Stori: Andrew Carlos
USIKU wa Agosti 13, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar patakuwa hapatoshi kwani ndiyo siku mahususi ambayo mkali wa nyimbo za Uswahilini, Seleman Jabir ‘Msaga Sumu’ atakapokuwa anakabidhishwa ufalme rasmi.
Katika usiku huo mkongwe wa Muziki wa Bongo Fleva kwa zaidi ya miaka 15, Juma Kassim ‘Nature’ anatarajiwa kuangusha shoo ya kufa mtu akiungana na Malkia wa Mipasho Bongo, Khadija Kopa ambaye pia amejitapa kufunika katika usiku huo wa kumsindikiza Msaga Sumu.
Akizungumza na Uwazi Showbiz, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa usiku huo Msaga Sumu atazipiga nyimbo zake zote zaidi ya 15 alizozifanya tangu alipoanza kuimba ambazo zipo kwa staili tofauti kama Singeli, Mchiriku, Ladha, Segere, Bongo Fleva na nyingine kibao.
“Nature kama tujuavyo ana ngoma ya Inaniuma Sana (Remix) aliyomshirikisha Msaga Sumu hivyo atakuwa jukwaani kumvisha ufalme wa uswahilini. Ijulikane kuwa Msaga Sumu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuufikisha muziki wa uswahilini hapa ulipo kiasi cha kupewa heshima kama miziki mingine,” alisema Mbizo.
Usiku huo pia, Msaga Sumu atasindikizwa na wakali wote wanaokubalika uswahilini wakiongozwa na Segere, Dogo Mfaume, Snura, Shoro Mwamba, MC Sudy na wengine kibao.