The House of Favourite Newspapers

USIYOYAJUA KUKUHU MAISHA HALISI YA MOZE IYOBO, AANIKA KILA KITU

MIONGONI mwa vijana wanaohamasisha vijana wenzao katika kujituma na kuendeleza vipaji vyao, yumo dansa maarufu anayeitumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Moses Peter Iyobo almaarufu Moze Iyobo. Jamaa huyu ni dansa matata wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye yupo naye tangu anaanza muziki hadi sasa.

 

Iyobo anasema amepitia kwenye changamoto nyingi kutokana na watu kudharau kazi ya kudansi na kuona kama hailipi, lakini ameonesha watu kuwa kazi ni kazi na ukiifanya kwa ubunifu utatoboa.

 

Ndiyo maana mpaka leo anaendesha maisha yake kupitia kudansi na hata kusafiri sehemu mbalimbali duniani kwa kipaji chake hicho. Iyobo amekuwa hamasa kwa vijana wengi mtaani leo.

Wengi sasa wanajifunza kucheza kwa sababu wanataka kuwa kama Iyobo, yote hiyo ni kwa sababu alithamini na kupenda kipaji chake na ndiyo maana leo kinampa heshima na kila mtu anataka kuwa kama yeye. Mwandishi wetu amefanya mahojiano na Iyobo ili kuweza kujua mawili-matatu kutoka kwake.

Ulikutana wapi na Diamond hadi kufikia kufanya naye kazi? Iyobo: Diamond nimesoma naye shule ya msingi, ingawa yeye alikuwa juu yangu, alinizidi madarasa mawili, akamaliza shule na mimi nikamaliza, kila mtu akaenda kivyake ila tukaja kukutana kwenye mashindano yaliyohusu madansa na waimbaji, mimi nikiwa nacheza yeye anaimba kipindi bado hajawa msanii mkubwa, ndiyo akaniomba tukaanza kufanya kazi pamoja.
Una elimu gani? Iyobo: Elimu yangu ni darasa la saba, sikufanikiwa kusoma sana.


Changamoto ipi unaipata kufanya kazi na Diamond? Iyobo: Changamoto ninayopata kwa kufanya kazi na Diamond ni kwamba watu muda wote wanadhani nipo naye (Diamond). Hata kama nipo katika matembezi yangu binafsi, unakuta mtu anakuja anakwambia; ‘oya Simba (Diamond) umemuacha wapi? Au shoo lini, yaani ni tafran ila mengine yote tunakwenda sawa.

Wewe ni dansa wa Diamond tu au na sehemu nyingine pia unafanya?

Iyobo: Sijawahi kufanya na mtu mwingine zaidi yake ila hajawahi kunikataza kufanya na mtu mwingine. Kwa hiyo kama ikitokea mtu anataka kufanya kazi na mimi ruksa, kikubwa makubaliano tu.

Nini siri ya mafanikio yako?

Iyobo: Siri ya mafanikio yangu ni kujituma katika kazi zangu, kuwa mbunifu kila siku na kuheshimu kila mtu anayenizunguka.


Mbali na Cookie na Jayden, je, una mtoto mwingine? Iyobo: Hapana, sina mtoto mwingine zaidi ya watoto wangu hao wawili na wanajulikana kila sehemu kuwa ni watoto wangu.

Hivi karibuni zilisikika tetesi kuwa uliachana na mama cookie (Aunt), je, ni kweli? Na ni nini chanzo cha ugomvi wenu?

Iyobo: Mimi na Mama Cookie hatujawahi kuachana ila tumeshawahi kupishana kauli zaidi ya mara mbili na huwa tunamaliza tofauti zetu wenyewe na maisha yanaendelea.

Tutegemee lini ndoa yako na aunt? I

yobo: Kwa jinsi tunavyoishi ni ndoa tayari kwa sababu tunakaa pamoja, Mungu ametujalia mtoto mzuri (Cookie), yaani sisi ni kama wanandoa bado sherehe tu ambayo muda wowote tutafanya wala haina haraka.

Mbali na dansi, ni ishu gani nyingine unafanya?

Iyobo: Hakuna kingine, nafanya dansi ndiyo maisha yangu, nafundisha dansi kwa wanaotaka kujifunza. Pia ni mtayarishaji wa dansi za kwenye video za wasanii mbalimbali. Lakini sitegemei kuwa dansa maisha yangu yote kwani kuna vitu ninaviweka sawa, vikikamilika mtaviona. Unadhani madansa wengine wanakosea wapi hadi wanashindwa kutimiza ndoto zao?

Iyobo: Wanakata tamaa haraka, wanashindwa kujua kwamba dansi ni kazi kama kazi nyingine, hivyo ukiifanya kwa moyo na mapenzi, lazima itakulipa, lakini ukiifanya kama kitu cha ziada, huwezi kufika unapotaka.

Kuna watu wanadharau kazi za wenzao, wewe hilo unalizungumziaje?

Iyobo: Mwanzoni nilikuwa najisikia vibaya sana wakati sijapata matunda yoyote kutokana na dansi, lakini sasa hivi mtu akidharau kazi yangu, kwanza namuona hana akili kwa sababu kwenye kazi hiyo wanayoidharau mimi ndiyo naendesha maisha yangu.

 

Wakati wao wanapanga bajeti ya kula elfu kumi, mimi natumia hiyo kuweka vocha ya kumpigia mwanangu Cookie.
Kuna watu wana ndoto za kuwa kama wewe, una kipi cha kuwaambia?

 

Iyobo: Kikubwa wajitume, wasikate tamaa, waamini katika wanachokifanya kwa sababu mwanzo ni mgumu, hata mimi wakati naanza niliwahi kukata tamaa ila sikuacha, nilijipa moyo siku moja nitatimiza ndoto zangu na leo hii niko hapa na watu wananifahamu kupitia kipaji changu hikihiki.

Comments are closed.