The House of Favourite Newspapers

Usiri Juu ya Rushwa ya Ngono Kwenye Vyumba vya Habari Unakomaza Tatizo Hilo

0

“Nilienda katika chombo fulani cha habari nikiwa na lengo kubwa la kujifunza uhariri wa sauti na video, nilipokelewa na mhariri ambaye alinifundisha kwa siku kadhaa na ghafla siku moja akanieleza juu ya kunihitaji kwake kimapenzi.

“Nilikataa na hapo mambo yakabadilika kwani alianza kunikwepa na hakutaka kunielekeza tena,” anasema Mwamvita Birumo (siyo jina lake halisi), mwanafunzi wa uandishi wa habari.

“Nilimfuata na kutaka kujua juu ya mabadiliko hayo, akadai ili anisaidie kujifunza ni lazima nimpe mwili wangu. Niliripoti kwa mhariri mkuu juu ya jambo hilo lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hivyo ilinilazimu kujifunza kwa mtu mwingine ambaye hata hivyo hakuwa na uzoefu, jambo ambalo liliathiri mafunzo yangu,’’ anasema Birumo.

Usiri juu ya rushwa ya ngono ndani ya vyombo vya habari unazidi kukomaza tatizo hili na kuota mizizi, jambo ambalo linazidi kuhatarisha usalama wa waandishi wachanga.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007 (PCCB Act, 2007), rushwa ya ngono hujitokeza pale mtu aliye katika mamlaka na katika kutekeleza mamlaka yake, anataka au anaweka upendeleo wa ngono kama kigezo cha kutoa ajira, cheo, haki au huduma ya upendeleo.

Kimsingi, rushwa ya ngono imekuwa ikiathiri watu wengi hasa wanawake wakiwamo wanahabari hadi kushusha ufanisi katika utendaji kazi wao.

Wanafunzi wanawake kutoka vyuoni wanapokwenda katika baadhi ya vyombo vya habari kwa ajili ya mafunzo wanakumbana na kadhia hii, jambo ambalo linaathiri mafunzo yao kwani wanashindwa kujifunza kwa kujiamini.

Kwa upande mwingine, ufanisi ndani ya vyombo vya habari unaweza kupungua kwa kuwa wanaoajiriwa huweza kukosa vigezo na wale wenye vigezo kukosa fursa kwa kuwa tu hawajatoa miili yao.

Wahariri nao kama kiungo muhimu ndani ya vyumba vya habari, wanatambua changamoto wanazokumbana nazo waandishi wa habari wanawake hasa wale wachanga kwenye tasnia hii ya habari.

“Mazingira ya ndani ya vyumba vya habari si rafiki kwa waandishi wa habari wanawake kwani wao wapo kwenye hatari zaidi ya kupitia unyanyasaji wa kijinsia au rushwa ya ngono,” alisema Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena.

“Lakini pia mifumo dume iliyojengeka ndani ya vyumba vya habari nayo inachangia kwani idadi ya wahariri wanaume ni kubwa ukilinganisha na ile ya wahariri wanawake. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa hatari ya waandishi wanawake kupitia unyanyasaji wa kijinsia na hata kuombwa rushwa ya ngono si tu na wahariri bali hata waandishi,” anasema Meena.

Nguvu ya madaraka waliyokuwa nayo wahariri juu ya waandishi wa habari ni sababu nyingine inayosababisha rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari, kwani barua za maombi ya kujifunza kwa vitendo hupita kwao lakini pia ni wao ambao huamua juu ya kazi za waandishi.

“Wahariri wanapata kipaumbele kwani wanaoalikwa katika vyumba vya habari barua zao mara nyingi hupita kwa mhariri,” anaongeza Meena.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inakiri kuwepo kwa rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na kuwa usiri juu ya jambo hili kwa wahanga unaendelea kuwaweka hatarini.

“Suala la ngono ni suala linalohusisha utu wa mtu, mila na desturi za Kiafrika hivyo si suala linalowekwa wazi hivyo wengi hawapo tayari kutoa taarifa,” anasema Afisa Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, Dorothea Mrema.

 

Imeandikwa na Rukia Mohamed.

 

Leave A Reply