The House of Favourite Newspapers

Usioghope Kuachika, Ogopa Kuchanika!

 

 RISASI MCHANGANYIKO  | MAISHA NA MAHABA

 

JAMANI salama huko mliko maanti zangu wa kisasa? Leo nimeamka nimechokachoka hata sijui kwa sababu gani, maana jana nimelala mapema tena nikiwa hata sijafanya kazi ngumu. Ingekuwa zamani ningesema wachawi wamenifanyisha kazi, lakini siku hizi, wanipate wapi, nalala na kitabu kitakatifu, waje wauone moto wake!

Hata hivyo, nikasema siwezi kuwaangusha mashosti zangu, lazima niwape kitu roho inapenda, si ndiyo makubaliano yetu bwana? Basi leo sasa ndiyo nataka niwape makavu mubashara, maana kila siku tumezoea kubembelezana hatutaki kupeana live!

Tunalo tatizo moja sisi wana wa kike, tukishawekwa ndani na hao watu wetu, kuachika tunaona kama mikosi, tunaogopa kuchekwa, kunangwa na hata kudharauliwa, kwa sababu tu, eti umeachika.

Nataka niwaambie kitu kimoja, katu usiogope kuachika, ilimradi tu kuachika kwenyewe, kuwe kwa haki. Ndiyo, sasa kwa nini uogope kuachika, yaani hata kama unachanika? Aka babu, usijikwaze.

Maana kuna wengine unapatwa na makwazo kwelikweli ndani ya nyumba, huyo bwana ana gubu, mawifi wana magubu, ilimradi hupumui! Ya nini bhana, mtoto wa kike jiondokee zako, tena uwe na tabasamu usoni!

Niwaambie ukweli, hapa mnaponiona, nimeishi na mabwana watatu na nimeolewa mara mbili, yaani kama hunielewi, wakati nakua natafuta mji wangu, nimeshakaa na wanaume watatu tofauti, wote nikaona wananizingua, nikaachana nao. Ndiyo nikampata mwanaume akanioa, nikazaa naye watoto watatu, nikaachika!

Unadhani hata nilikonda? Siku hiyohiyo narudi nyumbani kwetu, usiku nikaenda ngomani. Afu anicheke nani, kila mtu alikuwa anajua jinsi gani nilimvumilia yule mbaba. Ndiyo baadaye nikampata huyu mzee, ninayeishi naye hadi Mungu atutenganishe.

Kwa hiyo ninachowaambia, msiogope kuachika kuliko mchanike moyoni, kitu cha msingi ni je, wewe ndiye mkosaji au yeye. Kama ni wewe, ona aibu kabisaaa, usikimbie ndoa yako, jishushe, zungumza na mwenzio myamalize, maana katika maisha ya kinyumba, kugongana ni jambo la kawaida.

Lakini kama mkosaji ni yeye, msome. Kuna wengine ujue wanakosea lakini wenyewe hawajui kama wanakosea. Unaweza kuwalaumu kumbe walaaa, hawajui kama wanakukwaza. Sasa hapa lazima uwe makini, unatakiwa umwambie, mwenzangu hivyo unavyofanya mie sipendi!

Anatakiwa ajue kabisa kuwa hupendi, yaani hupendi. Sasa ukiona kila ukimwambia yeye ndiyo kwanza anaendelea, ujue huyo ana lake jambo, usije msichana ukanyauka wakati bado, akhaa. Hata pawe na hela vipi, maisha ya moyo kusononeka hayana ubora!

Na ili uende sawa, usijiondokee tu kama mtu asiye na kwao, wahabarishe wazazi, kwamba jamani mie huku nimeshindwa. Ninavyojua, wao watajaribu kuweka sawa na najua kama huyo mwenzio ndiyo tabia yake, siku zote tabia mazoea, atashindwa tu.

Muda wa kusepa ukifika, usikonde, chukua kilicho chako ujirudie kwenu. Cha msingi, mtaji mkubwa wa mwanamke, ni thamani ya mwili wake, utunze ukusitiri mbele ya safari!

Comments are closed.