The House of Favourite Newspapers

UTI; gonjwa linalosumbua wanawake

0

urinary-tract-infectionLeo tutazungumzia kwa undani tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo,  ugonjwa unaowasumbua wanawake wengi na watoto,  kitaalamu huitwa Urinary Tract Infection au maarufu UTI.

Maambukizi katika njia ya mkojo au kama unavyojulikana kwa wengi UTI huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na mrija wa ureter ambao ni mshipa unaosafirisha mkojo kutoka kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na urethra.

Ugonjwa huu unaathiri zaidi kibofu cha mkojo na urethra lakini unaweza pia kuathiri figo. Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalam huitwa Simple Cystitis au Bladder Infection, na maambukizi hayo yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa Pylonephritis au Kidney Infection.

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia coli (E. coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa.

Lakini baadhi ya watu wanaweza kupata tatizo hili kutokana na kuingiwa na fangasi ingawa pia zipo sababu nyingine chache. Bakteria wa Escherichia Coli hawasababishi peke yao UTI bali huambatana na wengine waitwao Staphylococcus, Saprophyti cus, Pseudom onas, Enterobacter na kadhalika.

 Maambukizi katika njia ya mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote. Wapo wanawake ambao wamekuwa wakidhani kwamba tatizo la kutokwa na uchafu ukeni ni ugonjwa huu na hilo si sawa kwani huo ni ugonjwa tofauti kabisa na UTI.

 Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo, inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo.

Kama maambukizi yako katika eneo la kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, kitaalam huitwa Lower Urinary Tract Infection na yakihusisha eneo la juu ya kibofu jina hubadilika na kuitwa, Upper Urinary Tract Infection.

 SABABU ZA UGONJWA

Mara nyingi maambukizi haya kwa wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri sehemu za siri na kuvaa nguo za ndani zilizo chafu. Pia huweza kusababishwa na matumizi ya pedi za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa eneo la sehemu ya siri na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi kuzaliana kwa wingi.

 Halikadhalika upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi. Matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa siku nyingi na kutokunywa maji ya kutosha pia huchangia tatizo hili.

 Uwepo wa mawe katika figo na mirija ya figo pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya mkojo.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply