The House of Favourite Newspapers

Usikubali udhaifu wa umpendaye, hamuwezi kudumu!

0

marriage-counseling-nycNi matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, nakukaribisha kwa mara nyingine katika safu yetu hii ambapo tunajuzana mambo mbalimbali kuhusu mapenzi na uhusiano.
Leo nataka tujadili kuhusu suala la kukubali udhaifu wa mwenza wako na umuhimu wake katika kujenga uhusiano au ndoa itakayodumu kwa kipindi kirefu.

Watu wengi ambao wana matatizo katika ndoa au uhusiano wao wa kimapenzi, wanapokuja kwangu kwa lengo la kutaka ushauri, huwa nina desturi ya kuwapa kwanza nafasi ya kujieleza kwa uhuru na uwazi tena katika mazingira tulivu.

Nilichokibaini ni kwamba, wengi huwa wanaingia katika matatizo makubwa kwa sababu tu ya kushindwa kuwaelewa wenzi wao na kukubali udhaifu wao kisha kuamua kuwasaidia.
Sikiliza mfano wa dada Zaituni wa Ilala (siyo jina lake halisi). Yeye alikuja kwangu na kuniambia kuwa ndoa yake imeingia katika mzozo mkubwa kwa takriban mwezi mzima. Akanieleza kuwa chanzo kilikuwa ni yeye kumkataza mumewe kunywa pombe na kuvuta sigara.

Akanieleza kuwa mumewe hakuwa mwepesi wa kumuelewa, matokeo yake wakapishana kauli na tatizo likaanzia hapo. Mume akawa anadai siku hizi mkewe amebadilika sana, anamdharau, anamfokea na kumuwekea masharti kama mwanaye wa kumzaa.

Kilichofuatia, mume akazidisha ulevi kupindukia, akawa anarudi saa nane mpaka tisa usiku akiwa hajielewi na kukipambazuka tu, anajiandaa na kwenda kazini. Hiyo ndiyo ikawa ratiba yake mpya, akawa hataki tena kukaa na mkewe na kuzungumzia suala hilo ili wafikie muafaka mpaka siku alipokutana na mimi kuomba ushauri.

Jambo la kwanza nililomuuliza dada Zaituni ni kwamba tangu amfahamu mwanaume huyo alikuwa akinywa pombe? Akanijibu alikuwa akinywa kwa kiwango cha kawaida. Nikamuuliza kama yeye binafsi aliikubali tabia hiyo ya mumewe kunywa pombe kabla hawajaingia kwenye ndoa?

Kidogo alibabaika kunijibu lakini akafunguka kuwa tangu akiwa mdogo, hakuwahi kutamani kuolewa na mwanaume mlevi.

Nikamuuliza nini sasa kilichosababisha akaingia kwenye ndoa na huyo mumewe?
Majibu yakawa ni kwamba anampenda sana na ana vitu vingi vizuri vinavyomvutia kiasi kwamba akawa hana ujanja zaidi ya kukubali kuoana naye. Bila shaka kwa mfano huu mdogo mtakuwa mmenielewa ninachotaka kukizungumza. Jambo kubwa ni kila mmoja kukubali kwamba hakuna binadamu aliyekamilika.

Unaweza kupata mume mzuri ambaye siyo mlevi kama alivyo mume wa dada Zaituni lakini akawa na kasoro nyingine kubwa zaidi. Suala la msingi ni kumchunguza vizuri mwenzi wako kabla hujaamua kuingia naye kwenye ndoa. Hata kama ana kasoro zake, lazima ana mambo mazuri ambayo ndiyo unayopaswa kuyatazama zaidi.

Dosari utakazozibaini ni jukumu lako sasa kuamua kama utazivumilia au huwezi. Ukiona huwezi huna sababu ya kuingia kwenye ndoa kwa sababu umeshindwa kuukubali upungufu wa mwenzako.
Wengi wanaodumu katika ndoa zao ni kwa sababu wanajua wao hawajakamilika, lazima wana udhaifu ambao wenzi wao wanaujua ila wameamua kuuvumilia hivyo nao wanakuwa wepesi wa kupokea udhaifu wa wenzi wao na kukubaliana na hali halisi.

Kuna mifano mingi ya watu ambao walikuwa walevi au wavuta sigara kupitiliza ambao baadaye waliamua kuacha wenyewe ili wasiendelee kuwakwaza wenzi wao.
Ukiujua udhaifu wa mwenzako usitumie maneno ya dharau ukali, msaidie kwa upendo naamini atabadilika.

Leave A Reply