Usajili wa Dilunga waziingiza vitani Stand, JKT
Hassan Dilunga.
Martha Mboma,Dar es Salaam
WAKATI kikosi cha JKT Ruvu kikitamba kunasa saini ya kiungo wa Stand United, Hassan Dilunga, timu yake hiyo ya zamani imeibuka na kudai kuwa bado ina mkataba na kiungo huyo ambao haujamalizika na alitakiwa kuwa Shinyanga na timu.
Dilunga ambaye anatajwa kuonekana katika mazoezi na kikosi cha JKT huku Stand ikiendelea na kambi yake ndani ya Mgodi wa Buzwagi kwa ajili ya maandalizi ya mechi za ligi kuu ambazo zinatarajiwa kuanza Desemba 12, mwaka huu ni mmoja kati ya viungo bora hapa nchini.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha msaidizi wa timu hiyo, Mrage Kabange alisema kuwa wapo na kiungo huyo kwa sasa na wanaendelea na mazungumzo na wachezaji wengine.
“Dilunga kwa sasa yupo na kikosi cha JKT Ruvu ni moja kati ya maboresho ambayo tumefanya katika kikosi chetu kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na timu kuweza kufanya vyema kwa michezo ijayo.
“Pia kuna baadhi ya wachezaji tunaendelea nao na mazungumzo baada ya siku chache tunaweza kuanika tulichokubaliana,” alisema Kabange.
Kwa upande wa Stand United kupitia, msemaji wao, Deokaji Makomba alifunguka hivi: “Hizo taarifa za Dilunga zinashangaza kwamba amekwenda JKT Ruvu wakati sisi tuna mkataba naye alisaini mwaka mmoja na ametumikia miezi kama minne tu hivyo bado ni mchezaji wetu.”