The House of Favourite Newspapers

Utata Msanii Beka Kuungwa Freemason!

DAR ES SALAAM: Utata mkubwa umeibuka juu ya picha zilizosambaa wikiendi iliyopita zikimuonesha msanii wa Bongo Fleva, Bakari Katuti ‘Beka Flavour’ akiungwa kwenye jamii ya siri inayohusishwa na imani za kishetani na utajiri wa ghafla ya Freemason.

 

Katika picha hizo, Beka ambaye ni zao la Yamoto Band anaonekana akisainishwa makaratasi na mwanaume aliyevaa mavazi yenye alama ya Freemason.

Baada ya kusaini makaratasi hayo yanayoaminika ni mkataba kati yake na jamaa hao, anaonekana akipongezwa na mtu huyo huku pembeni kukiwa na mwanamke ambaye naye amevaa mavazi ya Freemason.

 

Hata hivyo, kumekuwa na maoni mbalimbali juu ya picha hizo huku wengine wakidai ni kweli amejiunga na Freemason huku wengine wakidai huenda ni kiki anataka kutoa wimbo mpya hivyo ni sehemu ya kutafuta ‘attention’ ya watu wanaoamini kwenye mambo hayo.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la Ijumaa Wikienda, Beka adai kuwa picha hizo ni za kutengeneza na kwamba wanaofanya hivyo ni watu wa mitandaoni.

“Huyo siyo mimi. Hizo picha hata mimi nimetumiwa, ni za kutengeneza.

 

“Kwanza sitaki kuizungumzia sana hii ishu kwa sababu kadiri ninavyozungumza ndivyo ninavyozidi kuikuza. Kwa sasa nipo Mikumi (Morogoro) natoka kwenye shoo naelekea Dar, tuache hiyo ishu tuzungumze mambo mengine.

 

Hata hivyo, alipoulizwa kama picha hizo ni za kutengeneza atachukua hatua gani, Beka alifunguka;

“Siwezi kuchukua hatua yoyote maana watu wangapi wanazushiwa mambo kibao, wapo mpaka waliozushiwa wamekufa na wakaenda kulalamika kwenye vyombo husika, lakini hakuna kilichoendelea au hatua iliyochukuliwa.”

 

Beka anaungana na wasanii wengine wengi Bongo ambao wamekuwa wakihusishwa na jamii hiyo kwa madai kuwa hujiunga nayo ili kutoboa kimuziki na kufanya vizuri kimataifa kisha kujiingizia utajiri mkubwa kama walivyo akina Jay Z wa Marekani.

Stori: Memorise Richard

Comments are closed.