumiwa wakifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo kusikiliza kesi inayowakabili.

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi  inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya Almasi wa Serikali kwamba ifikapo Mei 21 mwaka huu kuhakikisha wanatoa jibu kuhusu hatua ya upelelezi wa kesi hiyo ulipofikia.

 

Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbad Mashauri baada ya Wakili wa Serikali, Saada Mohammed kudai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado  haujakamilika na kwamba jalada lipo  kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).

 

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Nickson Ludovick,  amedai walitegemea  upande wa mashtaka wangeiambia Mahakama ni lini wataendelea na kesi hiyo kwa sababu hapo awali walisema upelelezi ulishakamilika.

 

Ameiomba Mahakama imwamuru (DPP) aseme lini kesi hiyo itaendelea kwa sababu katika kumbukumbu za mahakama  zinaonyesha kesi ilishakuwa tayari kwa kuanza kusikilizwa.

 

Wakili wa Serikali Elia Athanas akijibu hoja hiyo alidai jalada bado linashughulikiwa katika sehemu ambazo hazipo sawa na hakuna uzembe wowote unaofanywa na ofisi ya (DPP).

 

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Hakimu Mashauri ameamuru upande wa mashtaka ifikapo Mei 21, mwaka huu, kuja na majibu sahihi kuhusu hatua ya upelelezi ilipofikia.

 

Washtkiwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania  (Tansort) Archard Kalugendo na mthamini almasi wa serikali, Edward Rweyemamu.

 

 

Na Denis Mtima/Gpl.

Comments are closed.