The House of Favourite Newspapers

Usichokijua kuhusu matatizo ya tezi dume (Prostatism)

Hali hii husababisha matatizo ya mkojo kwa mwanaume na kufanya mkojo ushindwe kutoka.

CHANZO CHA TATIZO

Matatizo ya tezi dume yamegawanyika katika sehemu kuu tatu. Kwanza ni uwepo wa maambukizi katika tezi hiyo ambayo husababishwa hasa na magonjwa ya zinaa kama kisonono. Pili ni uvimbe wa tezi dume ambao hutokea tu na tatu ni saratani ya tezi dume.

Matatizo haya ya tezi dume kwa ujumla huanza taratibu sana kati ya umri wa miaka thelathini hadi hamsini.

Kati ya umri wa miaka 30 hadi 45 wanaume wengi wenye matatizo haya huathirika na maambukizi  ya tezi dume ambayo husababisha awe anatoa manii iliyochanganyika na damu na harufu mbaya na wakati mwingine hutoka kama usaha katika njia ya mkojo.

Kuanzia umri wa miaka 45 hadi 50, hali ya uvimbe wa tezi dume huanza taratibu na kuanzia umri wa zaidi ya miaka 50 hadi 60 tezi dume inaweza kuwa saratani au kansa.

Kutanuka kwa tezi dume na saratani ndiyo husababisha mkojo usitoke vizuri au usitoke kabisa.

Kwa mujibu wa takwimu, inaonyesha asilimia arobaini ya wanaume hupatwa na tatizo hili la saratani ya tezi dume na nusu yao yaani asilimia ishirini huwa hawapati dalili za awali na wakichunguzwa tu, tayari saratani inakuwa  imeshafika mbali.

Saratani ya tezi dume ni miongoni mwa magonjwa machache yanayochangia kupunguza umri wa kuishi wa wanaume wengi hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Tatizo hili huanza taratibu kama uvimbe ambao siyo saratani. Huanza kama vivimbe vidogovidogo vingi    ambavyo hutokea sambamba na kuvimba au kubana kwa njia ya kutolea mkojo kwa ndani zaidi na kuzuia mkojo kutoka vizuri au kushindwa kabisa kutoka.

Saratani ya tezi dume hutokea kwa upande wa nyuma wa tezi dume ambayo imepakana na mfuko wa haja kubwa.

Kuvimba kwa tezi dume na saratani ya tezi dume huwa havihusiani moja kwa moja, mtu anaweza kuwa na uvimbe wa tezi dume na isiwe saratani au anaweza kuwa na saratani pia unaweza kuwa na vyote viwili, yaani uvimbe ukiambatana na saratani yake.

Tezi dume inapozuia mkojo, mgonjwa anaweza  kuathirika kwa kupata kirahisi maambukizi katika kibofu cha mkojo, kutanuka kwa mirija ya mkojo, kutanuka kwa figo, mawe katika kibofu cha mkojo na figo, mkojo kurudi kwenye damu, shinikizo la juu la damu na mwishowe ni kifo.

DALILIZA UGONJWA

Tezi dume zinapokuwa zimevimba sana hubana kibofu cha mkojo na kuziba njia ya kutolea mkojo, mgonjwa huhisi kukojoa lakini mkojo hautoki na kila wakati huenda chooni huku mkojo ukitoka kidogo kidogo.

Hali huwa mbaya nyakati za usiku ukiwa umelala, huamka mara kwa mara na ukijisahau unajikojolea, mkojo unapotoka huwa hauishi kwa hiyo kila wakati unaenda chooni na pia hautoki moja kwa moja, ukisukuma kwa nguvu ndiyo hautoki kabisa.

Hali hii inatokana na tezi dume kuvimba zaidi na kuziba njia ya mkojo.

Katika tatizo hili endapo mwili utatulia, basi mkojo hutoka mwingi kwa matonematone na hali hii ya mkojo kutotoka vizuri huathiri mfumo wa damu, shinikizo la damu au presha inakuwa juu, moyo huathirika na mgonjwa huchanganyikiwa kutokana na sumu ya mkojo kurudi kwenye damu ‘Uremia’.  Mgonjwa anapotoa mkojo uliochanganyika na  damu, husababishwa na kuvimba zaidi kwa tezi dume na hili husababisha tatizo sugu la kuziba kwa mkojo.

Mkojo unabaki kwenye kibofu kwa muda mrefu, hupata maambukizi kirahisi na kumfanya mgonjwa asipate muda wa kupumzika mchana na usiku,  kila wakati ni kwenda kukojoa huku akipata maumivu wakati wa kukojoa, homa kali, kutetemeka, kichefuchefu na kutapika.

Pia sehemu ya chini ya tumbo huvimba kutokana na mkojo kujaa au kuvimba na kuwa pakubwa zaidi.

UCHUNGUZI

Uchunguzi wa tatizo hili uanze mara moja hasa pale mtu mzima mwenye umri wa miaka 50 anapoanza kuhisi hali isiyo ya kawaida katika utoaji wa mkojo. Katika hali hii, endapo dalili tulizozieleza hapo juu zitakuwepo, basi moja kwa moja huyu mgonjwa atakuwa na tatizo la tezi dume na uchunguzi wa kina uanze.

 Uchunguzi hufanyika katika hospitali za mikoa ambapo kipimo maalumu kiitwacho ‘DRE’  ‘Digital Rectal Examination’ kitafanyika.

Kipimo hiki kitaonyesha jinsi tezi dume ilivyotanuka na kama dalili za saratani zipo.

MATIBABU NA USHAURI

Tatizo hilo linatibika vizuri kama utawahi mapema  kufanyiwa uchunguzi.

Inashauriwa kila mwanaume unapofikisha umri kuanzia miaka 45 uwe na desturi ya kupima afya hasa tezi dume ingawa upimaji wa afya kwa ujumla unatakiwa iwe desturi tangu utotoni.

Pima tezi dume angalau mara moja kila mwaka kuanzia umri wa miaka 45 hadi 50, baada ya hapo angalau mara mbili kwa mwaka. Katika  hatua  za  awali  unaweza  kutibiwa  kwa dawa.

Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

Duh! Hii Kali, Sangoma Anaswa Akimroga Darassa!

 

Comments are closed.