MBUNGE wa Jimbo la Mtama (CCM), Nape Nnauye leo Machi 07, 2018 amewataka wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kujali itikadi ya vyama, dini au rangi zao, kuwa kitu kimoja na kumuunga mkono Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, juu ya hoja yake binafsi aliyoiwasilisha kwa Katibu wa Bunge.
Nape amesema hivyo kupitia akaunti yake ya mtandao wa Tweeter.
Bashe aliwasilisha barua ya hoja binafsi kuunda Kamati ya Bunge ili ichunguze matukio mbalimbali yanayotishia umoja, usalama na mshikamano nchini ambapo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), alisema hatua hiyo ya Bashe ni ya “unafiki”, akimtaka mbunge huyo (Bashe) akikemee chama chake kirudishe uhuru wa kufanya mikutano kwa vyama vya upinzani, kuhakikisha watu hawatekwi na kuuawa.
Pia, Mbunge wa Kigoma Mjini, alimjibu Bashe akisema kwamba kwa yeye kuamua kuchukua hatua hiyo, ni mwanzo mzuri na anabidi kuungwa mkono kwani ana nia njema.
“Kazi ya mbunge ni pamoja na kuwasemea wananchi ambao kwa namna moja ama nyingine hawana fursa ya kwenda wenyewe Bungeni. Tumuunge mkono Mheshimiwa Bashe bila kujali tofauti zetu za itikadi, dini au rangi”, amesema Nape.
Nape ameongeza kwamba hoja binafsi ndani ya Bunge ni moja ya njia za kutafuta ukweli na suluhisho juu ya jambo fulani ambalo linatafutiwa ufumbuzi wake.
Comments are closed.