UTATA WAIBUKA MJENGO WA LYNN

UTATA! Ndiyo maneno unayoweza kusema baada ya muuza nyago maarufu Bongo ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Irene Godfrey ‘Lynn’ mjengo wake kuwekwa sokoni kwa ajili ya kupangishwa kitendo ambacho kimeibua maswali, Risasi Jumamosi linakupa habari kamili.  

 

Utata huo umeibuka baada ya Septemba mwaka jana Lynn kuaminisha watu kuwa anamiliki nyumba hiyo lakini cha kushangaza hivi karibuni dalali aliiweka mitandaoni kuwa inapangishwa.

 

“Jamani hii nyumba ninayoiona hapa mbona ni ile aliyoiposti Lynn na kuweka hatimiliki kwenye ukurasa wake na kudai kuwa ni ya kwake, sasa iweje leo imepostiwa na dalali kwamba inapangishwa?” alihoji shabiki wa Lynn anayeitwa Jamila ambaye aliiona nyumba hiyo kupitia ukurasa wa dalali wa Instagram.

 

Kutokana na utata huo kuibuka na mashabiki kuhoji mmiliki halali wa nyumba hiyo, Risasi Jumamosi liliingia kazini ili kuupata ukweli ambapo lilianza na dalali aliyeiweka nyumba hiyo mtandaoni kuwa inapangishwa anayejulikana kwa jina la Dalali Muigizaji na kufunguka ukweli wake anaoujua.

 

Dalali huyo alieleza kuwa nyumba hiyo Lynn amebakiza siku chache ahame na alikuwa amepanga kama wapangaji wengine.

“Hiyo nyumba mmiliki yupo lakini siyo huyo dada mnayemtaja kuwa ni msanii, anayeimiliki ni mtu wa kawaida tu ambaye hapendi kujulikana, kwanza hata kuongea hapa naona kama nimekiuka ila ukweli ni kwamba yeyote anayekaa pale amepangishwa na ile picha niliyoposti nilitumiwa na mmiliki wa nyumba hiyo ambaye alinipa kazi hiyo,” alisema dalali.

 

Aliongeza kuwa baada ya yeye kuweka picha hiyo na kuitangaza nyumba kuwa inapangishwa, Lynn alimpigia simu na kumwambia kuwa anaomba aifute kwani bado ataendelea kukaa yeye asitafutwe mpangaji mwingine. “Anaposema anaimiliki yeye anamaanisha nini wakati aliniomba nisitafute mpangaji ataendelea kuishi yeye? Nakuwa simuelewi,”alisema dalali huyo.

 

LYNN AWAKA

Baada ya kupata maelezo ya dalali, Risasi Jumamosi lilimtafuta Lynn na kufanikiwa kumpata kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar kulipokuwa na zoezi la kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba ambapo aliwaka kwa kusema;

 

“Jamani mnataka niongee nini hapo kama watu washajitafutia jibu lao? Nilishalizungumzia hilo suala na siwezi kuliongelea tena maana nitaonekana natafuta kiki kwaheri,” alisema Lynn na kuondoka bila kutatua utata uliopo.

MWENYEKITI ANENA

Kwa kuwa majibu ya Lynn hayakuanika ukweli Risasi Jumamosi lilifunga safari mpaka kwenye Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Goba Kunguru na kukutana na mwenyekiti, Musa Meso ili aweze kueleza ukweli wa mmliki halali wa nyumba hiyo ambapo alisema kuwa anamjua mwenye nyumba lakini si mtu anayependa kujulikana.

 

“Japokuwa sijawahi kumuona huyo Lynn ila nasikia alipangishiwa tangu mwaka jana na mwenye hiyo nyumba yupo ila siyo huyo dada bali ni mtu mwingine ambaye hapendi sana kujulikana maana hajawahi kuishi hapo kabisa huwa anapangisha tu, sasa kama huyo msanii anasema ni yake labda ni kiki tu ila mmiliki halali yupo na tunamfahamu tangu muda na hajaiuza hiyo nyumba,” alisema mwenyekiti huyo.

Toa comment