USIYOYAJUA KUHUSU MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CAG)

CAG Prof. Musa Assad akimkabidhi ripoti ya ukaguzi, Rais Dk. John Magufuli.

MWEZI Aprili mwaka huu umeanza na mjadala mkubwa juu ya ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali baada ya Bunge kukataa kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG) Profesa Musa Juma Assad.

 

Jambo hili ni pana hasa katika nyanja ya uchumi wa taifa kwa sababu yapo mambo kadhaa yanayooneshwa na CAG katika ripoti yake ya taarifa ya fedha za serikali kuu kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30. Hii ni ripoti kubwa sana.

Ukaguzi huo hufanywa kwa mujibu wa katiba chini ya Ibara ya 143 (4) pamoja na kifungu cha 34 (1) (C) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 sambamba na kanuni zake za mwaka 2009.

 

Ni ripoti inayokagua mambo mbalimbali kama vile matumizi ya fedha, sheria, mifumo ya ndani na masuala ya utawala wa Serikali Kuu, mafaili ya pensheni, ukaguzi maalum chini ya Serikali kuu na ukaguzi wa vyama vya siasa nk.

Kwa maelezo hayo mafupi ni dhahiri kwamba hii ni taasisi kuu ya ukaguzi katika sekta ya umma kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imekuwepo tangu zama za ukoloni ikiendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kulingana na wakati husika.

 

Wakati wa utawala wa Mwingereza ofisi hii ilijulikana kama Idara ya Ukaguzi ya Kikoloni na ilikuwa ikiripoti kwa Gavana ambaye alimwakilisha Malkia wa Uingereza. Wakati huo maofisa waligawanywa katika madaraja makuu matatu ambayo ni Ajira ya Mafao ya Ulaya, ngazi ya maafisa (Europian Pension Scheme- Officers Rank), Ajira ya Mafao ya Asia, ngazi ya ukaguzi wa hesabu (Asian Pension Scheme – Examiners of Accounts) na Ajira ya Mafao ya Afrika, ngazi ya makarani wa ukaguzi (Audit Clerks).

CAG Prof. Musa Assad (kushoto) akimkabidhi ripoti ya ukaguzi Rais Dk. Jakaya Kikwete enzi za utawala wake.

Kipindi chote hiki, ofisi hii ilikuwa ikiongozwa na Mkurugenzi wa Ukaguzi (Director of Audit) kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi Sura 386 (Audit Ordinance Cap. 386) hadi ilipoanzishwa Sheria ya Fedha na Ukaguzi ya mwaka 1961 (Exchequer and Audit Ordinance 1961) iliyobadilisha jina la cheo cha mkuu wa taasisi hii kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

 

Wakati na baada ya uhuru, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imekuwa ikijitegemea kimuundo na kiutendaji kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1961, ibara ya 73 ambayo ilitambua uwepo na kutoa mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Controller and Auditing General- CAG)) Lambaye ndiye kiongozi mkuu wa taasisi kama inavyoonekana pia katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ambaye sasa ni Professa Musa Juma Assad.

 

Hivi sasa mamlaka na wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) umefafanuliwa na kuainishwa katika Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nilivyosema hapo juu.

Nia ya ukaguzi ni kuhakikisha kwamba fedha zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na matumizi yake yanafanywa kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 143 ya Katiba ya Tanzania.

 

Katiba hiyohiyo inasisitiza kuwa katika kutekeleza majukumu yake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali.

Hata hivyo, mahakama imepewa nguvu katika ibara ndogo ya 143 ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Tanzania kwa kadri itavyoona inafaa.

 

MAKALA: Elvan Stambuli


Loading...

Toa comment