USIKU WA PIGA NIKUPIGE… BENDI 3 JUKWAA MOJA IDD HII DAR LIVE

KAMA ulikuwa ukijiuliza ni kiwanja gani utaenda kuburudika katika sikukuu hii ya Idd Mosi (Agosti 22, mwaka huu) jibu lake ni moja tu, Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar, unatarajia kushusha bendi tatu, mbili za Taarab na moja inayopiga nyimbo za ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja na Mratibu wa Dar Live, Rajabu Mteta ‘KP Mjomba’ alisema kuwa, usiku huo ambao shoo nzima itaanza ‘mishale’ ya saa 12:00 jioni na kuendelea, bendi zitakazoporomosha burudani mwanzo mwisho kwa upande wa Taarab ni Zanzibar Stars pamoja na Jahazi Modern huku The Hurricane wakikamua kwa upande wa nyimbo kali zinazotikisa Bongo na nje ya Bongo.

“Utakuwa ni Usiku wa Piga Nikupige, wote tunaijua Jahazi Modern ilivyo kongwe na tishio lakini pia wote tunaijua Zanzibar Stars ilivyo, kwa hiyo siku hiyo Zanzibar Stars wakiweka Utakiona Kimbembe na Twabonyeza Kibongobongo huku Jahazi Modern wanabandika Nia Safi Hairogwi na Kamwe Siumbuki, unakifiki itakuwaje? Njoo Dar Live.

“Lakini pia tutakuwa na Bendi ya Hurricane inayotikisa jijini Dar kwa kupiga live band ambapo usiku huo itapiga kopi ya nyimbo zote kali zinazotamba duniani,” alisema KP Mjomba.

Mbali na uwepo wa shoo hiyo ya kibabe, KP Mjomba aliongeza kuwa, siku hiyo wale mashabiki wa Singeli nao watakata kiu yao kwa kushuhudia bonge moja la shoo kutoka kwa wakali kibao wakiwemo Man Rongo, Pazo, Mreno pamoja na Sholo Machozi.

Kwa upande wa burudani ya watoto, pazia la burudani litafunguliwa mapema kuanzia saa 4:00 za asubuhi kwa michezo mbalimbali kama vile Ngoma za Asili, Sarakasi, Kucheza na Nyoka, Moto huku kundi kabambe la Sarakasi na Mazingaombwe Wakali Dancers likigawa zawadi kibao.

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment