The House of Favourite Newspapers

Usaliti ni mgumu kufutika akilini, bora usisaliti kabisa!

0

Couple-in-BedKwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita, tulijifunza kuhusu wapendanao kufichana vyanzo vyao vya fedha. Nilihitimisha mada yangu kwa kueleza kuwa wapendanao wanapaswa kuwekana wazi. Mnapokuwa kwenye uhusiano ‘serious’ au ndoa, hakuna sababu ya kufichana.

Mnaweka mapato yenu mezani, mnajadili kwa pamoja nini cha kufanya na mwisho wa siku mnatekeleza mipango yenu ya kila siku. Iwe ni miradi, mahitaji ya nyumbani na vitu vingine.

Nirudi moja kwa moja katika mada ya leo kama inavyojieleza hapo juu. Kwa kila mwenye akili timamu, mwenye mapenzi ya dhati, kamwe hawezi kufurahia usaliti. Usaliti unauma. Usaliti unatesa, usaliti ni jeraha la moyo.

Usaliti unapotokea, anayesalitiwa anaumia sana moyoni. Ni kama amepata kidonda. Upendo wa kweli unajengwa na uaminifu. Panapokuwa hakuna uaminifu, usaliti unachukua nafasi. Usaliti au viashiria vya usaliti vinapotokea kwenye uhusiano wowote, penzi husika lazima liyumbe.

Uhusiano husika unakuwa umewekwa rehani. Muda wowote unaweza ukavunjika. Sababu za kufikia kuvunja uhusiano ni matokeo ya kushindwa kutibu jeraha la usaliti. Au unaweza ukatibu jeraha la usaliti lakini kovu lake likachukuwa muda kufutika.

Kidonda kinapopona, huwa kinaacha kovu. Kabla hakijaacha kovu, kinahitaji ‘dawa’ ili kipone. Utafanikiwa kumtibu? Hapo ndipo kwenye kiini cha mada yangu. Maana waweza saliti, ukabainika na ukatubu na kuomba msahama lakini mwenzako akashindwa kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

Ukashindwa kuirejesha imani ambayo mwenzako alikuwa ameiweka kwako licha ya kuwa umekiri kosa na kuomba radhi. Bahati mbaya sana watu wanatofautiana katika suala la kusahau kitu au unayepaswa kumfanya mwenzako asahau, bado haumshawishi kusahau.

Umesamehewa lakini matendo yako yanashindwa kumuonesha yule ambaye unampenda kwamba hutarudia kosa hilo. Kwamba hutashiriki vitendo ambavyo vinaweza kumtia shaka mwenzako na akaanza kuhisi unataka kumsaliti tena.

Kovu la usaliti ni kama janga zito. Unaweza kufanikiwa kutibu kidonda chake kwa kuomba radhi lakini kovu lake lisifutike kirahisi. Mwenzako atakukubalia kwamba amekusamehe lakini moyoni bado ana dukuduku.

Mawazo ya kusalitiwa yanamzunguka kila wakati. Anakutathmini kila akuonapo. Hata ukiwa mbali bado anajiuliza maswali; kwa nini umefikia hatua hiyo? Umekosa nini kwake? Kipi kimekushawishi hadi wewe kufikia hatua hiyo? Maswali ambayo kila akiwaza atakuwa anajijibu mwenyewe kulingana na namna anavyofikiri.

Kovu la usaliti linaweza kufutika pale tu litakapopata tiba sahihi. Labda nifafanue kidogo, kwa nini kovu la usaliti linachukuwa muda mrefu kupona?

Mapenzi yanabebwa na kitu kinaitwa hisia. Macho yanaanza kuona, moyo unatamani kisha baadaye unapenda. Moyo unapofika kwenye hatua ya kupenda, kinachofuata hapo ni imani na uaminifu. Penzi linashamiri kwa siku, mwezi na hata miaka.

Kila mmoja anakuwa ana imani na mwenzake. Mwanamke anamuamini mwanaume na mwanaume anamuamini mwanamke. Wawili hao wanapoaminiana, kila mmoja anakuwa mwaminifu kwa mwenzake. Wanawekeana mtaji wa uaminifu ambao ndiyo unazaa thamani ya penzi.

Mwanaume anajitoa kwa mwanamke, mwanamke vivyo hivyo. Kila mmoja anajivunia kuwa na mwenzake. Kila mmoja anampa thamani mwenzake. Mwanamke anaona hakuna mwanaume mwingine zaidi yake duniani. Mwanaume naye anaona hakuna mwanamke mwingine zaidi yake.

Ikitokea ajali ya usaliti, msalitiwa huwa anapoteza imani. Kuirejesha imani inahitajika nguvu ya zaida. Kuondoa kandokando zote ambazo pia itategemea na namna mhusika atakavyokuwa tayari kusahau hivyo ndiyo maana nimesema kovu la usaliti ni gumu kufutika, epuka usaliti.

Hakikisha uliyenaye ni sahihi. Acha tamaa, ridhika na uliyenaye na mpe yeye kipaumbele na thamani ya juu kuliko mtu mwingine yeyote. Acha ‘macho juujuu’ na maisha mtayaona matamu.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

Leave A Reply