The House of Favourite Newspapers

USIOMBE YAKUKUTE… MREMBO YAMFIKA MAZITO MTAANI

WALIANZA kunipigia ndani, baadaye wakanitoa nje wakaanza kunitembeza mtaani huku wakinipiga.”

Simulizi ya Anastazia Ernest mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam inathibitisha kwamba mrembo huyo yamemkuta mazito mtaani, UWAZI linakupakulia mkasa mzima ulivyokuwa.

 

HABARI KAMILI

Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio Mikocheni jijini Dar es Salaam ni kwamba kabla ya Anastazia kuhamia Mbagala alikuwa akiishi na mama yake eneo hili na kwamba siku ya mkasa alikuwa amekwenda kumtembelea mzazi wake huyo anayeishi pia na mtoto wa mrembo huyo.

 

ANASTAZIA AELEZA KIFUPI

“Wakati napita Maria aliniita,” alisema Anastazia akimtaja msichana huyo sambamba na wengine watatu ambao ni Fatuma, Habiba na Rehema ambao inaelezwa kuwa ni mashoga zake wa kitambo kirefu.

 

Mkanda wa maelezo ya mrembo huyo unanukuu fupi kwamba alipoitwa na Maria na kuingia katika nyumba ya Fatuma ambamo kikosi kizima cha maswahiba kilikuwa kimepiga kambi, alianza kupewa kipingo cha mbwa mwizi.

 

Kwa maelezo hayo doti haziungi lakini dodoso kutoka upande wa watuhumiwa zinaeleza kwamba msichana huyo alikwenda nyumbani kwa akina Fatuma na kuiba pasi na deki jambo ambalo Anna analikanusha kwa kusema: “Sikuiba chochote mimi.”

 

UCHUNGUZI  MWINGINE

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi kutoka eneo la tukio unabainisha kwamba mrembo huo alipoingia ndani msichana aliyetajwa kwa jina la Maria ndiye aliyemfungia ndani ya chumba ambapo muda mfupi wenzake watatu ambao anaishi nao nyumba moja walipokuja na kuanza kumfanyia ukatili Annastazia.

 

MREMBO APEWA KIPINGO KIKALI

Video zilizonaswa kutoka eno la tukio zinaonesha kuwa kipingo alichopewa mrembo huyo kilikuwa kikubwa ambapo mwenyewe anasema alishambuliwa mfululizo kwa miko, ndala na mawe hadi nguvu zikamuisha. Kama hilo halitoshi wasichana hao walipasha moto pasi ya umeme na kuanza kumuunguza nayo Annastazia sehemu mbalimbali za mwilini na kumsababshia majeraha.

 

ATEMBEZWA MTAANI

Baada ya kumfanyia kila aina ya unyama walipokuwa wamemdhibiti chumbani wasichana wale watatu walimtoa nje Annastazia na kuendelea kumshushia kipgo huku wakimchania nguo na kuacha sehemu zake nyeti wazi.

 

Video zinaonesha kuwa wakati akifanyiwa unyanyasaji huo mrembo huyo alikuwa ameshika pasi na deki mkononi ambayo wasichana wale walidai kuwa ndiyo vitu alivyokuwa ameiviiba. Hata hivyo, Annastazia anakana kuiba na kudai kuwa alishikishwa kwa nguvu ili kubariki kipigo alichopewa.

 

MWANAUME ATAJWA

Swali la kisa cha mrembo huyo kufanyiwa hivyo lilikuwa la msingi kwa mwandishi wetu ambapo mrembo huyo anaeleza kwamba lilikuwa ni bifu kati yake na Maria. “Maria ana ugomvi na bwanangu Idd. Kuna siku tulikuwa baa Maria alimtukana bwana yangu, akamrushia chupa yule bwana akaanza kumfumua.

 

“Basi mimi nikamwambia Idd aachane na Maria kwa sababu mimi namjua kuwa ni mgomvi, alipomuacha Maria akamwambia wewe si ndiyo umenifanyia hivi lakini ipo siku mwanamke wako kuna siku nitakuja kumfanyia kitu kibaya,” alisimulia Annastazi.

 

Hata hivyo, simulizi yake bado iliacha maswali kwa nini ugomvi uwe kati ya bwana yake na Maria na mtu wa kufanyiwa kitu kibaya awe yeye wakati anakataa kuwa Idd hakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na shoga yake Maria.

 

WATU MTAANI WAPOTEZEA

Ingawa tukio hilo la kinyama limefanyika mchana tena mita chache kutoka zilipo ofisi za serikali ya mtaa usaidizi wa watu kumuokoa Annastazia asishambuliwe hauonekani kwenye video. Kitu pekee kinachoonekana ni mwendelezo wa kipigo kutoka kwa wasichana hao na kupitishwa mtaani akiwa anakokotwa kibabe.

 

APELEKWA POLISI

Huku akiwa na vitu vinavyotajwa kuwa ni vidhibiti vya tuhuma za wizi, mrembo huyo alipelekwa Kituo Kidogo cha Polisi Mikocheni ambako aliwekwa ndani kwa tuhuma za wizi. Inadaiwa kuwa alipofika hapo hakuhojiwa badala yake alitupwa sero na baadaye kuletwa chakula ambacho hakuweza kukila kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.

 

Mama mzazi wa Anastazia aliliambia UWAZI kwamba siku moja baadaye aliambiwa afike kituo cha polisi akamuone mwizi na alipofika huko alimkuta mwanaye. “Bila kujua niliinuka na kwenda, nilipofika huko nilimuona binti yangu akiwa amevalishwa dira, nikamtoa,” alisema mama huyo na kuongeza kuwa walalamikaji hawakutaka kuendelea na shauri hilo.

 

HALI YA ANNASTAZIA YASHITUA

Aidha, mama huyo alieleza kuwa wakati anatoka na mwaneye kuelekea nyumbani hakujua kama alikuwa amejeruhiwa na kwamba walipofika na kuona majeraha aliyopewa na hali aliyokuwa nayo ikabidi waende polisi kufungua mshitaka upya.

 

“Nilipoona majeraha mkubwa mwilini nilishitika nikamuuliza mwanangu mbona hukusema kuwa wamekujeruhi hivyo? Akasema walikuwa wanamchoma na pasi nikasema huu ulikuwa ni uuaji,” alisema mama huyo. Aliongeza kuwa baada ya kufika Kituo cha Polisi Oysterbay walipatiwa fomu namba tatu ‘PF 3’ kwa ajili ya matibabu, ambapo walimpeleka katika Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya matibabu ambako alilazwa.

 

SIRI YA KUVALISHWA DIRA YAVUJA

Inaelezwa kuwa wakati Annastazia anakwenda nyumbani kwa akina Maria alikofanyiwa unyama huo na wanawake wenzake tena marafiki alikuwa amevaa sketi ya jinsi na topu ya mauamaua ambavyo vyote viliharibiwa wakati wa shambulio.

 

Kama hilo halitoshi inadaiwa kuwa watuhumiwa walimvalisha dira mrembo huyo mbali na kumstiri aibu lakini ilikuwa ni pamoja na kuficha majeraha waliyomtia mwilini yasionekane kwa watu na polisi jambo ambalo walifanikiwa.

 

KIBAO CHAWAGEUKIA AKINA MARIA

Mara baada ya taarifa zao kufikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay kibao cha mashtaka kiliwageukia Maria na washirika wake kwa kitendo chao cha kujichukulia sheria mkononi na kujeruhi mtu. Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi wasichana wawili katika sakata hilo Habiba na Fatuma walikamatwa na kwamba Maria na Rehema bado wanasakwa.

 

MAMA FATUMA AFUNGUKA

Mama wa mmoja wa watuhumiwa, Fatuma alifunguka na kudai kuwa yeye siku ya tukio hakuwepo nyumbani kwake huku akiweka wazi kwamba kama angelikuwepo angeweza kuzuia tukio hilo lisifanywe na mwanaye kwa sababu limemletea matatizo makubwa.

 

“Kiukweli nimeumia kwani hapa nimeachiwa mtoto na Fatuma baada ya kukamatwa,” alisema mamahuyo huku machozi yakimlengalenga machoni.

 

NENO LA MHARIRI

Gazeti hili linalaani vikali vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi na badala kuwaomba wananchi kuheshimu sheria za nchi na kufuata utaratibu unaokubalika kisheria yanapotokea makosa kwenye jamii.

 

Rais MAGUFULI Akiendelea na ZIARA Yake Mkoani MTWARA

Comments are closed.