The House of Favourite Newspapers

USISIKILIZE WATU PEMBENI LAKINI KUWA MAKINI, LISEMWALO LIPO

UNAPOKUWA kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu unayempenda kwa dhati, unakuwa ni kama umepigwa na upofu fulani hivi, huwezi kusikia chochote kinachozungumzwa pembeni kuhusu huyo uliyenaye. 

 

Hivyo ndivyo mapenzi yalivyo, moyo unapopenda akili huwekwa kando, hata kama watu wote watakuwa wanamzungumzia vibaya huyo uliyenaye, maadam umempenda, huwezi kuwasikiliza hata kidogo. 

 

Hata hivyo, hisia za mapenzi huwa na kawaida ya kupanda na kushuka. Leo unaweza kuwa na hisia kali juu yake lakini miezi michache baadaye, utaona hisia zinapungua taratibu na hapo sasa akili zinaanza kufanya kazi. Ni katika kipindi hiki ndipo yale uliyokuwa ukiambiwa wakati fulani lakini ukaweka pamba masikioni, huanza kujirudia ndani ya kichwa chako au wakati mwingine huanza kujidhihirisha na kukufanya uyashuhudie mwenyewe.

 

Mahusiano mengi huwa yanaanza kulegalega katika kipindi hiki na ndiyo sababu wengi wakianzisha uhusiano, huwa hawawezi kudumu kwa sababu kuna mambo waliyapuuza mwanzo kabisa mwa mapenzi yao wakiamini siyo tatizo, lakini sasa hugeuka na kuwa kikwazo kikubwa.

 

Nimekuwa nikizungumza mara nyingi hapo nyuma kwamba kabla hujaamua kuukabidhi moyo wako kwa mtu fulani, kabla hujaamua kumpenda kwa dhati, ni vyema ukapata muda wa kutosha wa kumfahamu kwa undani. Hii itakusaidia kwamba hata baadaye utakapokuwa umekolea penzini halafu wambeya wakawa wanakuletea maneno, yatakuwa ni kama marudio kwako kwa sababu tayari unamjua kwa undani huyo uliyenaye.

Hapa sasa hata ukiamua kuweka pamba masikioni, itakuwa ni sahihi na mahusiano mengi yenye kufuata mfumo huu, hudumu kwa kipindi kirefu sana. Usione watu wameishi pamoja miaka chungu nzima ukawa unajiuliza wamewezaje?

 

Walijenga msingi imara wa penzi lao tangu mwanzo, walipata muda wa kufahamiana na kujuana kwa undani tangu mwanzo. Muda pekee ambao unatakiwa kufungua macho na masikio yako, ni kipindi ambacho unataka kuanzisha uhusiano na mtu fulani, siyo wakati mkiwa mmeshaanzisha.

 

Nguvu ya mapenzi jinsi ilivyo, mpenzi wako anaweza kuwa mwizi na watu wakakueleza kwamba huyu jamaa ni mwizi mzoefu, lakini kwa sababu tayari kuna mapenzi katikati yenu, utaona kama anasingiziwa na mwisho utaishia kuwachukia waliokwambia, siku akija kukamatwa kwenye tukio la wizi ndipo unapoanza kujiona huna akili.

 

Unaweza kuelezwa kabisa kwamba huyu mwanamke unayetaka kumuoa, ameshindikana, mtaani wanamuita maharage ya Mbeya, maji mara moja tu, lakini kwa sababu unampenda, utawaona kama wanakuonea wivu, utamchukia kila mtu, siku ukija kumfumania chumbani ndiyo akili inakukaa sawa.

Hoja ya msingi ambayo nitaendelea kukusisitiza, ni kwamba usikurupuke kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi. Usimuone mwanamke ana shepu nzuri, nyuma kajazia basi matamanio ya mwili yakakufanya uamini kwamba huyo anaweza kuwa mkeo.

 

Usimuone mwanaume ‘hendisamu’, anatembelea gari, ana fedha basi ukajua tayari umeshapata mume. Mchunguze kwanza kwa sababu usipokuwa makini, utakuwa unaukaribisha msiba wa nafsi kwenye maisha yako.

 

Unapofanya uchunguzi wako, wasikilize watu wanaomjua wanachokisema kisha pata muda wa kuchuja, sisemi kwamba kila watakachokwambia kitakuwa ni kweli, lakini angalau utapata mwanga kwamba yeye ni mtu wa aina gani. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri

Comments are closed.