Utajiri wa haraka unapatika kupitia namna hii
Wananchi wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro wameshauriwa kutumia nyuzi zinazotokana na migomba ikiwa ni chanzo cha kujipatia kipato kwa kutumia nyuzi za migomba kutengeneza vifaa mbalimbali.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) baada ya kupewa nafasi ya kutoa salamu katika kikao hicho.
Dk Mussa amesema nyuzi za migomba ni chanzo kimoja cha kujipatia kipato kutokana na zao hilo kuwa umuhimu wake hasa katika kutengeneza vifaa mbalimbali vikiwemo vikapu, mikoba, mikeka, vitambaa na hata taulo za kike.
“Tuliloligundua na wataalamu wangu, kuwa migomba ni utajiri kupitia nyuzi zake na tukijipanga vizuri tunaweza kusaidia kunyanyua mapato..”
Katibu Tawala huyo amezishauri Halmashauri za mkoa wa Morogoro yanayostawisha zao hilo kutotupa migomba hiyo badala yake wachangamkie fursa hiyo kuitumia kama moja ya chanzo cha kukuza mapato ya Halmashauri na kukuza Uchumi wa jamii inayowazunguka.
Aidha, Dkt. Mussa Ali Mussa amebainisha kuwa mashine inayotumika kutengeneza bidhaa hizo zinazotokana na migomba ikiwemo mikoba, vikapu, mikeka, nguo n.k. kwa kutumia nyuzi zake inapatikana Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA Mikumi, Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kwa bei ndogo ya shilingi 1.5 Mil.