
MADAI ya hoteli ya kitalii na kifahari ya nyota tano ya Ngurdoto Mountain Lodge ya jijini Arusha ya kugeuzwa hosteli za wanafunzi, yameibua jambo jipya.
Hoteli hiyo iliyopo eneo la Usa-River, Arumeru jijini Arusha, inatajwa kuwa sehemu ya utajiri wa kufuru aliouachwa marehemu Bilionea Melau Mrema almaarufu Bilionea wa Ngurdoto aliyefariki dunia, Agosti, mwaka 2017.
Habari za hoteli hiyo kugeuzwa hosteli na kutumiwa na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu cha Arusha (AIA) ndizo zimeibua gumzo la mali nyingine alizoziacha tajiri huyo.
Mbali na Ngurdoto, Bilionea Mrema anatajwa kuacha utajiri mwingine wa kufuru ambao ni hoteli za kitalii na kifahari za Impala za Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro na ile kubwa ya Naura Springs iliyopo eneo la Sanawari jijini Arusha.

NGURDOTO
Ngurdoto inatajwa kuwa miongoni mwa hoteli za hadhi ya juu kabisa nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Tovuti ya Ngurdoto, hoteli hiyo ilifunguliwa mwaka 2003 na ina vyumba 300 vikiwemo vya kulaza wakuu wa nchi (Marais) wapatao saba na wasaidizi wao.
Tovuti hiyo inaeleza kuwa, hoteli hiyo pia ina kumbi zaidi ya tano zenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 3,000 kwa wakati mmoja.
Kabla ya ‘mambo kuharibika’ kipindi cha nyuma, ili kulala kwenye hoteli hiyo ungetakiwa kulipia shilingi 450,000 hadi milioni 3 kulala kwenye vyumba vya wageni maarufu (VIP) ndani ya hoteli hiyo.
Wakati haya yanajiri, yanazirudisha kumbukumbu za Ngurdoto iliyoendesha mikutano mikubwa kati ya mwaka 2005 na 2010 ikiwemo ule mkutano mkubwa wa Sullivan mwaka 2008.
IMPALA
Mbali na Ngurdoto, utajiri mwingine aliouacha bilionea huyo ni Hoteli ya Impala iliyopo eneo la Kijenge, Round-About jijini Arusha.
Kwa mujibu wa watu waliopatiwa huduma ndani ya Impala Hotel, gharama ya kulala usiku mmoja kwenye chumba cha kawaida ni kuanzia Dola za Kimarekani 220 kwa mtu mmoja.
Kwa vyumba vya hadhi ya juu kabisa ni kuanzia Dola za Kimarekani 2000 kwa siku na hizo ni gharama za malazi tu, bado matunizi mengine.
NAURA SPRING
Ukiacha Ngurdoto na Impala, pia bilionea huyo ameacha hoteli nyingine ya kifahari ya Naura Springs iliyopo eneo la Sanawari pembezoni mwa Mto Goliondoi jijini Arusha
Naura Springs nayo inatajwa kuwa ni hoteli ya nyota tano na ipo kwenye orodha ya hoteli kubwa nchini Tanzania.Kwa mujibu wa wahudumu wa hoteli hiyo, gharama za kulala kwa usiku mmoja huanzia Dola za Kimarekani 200 kwa chumba cha kawaida au executive room.
Kwa upande wa vyumba vya VIP au presidential villa, gharama zake huanzia Dola za Kimarekani 2000 kwa usiku mmoja na kwa mtu mmoja.
MAKAMPUNI YA UTALII
Mbali na hoteli hizo, wakati wa uhai wake, bilionea huyo alikuwa akimiliki makapuni kadhaa ya utalii ikiwemo Classic Tours and Safaris ya mkoani Arusha na Kilimanjaro ambayo ina idadi kubwa ya magari ya kusafirisha watalii kwenda porini.

UMILIKI WA SASA
Wosia aliouacha Bilionea Mrema, unamtaja Joan Mrema ambaye ni mwanaye wa kike kuwa ndiye msimamizi na mkurugenzi wa Hoteli ya Ngurdoto.
Pia Wosia huo unamtaja Randy Mrema ambaye ni mwanaye wa kiume kuwa ndiye msimamizi na mkurugenzi wa Hoteli za Impala na Naura Springs.
Bilionea Mrema alifariki katika Hospitali ya Garden City nchini Afrika Kusini wakati akipatiwa saratani ya mifupa na alipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika eneo hilo la Hoteli ya Ngurdoto.
STORI: MWANDISHI WETU, ARUSHA

