The House of Favourite Newspapers

Usichokijua Kuhusu Vita ya Marekani Vs Korea Kaskazini – 3

0
Rais wa Marekani, Donald Trump (kushoto) na Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Yung.

KATIKA mfululizo wa makala haya, wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo Urusi na China zilivyoachana na mfumo wa Kikomunisti na kuiachia Korea Kaskazini ambayo sasa inavimbiana na Marekani.

Wakati huohuo, Serikali ya Tanzania inashtushwa na kitendo cha kuorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo zinachunguzwa na Umoja wa Mataifa na kuhusishwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na Korea Kaskazini inayoongozwa na Rais Kim Jong Yung.

Rais Donald Trump.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania, Dk Augustine Mahiga, licha ya uhusiano uliokuwepo awali, lakini tangu mwaka 2014, Tanzania imepunguza kabisa uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na nchi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, Marekani wameendelea kujiuliza juu ya nini lengo la vitisho vya Korea Kaskazini, wiki iliyopita nchi hiyo korofi ilirusha tena kombora baab’kubwa kupitia anga la Japani.

Rais Kim Jong Yung.

Inaaminika kuwa, Korea Kaskazini inamiliki zaidi ya silaha 1,000 zenye uwezo tofauti yakiwemo makombora ya masafa marefu ambayo kuna shaka kubwa duniani kuwa, kwa silaha hizo, inaweza kuishambulia Marekani.

Katika hali kama hiyo, Korea Kaskazini inaelezwa kujifanya kiziwi na kuendeleza mpango wake wa Pyongyang wa majaribio ya silaha kwa miongo kadhaa.

Bomu la nuclear.

Kwa kipindi kirefu, kumekuwa na mirindimo ya mizinga mikubwa, makombora ya masafa marefu na mafupi katika eneo hilo tangu miaka ya tisini.

Inaelezwa kuwa, ni katika kipindi hicho ambacho Korea Kaskazini ilijikita kwenye zoezi la kuunda makombora hayo yenye uwezo wa kurushwa kutoka bara moja hadi lingine ambayo yanaweza kushambulia Mataifa ya Magharibi.

Kwa vigezo hivyo, Korea Kaskazini inasadikiwa kutengeneza kombora la masafa marefu zaidi ambalo wachunguzi wamelitaja kuwa KN-08 au Hwasong-13, kazi ambayo ilikamilika tangu Septemba 2016.

Mbali na makombora, Korea Kaskazini inaelezwa kuwa inaifanyia majaribio mashine yake mpya ya roketi ambayo baadhi ya watu wanasema inaweza kurusha kombora kutoka bara moja hadi jingine kwa uhakika zaidi.

Vifaru vya mabomu vya Korea Kaskazini.

Idara ya Ulinzi ya Marekani ya Pentagon inaamini kwamba Korea Kaskazini inamiliki makombora 6 ya aina ya KN-08 ambayo yana uwezo wa kufika hadi Marekani.

Mnamo mwezi Januari, mwaka huu, kulikuwa na ishara ya jaribio, muda mfupi baada ya Rais Kim Jong kudai kwamba taifa hilo lilikuwa katika awamu ya mwisho ya kutengeneza kombora linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine.

Kwa wenye kumbukumbu au waliokula chumvi nyingi watakumbuka kuwa mpango wa kisasa wa kutengeneza makombora wa Korea Kaskazini ulianza kwa kutengeneza Scud mwaka 1976. Baadaye ilipofika mwaka 1984, taifa hilo liliyabadilisha jina na kuyaita makombora hayo Hwasong. Mbali na makombora ya masafa marefu, Korea Kaskazini pia ina makombora ya masafa mafupi ambayo yanaweza kulenga taifa jirani la Korea Kusini ambalo uhusiano wao umedorora kwa miaka mingi na sasa hali ni mbaya kiasi kwamba wamekuwa wakijiandaa kwa vita kamili muda wowote.

Bomu la Nuclear la Marekani.

Kombora la Hwasong 5 na Hwasong 6 ambayo pia hujulikana kama Scud B na Scud C yana uwezo wa kwenda kilomita 300 hadi 500 kulingana na kituo cha Marekani kinachofanya utafiti wa kuzuia kuenea kwa nuklia.

Silaha hizo za Korea Kaskazini zimekwishajaribiwa na kupelekwa katika maeneo yanayohitajika, tayari kwa vita. Pia kuna aina nyingine ya kombora liitwalo Nodong lenye uwezo wa kusafiri urefu wa kilomita 1,000 na linafanana kwa kiasi fulani na Scud.

Uchanganuzi unaonesha kuwa, makombora hayo yamethibitishwa kuwa yanaweza kupiga maeneo yote ya Korea Kusini na jirani zao, Japani.

Katika maonesho ya silaha zake, mwaka 2010 Korea Kaskazini ilithibitisha kuwa kombora lake hilo linaweza kufika urefu wa kilomita 1,600 wakimaanisha kwamba linaweza kupiga kambi kadhaa za Marekani zilizopo katika eneo la Okinawa.

Mbali na Nodong, jamaa hao wana kombora lingine liitwalo Musudan ambayo nayo waliyafanyia majaribio mwaka 2016.

Hadi hapo, tayari Korea Kaskazini wamekwishatambulisha aina hizo za makombombora ambayo ni hatari kwa dunia hii. Je, nini hatma ya suala hili?

Tukutane wiki ijayo.

MAKALA:SIFAEL PAUL NA MTANDAO

SHUHUDIA Bomu Lilivyolipuka na Kuua Watoto 3 kwa Mpigo Arusha

Leave A Reply