Urusi: Ndege Anayodaiwa Kupanda Bosi Wa Wagner Group Yapata Ajali Na Kuua Abiria Wote
KIONGOZI wa kundi la Wagner ambaye ni mpinzani mkubwa wa Rais Vladimir Putin wa Urusi anahofiwa kufariki katika ajali ya Ndege iliyotokea jijini Moscow.
Taarifa zinadai kuwa jina la Yevgeny Prigozhin limo kwenye orodha ya abiria 10 waliokuwemo ndani ya Ndege hiyo binafsi.
Prigozhin ni Kiongozi wa juu wa kampuni binafsi ya kijeshi, aliyeongoza maasi dhidi ya majeshi ya Rais Putin mwezi Juni mwaka huu ambapo alishindwa.
Ziko tetesi kuwa Ndege hiyo imeangushwa na majeshi ya anga katika mkoa wa Tver kaskazini mwa Moscow mara tu baada ya kuruka.
Shirika rasmi la habari la Russia linasema miili ya watu wanane imepatikana kwenye eneo la ajali.
Mapema mamlaka ya usafiri wa ndege Russia ilisema kwamba kulikua na majina ya watu 10 kwenye orodha ya abiria wa ndege hiyo iliyokua inatoka Moscow kuelekea St. Petersburg.
Ripoti zisizothibitishwa za vyombo vya habari zinasema ndege hiyo ilimilikiwa na Prigozhin, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya kibinafsi ya kijeshi ya Wagner.
Mamlaka ya usafiri wa anga ya Russia, Rosaviatsia, imesema Prigozhin alikuwa kwenye orodha ya abiria. Hata hivyo, haikufahamika mara moja iwapo aliwahi kupanda ndege hiyo.
Shirika la habari la serikali ya Russia, Tass limewataja maafisa wa dharura wakisema kuwa ndege hiyo ilibeba marubani watatu na abiria saba. Maafisa wanasema wanachunguza ajali hiyo, iliyotokea katika mji wa Tver zaidi ya kilomita 100 kaskazini mwa Moscow.
Prigozhin, ambaye kundi lake binafsi la wanajeshi la Wagner lilipigana pamoja na jeshi la kawaida la Russia huko Ukraine, lilifanya uasi wa muda mfupi dhidi ya uongozi wa kijeshi wa Russia mwishoni mwa mwezi Juni.
Video kwenye mtandao wa kijami Telegram zilizotangazwa na Wagner zilionesha picha — ambazo AFP haikuweza kuthibitisha kwa njia huru — za mabaki ya ndege ikiungua kwenye uwanja.
Siku ya Jumatatu, kulikuwepo na video iliyosambaa ikimuonyesha kiongozi huyo wa Wagner akiwa Afrika, ambako alisema ataongeza ushawishi wa kundi lake na kulifanya bara la Afrika kuwa “huru zaidi”.