The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!-6

0

ILIPOISHIA:
“Tumechoshwa na uchawi hapa kijijini kwetu. Kwa pamoja tumefanikisha ujio wa mganga Mabwanji kutoka Malawi kwa lengo la kusafisha kijiji chetu. Wale wote waliokuwa wanaringia uchawi wao, kiboko yao amewasili, karibu uwasalimie wanakijiji,” alisema mzee wa kimila pale kijijini ambaye tulizoea kumuita Mwene.

SASA ENDELEA…

Mwanaume mzee mwenye macho mekundu sana na midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi, kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu wote wakashangilia kwa nguvu.

“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo, akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.

Baada ya maelezo marefu yaliyojaa vitisho kwa watu waliokuwa wakitajwa kuhusika na uchawi, mkutano uliahirishwa, watu wakatawanyika huku kiongozi huyo wa kijiji akiwataka watu wote kutoa ushirikiano kwa mganga Mabwanji atakapoenda kuwatembelea kwenye nyumba zao.

Hofu niliyokuwa nayo ilikuwa kubwa mno, kwa jinsi watu walivyokuwa wanatuchukia pale kijijini nilijua lazima moto utawaka. Baadhi ya wazee waliokuwa wanaheshimika pale kijijini, walianza maandalizi ya kumsaidia mganga huyo kwa kila alichokuwa anakihitaji, dawa zikaandaliwa na hatimaye muda uliokuwa ukisubiriwa na wengi ukawadia.

Saa tatu juu ya alama usiku, kazi ya kuzunguka kwenye nyumba za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa wachawi ilianza, kutokana na jinsi nilivyokuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kazi hiyo inavyofanyika, nilichomoka nyumbani kimyakimya na kwenda kushuhudia licha ya kwamba baba alitutaka wote tukae ndani kwa sababu siku hiyo ilikuwa mbaya kwa familia yetu.

Mtu wa kwanza kufuatwa alikuwa ni mwanamke mjane ambaye tulizoea kumuita mama Chinga, Mmakonde kutoka Kusini aliyekuwa akifanya kazi ya kupika pombe za kienyeji.

Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikiasikia kwamba eti mwanamke huyo alikuwa akitumia viungo vya binadamu kupikia pombe zake ndiyo maana alikuwa na wateja wengi sana hapo kijijini. Tangu nikiwa mdogo niliaminishwa kwamba eti ule ambao huwa tunaona kama ni mwiko mkubwa anaoutumia kukorogea mapipa yake ya pombe, ulikuwa ni mkono wa binadamu.

Watu hao walipofika, huku ngoma ikipigwa na pembe za wanyama zikipulizwa, kila mtu akiwa ameshika tochi za kienyeji ambazo hutengenezwa kwa kuviringisha matambara mbele ya kipande cha mti kisha kuchovya kwenye mafuta ya taa, nyumba yake ilizungukwa kisha mganga akaanza kazi yake.
Akawa anafanya uchawi wake pale, mara afukue kwenye kona ya nyumba na kutoa hirizi kubwa, mara afukue pembeni ya mlango na kutoa fuvu la mnyama wa ajabu, yaani ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.

Mwanamke huyo na yeye akatolewa na kukalishwa chini, mbele ya nyumba yake, akapakwa unga mweupe kichwani na kuanza kunyolewa nywele huku ngoma zikiendelea kupigwa, mganga akawa anaimba nyimbo za ajabu na kumtolea vitisho vingi mwanamke huyo kwamba akirudia tena kujihusisha na uchawi lazima atakufa.

Baada ya zoezi hilo lililochukua karibu saa zima, watu wote waliondoka na kumuacha mwanamke huyo akilia kwa uchungu, huku akiendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi wala haujui uchawi. Safari ya kuelekea kwenye nyumba nyingine ikaanza, na mimi nikawa nawafuata kwa nyuma.

Cha ajabu, niliwaona wakielekea nyumbani kwetu, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, sikujua mwisho wake utakuwaje. Walipofika, walifanya kama walivyofanya kwa yule mwanamke, wakaizunguka nyumba yetu huku wakiimulika na tochi za kienyeji, ngoma ikawa inapigwa huku mganga akiimba nyimbo ambazo hakuna aliyekuwa anazielewa.

Akawa anazunguka huku na kule kama anayetafuta kitu fulani pale nje kwetu, ghafla nikaona mlango ukifunguliwa, baba akatoka kwa kasi na kuwapita watu wote, akasogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amesimama, wakawa wanatazamana.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply