Uturuki Waanza Mchakato Wa Kuandika Katiba Mpya, Wataalamu Wa Sheria Kuanza Mchakato
Uturuki Waanza Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki ameteua timu ya wataalamu wa sheria kuanza mchakato wa kuandika katiba mpya.
Wakosoaji wake wanasema katiba hiyo itamruhusu kiongozi huyo kusalia madarakani hata baada ya mwaka 2028, pale muhula wake wa sasa utakapomalizika.
Akizungumza na maafisa wa chama chake, Erdogan alisema wataalamu hao kumi aliowachaguwa watatimiza jukumu la kupatikana kwa katiba mpya, kuchukuwa nafasi ya sasa ambayo iliandikwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1980.
Erdogan, ambaye ameitawala Uturuki kama rais tangu mwaka 2014 na aliyekuwa waziri mkuu kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya hapo, amekuwa akiwania upatikanaji wa katiba mpya, akisema kuwa iliyopo sasa imepitwa na wakati na bado inabeba athari za utawala wa kijeshi, licha ya kufanyiwa marekebisho mara kadhaa.