The House of Favourite Newspapers

Utajiri Wa Kakobe Siri Yavuja! Uwazi Labaini Kanisa Lake Linavyovuna Mabilioni

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe.

 

SIKU chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe kutoa kauli kuwa ana fedha nyingi kuliko serikali, siri ya utajiri wa mtumishi huyo wa Mungu imefichuka.

Baada ya kutoa kauli hiyo kanisani kwake Jumapili ya wiki iliyopita, mjadala mkali umeibuka kuhusu ukweli wa maneno hayo, huku Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikitaka kufanya uchunguzi ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote wa sheria.

 

UWAZI LAINGIA KAZINI

Ili kujiridhisha kuhusu ukweli wa kauli yake, Uwazi liliingia mtaani na kanisani kwake na kuanza kudodosa ili kupata uhakika kutoka kwa wadau ambao bila kupepesa macho, walisema upo uwezekano mkubwa wa mtumishi huyo wa Mungu kuwa na fedha nyingi kutokana na muda alioanza kutoa huduma, pamoja na ukubwa wa kanisa analoliongoza japokuwa walikiri kuwa na vitega uchumi kama viwanda na mashamba makubwa.

 

MUUMINI KANISANI KWAKE MWENGE

Muumini mmoja wa kanisa hilo lililopo Barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina moja la Issac, alisema amemtambua Askofu Kakobe tangu mwaka 1989 na kila siku huduma yake imekuwa ikikua na kupata wafuasi wengi.

“Kitu pekee ninachokijua kinacholiingizia kanisa fedha ni sadaka siyo miradi ya kiuchumi, hapa kuna waumini wengi na wote ni watoaji wa sadaka, lakini pia kuna matawi katika kila wilaya nchi nzima, unafikiri ni kiasi gani cha fedha kanisa linakusanya?” alihoji muumini huyo.

 

Muumini huyo alisema TRA hawawezi kuambulia chochote kwa sababu kanisa halina mradi wowote zaidi ya kufanya ibada ya kuombea roho za watu.

MTANDAO WA KANISA WAIBUA KILA KITU

Katika mtandao wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, unaonyesha kuwa kanisa hilo lina matawi karibu kila sehemu nchini, lakini baadhi ya makanisa hayo yakiwa katika maeneo 63, ambayo ni makubwa na yenye wafuasi wengi.

 

HAYA HAPA MATAWI YA KANISA LAKE

Tofauti na makanisa mengine ya aina ya kanisa lake, ambayo matawi yake ni machache tena yakiwa katika miji mikubwa pekee, Uwazi limegundua kuwepo kwa makanisa hayo 63 maeneo ya Arusha, Bukoba, Bunda, Dodoma, Geita, Iringa, Itumba, Kahama, Kakola, Kakonko, Karagwe, Karatu, Kasulu, Kibondo, Kigoma, Kilindoni, Kingerikiti, Kisarawe, Kondoa, Korogwe na Kyela.

 

Mengine yapo Ludewa, Lushoto, Mabamba, Magu, Makambako, Makiungu, Masasi, Matembwe, Mbeya, Mbinga, Mbulu, Mererani, Misasi, Mlandizi, Morogoro, Mpwapwa, Mtwara, Muheza, Mwanza, na Mwese.

 

Pia yapo Nachingwea, Nansio, Ngara, Ngudu, Njombe, Rujewa, Runzewe, Same, Sengerema, Shinyanga, Sikonge, Singida, Songea, Sumbawanga, Tabora, Tanga, Tukuyu, Tunduru, Turiani, Urambo, Usa-River na Vwawa.


KIASI CHA FEDHA ANACHOWEZA KUPATA

Licha ya ukweli kwamba kanisa hilo lipo karibu kila mkoa na wilaya nchini, kwa kufanya makadirio ya makanisa ndani ya wilaya 185 (mojamoja kila wilaya) zilizopo nchini kwa sasa, zinazoweza kuwa zimekusanywa hadi sasa, ni mabilioni ya shilingi.

Hesabu rahisi za makusanyo ya sadaka pekee kwa ibada tatu kwa wiki ni wastani wa shilingi milioni mbili kwa ibada moja, hivyo kwa ibada hizo kanisa hilo linaweza kuingiza zaidi ya shilingi bilioni moja kwa kipindi hicho.

 

Kwa maana hiyo, kanisa hilo linaweza kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 4.4 kwa mwezi, ambapo kwa mwaka ni mabilioni ya shilingi, ambazo kisheria hazitozwi kodi kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Charles Kichere.

Askofu Kakobe anatajwa kutoa huduma za kiroho pia katika nchi za Marekani, Canada, Sweden, Norway, Denmark na Finland ambako haijulikani kama ana makanisa au la.

 

KAKOBE AFAFANUA UTAJIRI WAKE

Akielezea mali zake juzi Jumapili kanisani kwake, Askofu Kakobe alisema mwaka 2006 alipiga picha maeneo yote ya ndani na nje ya nyumba yake iliyopo Mabatini Kijitonyama, Dar es Salaam na kuonesha kwenye runinga.

Kakobe alisema nyumba hiyo ambayo anaishi hadi leo aliijenga mwaka 1986 kwa shilingi milioni mbili ikiwa ni gharama ya kila kitu hadi kiwanja.

 

“Tangu kanisa lianze mwaka 1989 sijajenga nyumba yoyote. Mwaka 1995 nilinunua gari aina ya Nissan Patrol kwa kutumia sadaka za washarika wa kanisa.

“Majuzi waliibuka watu walijichangisha bila mimi kujua wakanipa zawadi ya gari mnaloliona hapo nje, wangeniambia nisingekubali,” alisema Askofu Kakobe na kusisitiza kuwa hata kijijini kwake Kakonko hata choo hajajenga.

“Mwaka 2006 nilisema kwenye runinga kuwa sina shamba, sifugi kuku wala ndege yoyote. Anayejua mali zangu ajitokeze hadharani, lakini imepita miaka kumi na moja hakuna aliyejitokeza, hata fundi ujenzi angeweza kusema maana ujenzi siyo siri,” alisema.

 

Akifafanua kuhusu madai ya miradi ya kanisa, alisema ndani na nje ya nchi, kanisa la FGBF halina mradi wowote wa kiuchumi kama shamba au hoteli na ameitaka serikali kuchunguza ili ijue ukweli.

 

AZUNGUMZIA SADAKA

Akizungumzia sadaka kiongozi huyo wa kidini, alisema makusanyo yote ya sadaka huhifadhiwa katika akaunti iliyofunguliwa mwaka 1990 katika Benki ya NBC na ni mali ya Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la FGBF ambayo imesajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

 

“Wokovu ni utajiri wa Kristo usiopimika, narudia, Askofui Kakobe mi tajiri kuliko Serikali ya Tanzania, Marekani, Ujerumani na mataifa yote makubwa unayoweza kuyafahamu,” alisema Askofu Kakobe.

Pamoja na hayo, hajawahi kusema kama ana ndege kama walivyo baadhi ya wachungaji nchini au kumiliki nyumba ya kifahari japokuwa alisema amepata taarifa kuwa kuna maaskofu, wachungaji na waumini wanachangishana ili kumjengea nyumba ambayo hajaiona wala kujua iliko.

 

KAMISHNA WA TRA ANENA

Wakati hayo yakiendelea, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema kwa kawaida fedha za sadaka huwa hazitozwi kodi.

Alipoulizwa kwa nini uhakiki kwa Kakobe ufanyike sasa na siyo miaka ya nyuma, alisema ni baada ya kusikia kwamba ana fedha nyingi kuliko serikali wakati anafahamika ni kiongozi wa taasisi ya dini.

STORI NA MWANDISHI WETU | GAZETI LA UWAZI

Comments are closed.