UTAJIRI WA MBUNGE MATIKO BALAA

FEDHA inaongea! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia ukwasi anaodaiwa kuwa nao Mbunge wa Tarime-Mjini, Ester Matiko, Gazeti la Ijumaa Wikienda linakudondoshea ubuyu kamili!  Sehemu kubwa ya utajiri wa mbunge huyo machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inatajwa kuwa jijini Dar huku pia akiwekeza kwenye jimboni kwake Tarime-Mjini.

TUJIUNGE NA MTOA TAARIFA

Mtoa taarifa ambaye anamfahamu kinagaubaga mbunge huyo msomi aliyehifadhi kichwani Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara na Fedha (MBA), ameeleza kuwa mbali na kuwa na mtonyo wa kutosha kusukuma maisha, Matiko anamiliki mijengo mitatu ya kifahari jijini Dar. “Ni mfano wa kuigwa kwa mabinti ambao wanapenda kujifunza kupitia watu waliozichanga fedha kutokea chini hadi kuwa nyingi.

“Amepambana akiwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka hiyo, akaingia kwenye ubunge wa viti maalum na baadaye wa kuchaguliwa, akapita, hili si jambo ndogo,” alisema mtu huyo. Mtoa taarifa huyo alizidi kuweka bayana kuwa, nyumba hizo za kifahari anazomiliki zipo katika maeneo tofauti jijini Dar ikiwemo anayoishi yeye iliyopo maeneo ya Mashuka, Goba jijini Dar.

“Siyo wa mchezomchezo, kama mnataka kumjua zaidi, nendeni pale kwake Goba mkajionee wenyewe kwani pale ndipo anapoishi na mtaona jinsi parking yake ilivyosheheni magari,” alisema. Baada ya kushibishwa taarifa hiyo, Gazeti la Ijumaa Wikienda liliona hakuna sababu ya kupoteza muda, moja kwa moja likafunga safari hadi Goba na kujionea moja kati ya mijengo anayomiliki mbunge huyo.

Ijumaa Wikienda lilishuhudia mjengo huo wa ghorofa moja wenye rangi nyeupe ukiwa na bonge la nafasi ndani huku parking ikiwa imependeza mikoko kama 6 ikiwemo Land Rover Discovery 3.

Gazeti la Ijumaa Wikienda lilipomaliza kuchukua picha na mandhari nzima ya mjengo huo, liliweza kuzungumza na mbunge huyo kuhusu ukwasi huo anaotajwa kuwa nao ambapo alisema kwake hivyo si kitu kwani bado ana ndoto kubwa zaidi.

“Namshukuru Mungu kwa hivi nilivyo sasa, lakini bado nina ndoto kubwa zaidi ya hapa unavyoniona,” alisema. Alipoulizwa kuhusu mijengo mitatu ambayo ilielezwa anaimiliki jijini Dar, mbunge huyo alikiri na kusema aliipata kabla hata hajawa mbunge.

“Hizi nilijenga pamoja na mume wangu kabla hata sijawa mbunge, kipindi hicho nilikuwa ninafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Unajua hivi vitu vinawezekana kama tu utaweka nia, kama nilivyosema naweza kuwa mwalimu, nikawa. Nilisema naweza kuingia kwenye siasa na nikawa mbunge kweli ikawezekana, katika hii dunia kila kitu kinawezekana kama tu utakuwa umejiwekea malengo na mipango ya kufanikisha,” alimaliza Matiko.

Matiko alilikamata Jimbo la Tarime-Mjini katika kinyang’anyiro cha uchaguzi uliopita wa mwaka 2015. Kabla ya ubunge huo, alikuwa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Mara kupitia chama chake cha Chadema.


Loading...

Toa comment