The House of Favourite Newspapers

Usaliti ni kama asali, chunga usiionje!

TUMSHUKURU Mungu kwa kutujalia uhai. Ni Jumatatu nyingine tunakutana kwenye uwanja wetu huu wa kupeana darasa la masuala ya uhusiano wa kimapenzi na maisha kwa jumla. Tujifunze kwa pamoja na tubadilike kwa sababu kujifunza ni jambo moja na kubadilika ni jambo lingine.  Kuna watu wengi wanajifunza kila siku, lakini shughuli imekuwa kwenye kubadilika. Hata kwenye somo langu la leo kama linavyojieleza hapo juu. Hakuna mtu ambaye ni mgeni na jambo hili, wengi wetu tumeshalisikia kama si kulitenda.

Usaliti unasababishwa na mambo mengi, lakini miongoni mwa vitu vinavyosababisha jambo hili ni pamoja na tamaa au mazingira halisi ya wapendanao. Kuna wakati mazingira yanasababisha vitendo hivi kwa maana gani, mmoja wenu anapokuwa bize kupita kiasi na mambo mengine kisha kumsahau mtuwe.

Kuna tamaduni sasa hivi zimejengeka kwamba, mwanaume na mwanamke wakishazoeana sana, basi kila mmoja anakuwa hana mpango na mwenzake. Suala la wivu wa kimapenzi wanalipa kisogo. Mwanaume anaweza kuwa bize na mambo yake, vivyo hivyo mwanaume naye ana mambo yake.

Mwanamke anakuwa bize na rafiki zake, hana muda na mwanamke wake. Mwanamke naye anakuwa huru tu na rafiki zake. Hakuna mipaka maana wameshaamua kuyafanya maisha yao yawe hivyo, wameshazaa pengine basi kila mtu anaponda raha kivyake.

Rafiki zangu, hayo ndiyo mazingira hatarishi ambayo yanasababisha mtu kusaliti maana mazingira yanamruhusu. Yanamruhusu kwa sababu yupo huru, anakwenda kwenye starehe zake peke yake na mwenzake anakula raha kivyake.

Sina maana kwamba wapendanao wanatakiwa kustarehe pamoja, lakini suala hili mnapolifanya kama sehemu ya mazoea, hamjaliani, basi mmoja wenu anapokutana tu na kishawishi, ni rahisi mno kujikuta ameingia kwenye dhambi hiyo ya usaliti.

Kama nilivyosema kwenye utangulizi, suala la usaliti ni kama asali. Unapoingia ni rahisi sana kurudia tena na tena kwa sababu kile utakachokutana nacho ndicho kitakachokupa utofauti. Yawezekana mtu wako alikuwa hakupi kitu fulani, basi ukionja, huachi.

Halafu ukizingatia sasa, mtu wako yuko bize na rafiki zake, basi wewe inakuwa rahisi tu kufanya mambo yako. Hakuna mtu wa kukubughudhi. Mtu wako mtakutana jioni, hii ni aina mbaya sana ya maisha ambayo wengi huitumia kwa sasa.

Usaliti umegeuka kuwa jambo la kawaida sana. Mtu ana mke au mke ana mume, lakini pembeni anakuwa na mtu mwingine akidai anampa furaha. Rafiki zangu, hii furaha tunayoisema haiwezi kuwa na afya. Sanasana itakuongezea matatizo bure.

Madhara ya usaliti, mbali suala zima la magonjwa, linarudisha nyuma kimaendeleo. Unapokuwa na mchepuko, lazima uugharamie. Bahati mbaya sana mchepuko anafanya kila linalowezekana ili kuweza kukupumbaza uendelee kumuona yeye ni wa maana kuliko mtu wako.

Utajikuta unamaliza fedha nyingi kwake kwa maana ya matumizi, nyumbani huachi kitu au unashindwa kuwatimizia mahitaji kama ya watoto na mambo mengine ya kutunza familia. Kwa nini uhangaike na michepuko? Kwa nini uitelekeze familia yako? Acha kabisa kuonja ‘asali’ ya usaliti. Uogope usaliti kama ukoma!

Jiheshimu, tafuta mtu wako anayekuridhisha na ufanye naye maisha. Itakusaidia, kwanza utakuwa salama, lakini pia utafanya maendeleo kwa haraka!

Nikutakie mabadiliko mema, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Na  Erick Evarist

Comments are closed.