Usikubali sikukuu ikuchanganye, ikuache na madeni!

love, family, finance, money and happiness concpet - smiling couple with money and piggybank ot table at homeNi wiki nyingine tunakutana tena kupitia ukurasa huu nikiamini kuwa umzima na unaendelea na mishemishe zako za kila siku kama kawaida. Kwa wenzangu Waislam najua zimebaki siku chache waisherehekee Sikukuu ya Idd. Furaha iliyoje!

Kikubwa tumuombe Mungu atujaalie tuifikie siku hiyo tukiwa wazima kwani sisi tunapanga na Mungu anapanga yake.

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nataka kuzungumzia suala la baadhi ya watu kuchanganyikiwa na kujikuta wakitengeneza madeni ili tu kuifanya siku hiyo ipite vizuri.

Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba hakuna kitu kibaya kama kuandamwa na madeni. Ni kweli kila mtu kuna wakati anafanya hivyo pale inapobidi lakini madeni yanakosesha watu amani.

Wapo watu waliolazimika kuhama mitaa yao kwa sababu ya kuwa na madeni. Sasa huwa najiuliza ni kwa nini mtu ujikoseshe amani kwa kitu ambacho unaweza kukiepuka?

Nauliza hivyo kwa sababu, katika kuelekea kwenye Sikukuu ya Idd wapo watu ambao tayari wameshapanga kuwa nguo watakopa kwa f’lani na mchele kwa ajili ya kupikia pilau watakopa duka f’lani.

Watu hao wapo, yaani mtu hana uwezo wa kufanya mambo makubwa lakini atajilazimisha ili naye aonekane wamo. Hapo ndipo tunapokosea!

Nasema tunakosea kufanya hivyo kwa sababu, ni kweli siku ya sikukuu lazima ufurahi kwa kula na kuvaa vizuri lakini kama uwezo wa kufanya hayo huna kwa nini ulazimishe?

Ni sawa utafanikiwa kukopa lakini vipi pale ambapo utamaliza sikukuu kisha kujikuta ukisumbuliwa na watu wakitaka uwalipe vitu ulivyokopa? Kimsingi si jambo jema hata kidogo! Kopa pale inapobidi, siyo unakopa ili ukanunue nguo za bei mbaya uwaringishie wenzako.

Au unakopa ili siku hiyo ualike watu kwako waje wale na kunywa, hakuna faida yoyote ya kufanya hivyo zaidi ya kujiandalia presha za kujitakia.

Kama nilivyosema hapo awali kwamba, siku za sikukuu ni za kufurahi lakini mambo ya kufanya ili kuifanya siku hiyo iwe nzuri itategemea na uwezo wako.

Kama sikukuu imekukuta vibaya, huna kitu mfukoni, mshukuru Mungu kisha pika ugali wako na maharage, kuleni na mvae nguo zilizopo, wala msijione wanyonge!

Kumbuka sikukuu ni siku kama siku nyingine, itapita na maisha mengine yataendelea hivyo huna haja ya kulazimisha mambo ambayo yako nje ya uwezo wako.

Najua wengine huwa hatuumizi kichwa kwa sababu yetu bali watoto wetu! Niwaambie tu kwamba, kama huna uwezo kabisa, siku ya sikukuu ikifika na watoto wako wakashindwa kuvaa vizuri, utaumia lakini huwezi kuumia sana kwa kuwa unajua huna uwezo na huwezi kulazimisha mambo.


Loading...

Toa comment