The House of Favourite Newspapers

UTAJUAJE KAMA UMEMPATA MTU SAHIHI? SOMA HAPA

YAWEZEKANA kwa kipindi kirefu ulikuwa ukitamani kumpata mpenzi wa kweli ambaye atakupenda na kukufanya uyafurahie mapenzi na maisha kwa jumla. Mara nyingi, kila mtu huwa na matarajio yake ndani ya kichwa chake. 

 

Kinachowakwamisha wengi na kufanya waendelee kuhangaika, huwa ni kujiwekea viwango vikubwa vya sifa za mtu anayetaka kuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi. Ukifuatilia kwa makini, wanawake wengi wanaochelewa sana kuolewa, huwa ni wale ambao ndani ya vichwa vyao wameshajiwekea viwango vya wanaume wanaotaka kuwa nao.

 

Utamsikia mwanamke anakueleza kwamba mimi nataka kuolewa na mwanaume mwenye kazi, nyumba na gari au nataka kuolewa na mwanaume mwenye mwili wa mazoezi, ‘six packs’, hendisamu na sifa nyingine kibao. Kama na wewe ni mtu wa aina hii, basi tambua kwamba utakuwa unapishana sana na fursa kwa kushindwa kuuona ukweli mkubwa.

 

Kwa wanaume nao, utakuta mtu ameshajiwekea viwango ndani ya kichwa chake, kwamba nataka kumuoa mwanamke mwenye shepu nzuri, mrembo, anayevaa mavazi ya kisasa, mwenye kazi, anayetokea familia ya kitajiri na sifa nyingine kedekede.

 

Haya ni makosa makubwa wanayoyafanya watu wengi kwa sababu ukweli ni kwamba, penzi la dhati huwa halina masharti wala vigezo. Huwezi kujua ni lini na wapi utakutana na mwanaume au mwanamke wa maisha yako, kama bado haujaingia kwenye uhusiano.

Penzi la kweli hutokea kama ajali, yaani mahali ambapo hukutegemea kabisa. Ushahidi wa hilo, jaribu kufuatilia historia za watu ambao wamedumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu na angalia jinsi walivyokutana.

 

Wapo ambao walikutana hospitalini, yaani mwanaume anaumwa, mwanamke naye anaumwa au ameenda kumuangalia mgonjwa, wakakutana, wakapendana, wakaanzisha familia na sasa wanadunda pamoja.

 

Wapo waliokutana sokoni, wapo waliokutana barabarani na kadhalika na mpaka leo wanadumu pamoja. Mapenzi hayana kanuni na kama nilivyosema, huwezi kujua moyo wako utamuangukia nani, kwa hiyo kujiwekea viwango na madaraja ni kupoteza muda au kutafuta maumivu.

 

Sasa utajuaje kama huyo uliyekutana naye ndiye uliyeandikiwa kuwa naye? Moyo jinsi ulivyo, unapotokea kumpenda mtu, huwa hauwezi kujificha. Utajisikia amani unapokuwa karibu naye, utafurahi kumuona, utatamani muda wote awe pembeni yako na utahisi uhuru mkubwa ndani ya nafsi yako.

Penzi la dhati, siyo lile linalokulazimisha, eti ukaazime nguo ili upendeze au ukodi gari ili uonekane unazo, litakutokea katika mazingira yako ya kawaida kabisa, ukiwa katika maisha yako halisi. Ukiona mtu anaonesha hisia na wewe kwa vile jinsi ulivyo, bila kuhangaika kutumia nguvu kubwa kumshawishi, elewa kwamba hilo ndilo penzi la kweli.

 

Ukiona moyo wako unampenda hata kama hajapendeza, hana kazi ya maana au hana kitu chochote kikubwa, yaani unampenda vile alivyo tu na huhitaji kitu kingine chochote cha ziada, basi tambua kwamba hilo ndiyo penzi la dhati.

 

Sasa kulitambua penzi la dhati ni jambo moja, lakini kulifukuzia na kuhakikisha unalipata, hilo pia ni jambo lingine. Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo nitakueleza mbinu unazotakiwa kuzitumia ili kuhakikisha unampata yule ambaye moyo wako umemchagua kwa sababu wapo watu wengi ambao wanateseka kwa sababu ya kumpenda mtu fulani, lakini hawajui nini cha kufanya kufikisha hisia zao.

Tukutane wiki ijayo.

 

 

Comments are closed.