Upendo unavyoweza kugeuka silaha kwa adui yako!
Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo mengine tunaelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kila siku.
Mpenzi msomaji wangu, leo nitazungumzia upendo unavyoweza kuwa silaha kwa adui yako ambaye mara nyingi amekuwa akikupa hofu na wakati mwingine kuhisi ana dhamira ya kukufanyia mabaya.
Nimeamua kuandika makala haya baada ya kuona na kusikia kesi nyingi juu ya watu kuishi maisha yaliyojaa hofu ya kudhurika kwa visasi na vijicho vya wabaya wao.
Hakuna ubishi katika mtazamo wa dunia kwamba kuna maisha chanya na hasi ambayo yanamzunguka mwanadamu. Lakini ugumu anaoupata mwanadamu na pengine ndiyo ambao nataka kuuzungumzia leo ni jinsi gani anaweza kuishi ndani ya mambo mema na mabaya.
Kama kilivyo kichwa cha habari hapo juu, leo nimeona nijikite zaidi katika kutoa elimu ya namna ya kujikinga na kumshinda mtu anayetaka kukuangamiza. Labda nitaje dhana tu ambazo zinawaogopesha wengi katika maisha yao.
Kimsingi jamii inaogopa sana kurogwa, kuuawa kwa nguvu za asili au kutendewa aina yoyote ya ukatili na watu wabaya. Kuna kesi nyingi sana kwenye ndoa kuhusiana na kutaka kuangamizana kwa uchawi na kutoana roho kwa silaha. Hali hii iko karibu kila mahali anapoishi mwanadamu.
Katika maeneo ya kazi watu wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa hofu ya kutendewa mabaya na wabaya wao, lakini wapo ambao wamekufa kabisa kwa kufanyiwa hivyo na maadui zao, inawezekana hata wewe unayesoma mada hii umeshasikia au kukumbwa na kadhia ya adui yako.
Kimsingi hii ni changamoto isiyoepukika katika maisha. Huwezi kuamua kuishi na watu wema tu na ukawakwepa wenye roho mbaya na chuki zisizokuwa na sababu. Wale unaokula nao ndiyo wabaya wako, methali ya Kiswahili inasema.
Unachotakiwa kufanya ni kujua tu nini cha kufanya ili umshinde adui yako na wewe uendelee kuishi maisha yako.
Muoneshe upendo adui yako
Watu wengi wamejikuta wakiwapa nafasi adui zao kuwaangamiza kwa sababu hawajui nguvu ya upendo. Mara nyingi upendo hutafsiriwa kama haki. Ninamaana kwamba kila apendaye anatenda haki ambayo ina nguvu ya kumkinga na mabaya yote kutoka kwa hao aliowapenda.
Zingatia jambo moja muhimu kuwa hatua ya kwanza ya mtu kudhurika inaanzia kwenye hofu ambayo hukuzwa na mawazo yake mweyewe, na siku zote mtu mwenye upendo hawezi kuhofu kutendewa mabaya na watu aliowatendea wema na kuwapenda.
Kuwa na mawazo hayo pekee huweka kinga thabiti ya mwili kukabili nguvu mbaya za asili zinazoelekezwa kwake, kwa vile stahili ya kulipwa mabaya hukosekana moyoni.
Hutakiwi kumchukia mtu ambaye unahisi ni adui yako. Unachotakiwa kufanya ni kumpenda na kujipendekeza kwake, ili yeye aone aibu ya kukufanyia ubaya. Usilipe ubaya kwake hata kama ushahidi unaonesha kuwa yeye ndiye aliyekufanyia kitu kibaya.
Ukifanya hivi utakuwa umejiokoa na shambulio la adui yako kwa kiwango kikubwa. Nasisitiza upendo! Wanawake mlioolewa wapendeni wifi, wakwe zenu hata kama mtahisi wana chuki dhidi yenu.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
[…] na Wema isaac Sepetu baada ya kila mmoja kurusha kombora kwa mwenzake na kuonesha wazi kuwa bado kuna visasi kati yao ambavyo haviwezi kumalizika kirahisi na pengine hadi […]