Utata kifo cha Mbalamwezi wa The Mafik – Video

Abdallah Yusufu Matimbwa ‘Mbalamwezi’ (katikati) akiwa na wasanii wa kundi lake la Kundi la The Mafik kabla ya kifo.

KIFO cha msanii wa Kundi la The Mafik, Abdallah Yusufu Matimbwa ‘Mbalamwezi’ kimegubikwa na utata mkubwa kufuatia madai mwili wake kuokotwa juzi Ijumaa usiku katika eneo la Africana Mbezi Beach jijini huku ukiwa mtupu.

 

Mbalamwezi alikuwa ni mmoja wa wasanii wanaounda Kundi la The Mafik wakiwemo wengine wawili, Hamadai na Rhyno ambapo walijipatia umaarufu zaidi kupitia wimbo wao wa Passenger.

Utata huo umetokana na kuwepo kwa taarifa zinazodai kuokotwa kwa mwili wa msanii huyo ukiwa hauna nguo huku ikidaiwa na familia yake kuwa alipotea kwa muda wa siku tatu kabla ya kupata taarifa za kifo chake juzi usiku.

Kundi la The Mafik walipotua Global Radio siku za hivi karibuni.

Akizungumza na Championi Jumamosi memba mwingine wa kundi hilo, Hamadai alisema; “Kweli Mbalamwezi amefariki na tulikwenda kuhakiki mwili wake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuthibitisha kuwa ni kweli mwili ni wa kwake.”

 

Championi halikuishia hapo lilifika hadi nyumbani kwa marehemu, Tandika karibu na Shule ya Sekondari Tandika na kuzungumza na mama wa marehemu, Tabia Mponda ambaye alikiri kuwa mtoto wake kufariki dunia licha ya taarifa zake za kifo chake kuchanganya.

 

“Ni kweli amefariki lakini bado taarifa zake zinatuchanganya kama familia, wapo wanaosema kwamba mwili wake umeokotwa ufukweni na wapo ambao wanaosema umeokotwa huko Africana kwa sababu hatujui amepigwa au amegongwa maana miguu yake imeharibika vibaya.

 

“Lakini kabla ya hapo alipotea kwa muda wa siku tatu kabla ya kupata taarifa kwamba amefariki na mwili wake kupelekwa Muhimbili, alikuwa hapatikani kwenye simu hivyo tulishindwa kujua amepatwa na jambo gani, yeye hatuishi naye hapa zaidi huwa tunawasiliana naye sasa hatujui nini kilimpata,” alisema Tabia.

 

Championi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Musa Taibu ambaye alivyopokea simu alisema: “Mnapiga simu mnataka nini, hamjui kwamba kuna wageni wa SADC? Ulikuwa unasemaje,” kabla ya kuelezwa akawa amekata simu.

 

Hata hivyo, familia ya marehemu imesema kuwa inatarajia kufanya mazishi ya msanii huyo leo Jumamosi saa saba mchana baada ya kuombwa na wasanii wenzake kufanya hivyo.

 

Imeandikwa na: Ibrahim Mussa, Ammar Masimba na Issa Liponda


Loading...

Toa comment