The House of Favourite Newspapers

Usipige Bwana…Tuma Meseji!

0

Bony alikaa sebuleni kwa rafiki yake Mudy akimsikiliza kwa makini kuhusu maelezo yake ya safari yake ya Ulaya kusoma…

“Kwa hiyo rafiki yangu Bony ndiyo hivyo bwana. Ninaomba sana shemejio Aisha aje kuishi nyumbani kwako mpaka nitakapomaliza masomo. Unajua hata ofisi yenyewe imeniambia ghafla tu,” alisema Mudy…

“Sawa bwana Mudy. Bahati nzuri kwa sababu umeniita nikiwa na mke wangu hapo, Neema amesikia, naamini ameafiki mkeo au shemeji yangu aje kuishi kwangu,” alisema Bony huku akimwangalia mkewe ambaye alianza kwa kutingisha kichwa kuashiria amekubaliana…

“Mimi sina neno mume wangu, sina neno shemeji yangu Mudy. Aisha karibu sana nyumbani,” alisema Neema huku akimwangalia mwanamke mwenzake ambaye naye alitingisha kichwa kukubali lakini huku akimwaga machozi…

“Sasa unalia nini mke wangu?” Mudy aliuliza kwa sauti ya upole sana…
“Au hutaki nikasome?” aliendelea kusema Mudy…

“Siyo hivyo mume wangu bali nitakumisi sana. Unajua tumetoka kufunga ndoa hata mwaka mmoja haujaisha tayari umepata safari ya nje kusoma mume wangu…”
“Ndiyo kutafuta maisha shemeji, unatakiwa kuvumilia tu,” alisema Bony akimsihi Aisha kuacha kulia kwa vile mume wake anakwenda masomoni Ulaya.
***
Bony na Mudy ni marafiki kiasili. Wamezaliwa mkoa mmoja wa Morogoro, wakasoma sekondari shule moja, wakaenda chuo kimoja, wote wakaajiriwa na benki moja ya jijini Dar es Salaam.
Mudy ndiye aliyeanza kuoa, alifunga ndoa na Aisha. Msichana mrembo aliyekuwa akisomea biashara kwenye Chuo cha CBE.

Ndoa yake kwa sehemu kubwa ilipigwa tafu na Bony kwani aliisimamia kama ndugu. Baada ya Mudy kufunga ndoa, akafuatia Bony na Neema miezi sita mbele, nayo ilipigwa tafu sana na Mudy.
Sasa wote wakawa wameoa. Mudy aliishi Masaki, Bony Mikocheni. Walijaliwa kuwa na usafiri wa maana na maisha kwao ni kama yalikuwa yamenyooka.

Ndipo sasa Mudy akapata safari ya kwenda kusoma nchini Uingereza kwa mwaka mmoja. Aliomba safari hiyo kwa muda mrefu lakini akaja kushtukiwa ghafla tu kwamba safari iliiva.
***
Siku hiyo ya safari, saa tatu usiku, Mudy alisindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Wasindikizaji walikuwa Bony na mkewe, Neema na Aisha mke wa Mudy.
Kisa cha Mudy kutaka mkewe akaishi kwa Bony ni ukaribu wao na pia, Mudy hakuwa na ndugu Dar na mkewe alikuwa akifanya kazi…

“Mmh! Mmmh! Baby nitakumisi sana tena sana,” alisema Aisha huku akimwangalia mumewe kwa macho yaliyojaa huruma na wasiwasi…

“usiwe na wasiwasi baby, wewe ni mke wangu na nitakuja kukuona ukiwa mzima wa afya njema. Ungekuwa hufanyi kazi ningesema uende nyumbani Morogoro, lakini sasa upo kazini ndiyo maana nimetaka uishi kwa shemejiyo Bony,” alisema Mudy kwa sauti iliyojaa amri na kuhitimisha.
Muda wa wasafiri kuingia kwenye chumba cha kusubiria ndege ulifika, Mudy akawaaga wote kwa kuwachumu, akaenda zake huku Aisha akimwaga machozi. Lakini hakuwa na jinsi.

Wakiwa kwenye gari moja la Mudy wakirejea Mikocheni, Aisha alikuwa akisimulia jinsi ilivyokuwa ngumu mumewe kumwelewa pale aliposema amwache nyumbani…
“Nilimwambia Mudy kwa nini asiniache pale home Masaki, akakataa katakata. Akasema atakuwa na amani mimi nibaki kwenu kuliko kuniacha mwenyewe kwa muda wa mwaka mmoja,” alisema Aisha akiwa anacheka.

Neema naye akacheka na kusema…
“Wivu wote huo. Yaani akuache peke yako ili? Ungekuwa na mtoto tayari angeweza kukuacha.”
“Lakini mimi nadhani shemeji uwezo wa kujitunza kwa kuishi mwenyewe unao. Ila kwangu mimi nisingeweza kumwambia hivyo Mudy, angeona kama nakataa, jambo ambalo lisingekuwa zuri kwa uhusiano wetu,” alisema Bony huku macho yakikaza mbele…
“Kweli kabisa,” alishadadia mkewe, Neema.

Walifika nyumbani kwa Bony, Aisha alishatanguliza kupeleka mabegi yake ya nguo na vitu vingine vidogovidogo siku mbili nyuma. Na tayari alishakabidhiwa chumba cha kuishi kwa muda huo wa mwaka mmoja.

Muda wa kulala ulifika, Aisha alikwenda kulala. Kwa mara ya kwanza tangu amefunga ndoa, alilala mwenyewe siku hiyo.
Mawazo yalimjaa, alimuwaza sana mumewe, alimtakia safari njema na mafanikio mema katika elimu. Alimwambia Mungu amsaidie mume wake.
***
Asubuhi, Bony ndiye alitangulia kuamka, akakaa sebuleni akiangalia habari za ulimwengu kwenye runinga kupitia BBC. Mkewe alipotoka chumbani, akamuuliza kama Aisha alishaaamka…
“Sijamwona, labda kama kaamka halafu amerudi kulala ndani,” alisema Bony huku macho yakikaza kwenye runinga.

Neema alirudi chumbani kwake, akaoga akajiandaa kwenda kazini.
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma chombezo hili jipya kwenye Gazeti la Ijumaa, Ijumaa ijayo.

Leave A Reply