The House of Favourite Newspapers

USILALAMIKE KWA NINI HUOLEWI,HUENDA UNAJICHELEWESHA

NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha mpendwa msomaji wangu kwenye uku­rasa huu murua. Siku chache zilizopita, nilipata bahati ya ku­zungumza na msomaji wangu mmoja aliyepo Morogoro, si­talitaja jina lake kwa sababu maalum. 

 

Alikuwa akihitaji ushauri na kubwa linalomsumbua, ni kwamba anajihisi hana bahati katika maisha yake ya kimapenzi. Kila mwanaume anayekutana naye, anaishia kumchezea na kumuacha njiani.

 

Wasichana wa rika lake wote wame­shaolewa, wengine walishajenga familia na wengine wapo kwenye hatua ya uchumba rasmi, lakini yeye ni mtu wa kulia na upweke kila siku, akim­pata mwanaume wanakaa baada ya muda fulani kisha anaanza ku­muonesha ku­muonesha mabadiliko makubwa ya tabia na mwisho wanaishia kuachana.

 

Sasa anajihisi umri unaenda, ameshachoshwa na upweke, anahitaji mwenza wa kuan­zisha naye familia, ambaye atampenda na kumheshimu lakini hajui atampata vipi au atamjuaje kama ni mkweli au ndiyo walewale?

 

Huenda dada yangu huyu anawakilisha wanawake wengi huko mitaani ambao licha ya kujaliwa kila kitu, bado wameendelea kuteseka na upweke, wanaishia kutumiwa tu na kuachwa, wengine wa­najikuta wakizalia nyumbani na kuendelea kuzisikia ndoa kwenye bomba.

 

Tunakubaliana kwamba suala la ndoa ni bahati, unaweza kuwa unalalamika kwamba hupati mtu wa kukuoa, lakini kuna mwanamke mwingine ameshaolewa zaidi ya mara tatu na wanaume tofauti na kuachana nao.

 

Anaolewa, anaachika. Baada ya muda fulani anaolewa tena, anaachika na mtiririko unakuwa ni huo. Unaweza kujiuliza, kwa nini mwingine apate bahati ya kuolewa mara mbili au tatu kwa nyakati tofauti, wakati kuna mwingine hajawahi kabisa kuolewa na mpaka sasa hakuna dalili?

Ukiwauliza wanaume am­bao hawajaoa wanapenda kuwaoa wanawake wa aina gani, utashangaa kwamba watapishana kidogo kwenye sura na mwonekano, lakini mambo mengine yote yatakuwa yakifanana. Sifa atakazokuwa anazitaka Juma kwa mke atakayem­uoa, hazitapishana sana na sifa anazozitaka Hamis na ndizo hizohizo anazozitaka Mohamed.

 

Lakini bahati mbaya wakati wanaume wakiwa na vigezo vyao, wanawake wengi hawajui namna ya kujiweka ili mwanaume asiishie kutembea naye kwa mwezi mmoja au miwili kisha akamuacha.

 

Na hapa ndipo unapokuta wanawake wanatumia muda mwingi nyuma ya vioo, kujipamba, kujipodoa, wa­nashinda saluni, wanatu­mia vipodozi vikali, wakati mwingine vinawasaba­bishia madhara makubwa. Wanachokiamini wao, wakipendeza itakuwa ni rahisi kuwapata wa­naume wa kuwaoa. Hata hivyo, wapo am­bao licha ya juhudi zote za kupendeza wanazozi­onesha, bado wanajikuta wakiendelea kusota bila ndoa.

 

Ndoa siyo jambo la mchezo, hadi mwanaume aamue kwamba kweli huyu anafaa kuwa mke, ni lazima awe ame­kupitisha kwenye chujio kali bila wewe mwenyewe kujua. Upo naye, lakini mwenzako anakusoma, kila unachokifanya anajaribu kukitathmini kwa kina, akiona huelekei, mwisho anakuacha na kumuoa msichana mwingine wa mtaani.

 

Sasa swali la msingi unalopaswa kujiuliza ewe dada au mwanamke, ni wapi unapokosea hadi ndoa inaen­delea kuwa msamiati mgumu kwako? Nitumie majibu yako na wiki ijayo nitakupa siri zinazowafanya wengine wanaolewa mara kadhaa huku wengine wakizeeka bila kupata ndoa

Comments are closed.