Usiku wa Raha za Pwani Waja, Khadija Yusuf, Kivurande, Msagasumu, Misambano Ndani
NGOMA inogile: Usiku wa Raha za Pwani waja, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia burudani ya aina yake iliyoandaliwa na Kampuni ya Mbizo Entertainment ndani ya ukumbi wa burudani wa Mbizo Garden uliopo Magomeni Dar ambayo itafanyika Agosti 30 mwaka huu.
Akizungumza na paparazi wetu muandaa wa burudani hiyo, Mkurugenzi wa Mbizo Entertainment, Juma Mbizo amesema usiku huo si wa kulala na kusubiri kuhadithiwa usije sumbua watu.
Mbizo amesema katika usiku huo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali yakiwemo makundi ya taarab ya Jahazi, East African Melody, Zanzibar Stars. Bendi ya Maquis International chini ya Bobo Sukari nayo itafanya yake ukumbini hapo na kunogesha usiku huo.
Mbizo aliwataja wasanii wengine kwenye usiku huo kuwa ni pamoja na Abdul Misambano, Msagasumu bila kusahau mdatishaji wa mjini mwenye vigoma vyake vya kibao kata almaarufu Kivurande ambaye kundi lake lilizinduliwa rasmi hivi karibuni.
Watoa burudani hao kila mmoja na kila kundi limeahidi kumfunika mwenzake na kuugeuza usiku huo kutoka usiku wa raha kuwa usiku wa kufunikana na kuacha gumzo.