The House of Favourite Newspapers

Usidharau tende kisa zinaliwa kwa msimu

HAYA tena shosti wangu ndo naingia tena mjini, najua umenisubiri sana baada ya wiki jana kuwachamba wale wavivu, wakilala hawaamki mpaka waume zao wanaenda kazini. Hawajui kumtengea mume maji, kumpigia pasi wala kumchagulia nguo ya kuvaa, haloooo eehhhhh!

Tena inafikia mahali shoga, mpaka mumewe ameondoka hajui amevaa nguo gani, hajui amependeza au haikumpendeza, yeye anaupiga usingizi na kuamka saa nne, chumba kichafu vyombo vinang’ongwa na inzi halafu huyohuyo anasimama mbele ya watu anajiona mke wa mtu? Mke wa mtu labda kijijini kwenu! Shuuutuuuuu!

Kwa somo nililowapa naona wamenyooka, basi leo shoga yangu nataka tuzungumzie kujitunza wanawake katika suala zima la kuzaa watoto wengi bila kuangalia hali zetu.

Unakutana na mwanamke ana watoto saba lakini wanaishi chumba kimoja. Siingilii mpango wa Mungu katika kupata watoto au tumeze vidonge vya mpango na kuweka vijiti, la hasha, kinachotakiwa ni kupanga jinsi ya kupata watoto wetu ili waachiane na kukua vizuri pia mzazi kuwa katika afya njema, au nadanganya shoga yangu?

Nalisema hili kutokana na kumuona mama mmoja akisumbuka na watoto wanne ambao wamepishana kwa miezi na si mwaka. Nami si unajua mama usipitwe. Nilimdodosa sababu ya kuzaa watoto kama mayai ya chura? Mmh! Alichoniambia nilichoka shoga nikaamini kama ataendelea vile basi atajaza timu ya mpira na rizevu wake.

Alinieleza kuwa mumewe ni askari na kuna kipindi kutokana na kazi yake nyumbani huwa anarudi mara moja kuoga na kwenda kazini tena mchana, hajui hata analala saa ngapi.

Yeye aliamini mumewe ana mwanamke wa nje, kwa vile haki yake ya ndoa kuipata imekuwa mbinde. Kwa hiyo siku alipokuja hata akiwa kwenye siku za hatari huwa hataki kumuachia mumewe lazima apate haki yake.

Ile imesababisha kila akikutana na mumewe anaruka na ujauzito kitu ambacho hakimpi tabu kwa vile anaamini hana njia nyingine ya kupata haki yake kwa mumewe.

Mmh! Kazi kwelikweli umeona wanaume mnavyotutesa? Jamani wewe ni mwanaume gani huna huruma unaona raha kumzalisha mkeo kama mbuzi wajichungao porini.

Sawa kazi ndiyo inayowaweka mjini, lakini kazi gani hiyo ya kushindwa kumpa haki mkeo mpaka akubake kwa kukulazimisha ndipo apate haki yake? Unataka mkeo haki yake akapate wapi sasa? Shuuutuuuuu! Hebu ona jinsi wanawake wengi wanavyozalishwa bila huruma huku afya zao zinakongoroka.

Unamnyima haki yake, akaipate wapi au unataka kumlazimisha achepuke, akadange nje ya ndoa ili upate sababu ya kumtelekezea mtoto?

Nakataa hakuna kazi ya kukesha kila siku, kwanza jeshi gani hilo? Mumeo ni askari katika kituo kidogo cha polisi ‘polisi posti’ ajabu nyumbani anarudi kwa mwezi haizidi hata mara nne.

Kwa vile sasa hivi tupo wanawake wengi na wengi wao wazuri, ukiangalia tunaozurura tunajua kujipamba ili tuwanase waume za watu na tukiwapata basi tutajituma kila kona kuhakikisha hatumpotezi.

Kwa vile ndani ya nyumba havipati basi akili yake nyumba ndogo. Na nyumba ndogo kwa kutaka sifa utasikia; “Mpenzi leo tafuta kila njia ulale kwangu.” Hooooovyoooo! Mwanaume ukionja umeumia utatamani kila siku ukalale huko, hapo ndipo unapomsahau mkeo kumpa haki yake.

Jamani waume zetu hebu tuoneeni huruma, usidha-rau tende kisa zinaliwa kwa msimu. Mpende mkeo kwa vile yeye ni kila kitu kwako. Huyo anayekuzuzua anakupenda kwa vile una kitu ukiishiwa humuoni. Tuoneeni huruma kumbukeni tunawavumilia kwa mangapi?

Hebu heshimuni ndoa kwa kumjali mkeo si kumzalisha kama nguruwe pori na kumuacha na watoto, starehe ufanye na mchepuko.

Nina imani nimesikika, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

 

Comments are closed.