The House of Favourite Newspapers

Upo ‘Sirias’ Kweli au Ndiyo Yaleyale ya Ray c?

Kahrid Mohammed (T.I.D) na Ray C

Na HASHIM AZIZ| GAZETI LA AMANI| MAKALA

“KAMA wanipenda, kaninunulie zezee, nikilala kitandani, zeze lanibembelezaaa!!” hayo ni baadhi ya mashairi ya msanii mkongwe kunako tasnia ya Muziki wa Kizazi Kipya Bongo, Khaleed Mohamed ‘TID , siku hizi anapenda zaidi aitwe Mnyama! Zeze ndiyo wimbo uliomtambulisha, miaka ya mwanzoni mwa 2000!

 

T.I.D

Nani hakuupenda Zeze kipindi hicho? Ulikuwa kama wimbo wa taifa, jina lake likavuma kwa kishindo, hata alipokuja kutoka na Siamini, akionesha staili mpya ya ‘kusheki’, jina lake lilizidi kupaa kila kona ya nchi. Haukupita muda mrefu, akaandika historia nyingine kwa kushiriki kwenye filamu ya Girlfriend, kipindi hicho hata Bongo Muvi haijulikani ni nini.

Ndani ya filamu hiyo ambayo nathubutu kuiita kuwa ndiyo ya kwanza kwa filamu za kizazi kipya, alishiriki kama msanii chipukizi anayetafuta njia ya kutoka na kama hiyo haitoshi, wimbo wake wa Girlfriend ulitumika kama sound track ya filamu hiyo, akiwa na wakali kama Jay Moe, Yvonne Cherry  Ngatikwa ‘Monalisa’ na wengine kibao!

Ray c

Ulimwengu wake ukawa umefunguka, mafanikio yakamwagika kwake, jina lake likazidi kushaini huku sauti yake ya kipekee na ukali wa kusheki, vikizidi kumpa umaarufu! Akazidi kukaza na nathubutu kusema kwamba mpaka leo hii, TID ni miongoni mwa wasanii waliodumu kwa muda mrefu kwenye gemu bila kuchuja.

Hadhi yake bado ni ya juu, muziki wake bado ni wa kipekee na hata shoo zake, zipo classic sana, kwa hilo anastahili pongezi. Lakini kama walivyosema wahenga, hakuna binadamu aliye mkamilifu, kama ambavyo mimi na wewe tunayo mapungufu yetu, TID naye anayo mapungufu yake na miongoni mwa mapungufu hayo ni kujihusisha kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa muda mrefu.

Sitaki sana kuzungumzia yaliyopita katika maisha yake, lakini kama mwenyewe alivyosema, anawaomba radhi wote ambao kwa namna moja au nyingine, aliwakosea katika kipindi ambacho akili yake ilikuwa ikiongozwa na unga! Ipo wazi kwamba yapo matukio kadhaa aliyokuwa akiyafanya mkali huyo, ambayo kama unamfahamu vizuri TID halisi, ilikuwa lazima ujiulize, amepatwa na nini?

Ushujaa aliouonesha juzikati, wa kusimama mbele ya umati wa watu, wengi wakiwa ni viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda na kamishna mwenye dhamana ya kuongoza mapambano ya madawa ya kulevya nchini, Rogers Sianga, kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Posta jijini Dar ni wa kuigwa.

Kila shabiki wa TID atakiri kwamba hakuna maneno yaliyomfurahisha kila mtu kama kumsikia TID kwa kinywa chake, akisema yeye Mnyama, anaomba radhi kwa yote yaliyotokea na kamwe hatarudia kubwia madawa.

Unga ni hatari na TID anaweza kuwa balozi mzuri wa kuwaelimisha wengine kwa sababu yeye ameishi kwenye unga, anaelewa akili za unga, anaelewa raha na karaha ya unga, anaelewa madhara yake na anaelewa ni kwa kiasi gani unga umemchelewesha kufikia zile ndoto alizokuwa nazo, kipindi anaanza kung’ara kwenye muziki.

Wasiwasi wangu ni kwamba, kabla ya haya yaliyotokea kwa TID hivi karibuni, kuanzia sakata la kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akitakiwa kwenda kuripoti  central ambako baadaye alishikiliwa kwa siku kadhaa kabla ya kuja kuachiwa baadaye na mahakama, akitakiwa yeye na wasanii wenzake waliokuwa wakishikiliwa pamoja, kurekebisha mienendo yao, kulishakuwa na sakata la mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’, naye kutopea kwenye madawa.

Ray C amewahi kusaidiwa mpaka na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete na akaapa kwamba hatarudia tena kutumia madawa ya kulevya, kama TID alivyoapa mbele ya Makonda, na sote ni mashahidi ya nini kilichofuatia baada ya kiapo chake hicho.

Nikiri kwamba mimi ni shabiki mkubwa wa TID tangu anaanza kutoka na hakuna kitu kilichokuwa kinaniumiza kama tuhuma dhidi yake kwamba anakula unga lakini kwa kuwa amekiri mwenyewe, basi moyo wangu umetulia sasa lakini nakuuliza TID, je, kiapo chako kipo ‘sirias’ au na wewe unatuzuga kama alivyofanya dada yetu Ray C? Muda utazungumza ila nakuombea kila la heri kwa sababu najua kazi iliyopo mbele yako si nyepesi.

Comments are closed.