The House of Favourite Newspapers

UVIMBE KATIKA MLANGO WA UZAZI (NABOTHIAN CYST)

TATIZO hili la uvimbe wa mlango wa kizazi au kitaalam linaitwa Nabothian Cyst au Nabothian Follicle ni vivimbe au uvimbe ambao ndani yake una uteute mwingi uliohifadhiwa kwenye vifuko ambavyo ndivyo huwa vinakuwa na uvimbe. Uvimbe au hali hii ya mabadiliko ukeni hufanana sana na saratani ya mlango wa kizazi katika hatua za awali.

 

CHANZO CHA TATIZO

Hali hii hutokea baada ya uwepo wa mabadiliko makubwa ya chembe hai au seli za mlango au shingo ya kizazi, upande wa ukeni kitaalam huitwa Ectocervix na sehemu ya mlango wa kizazi kuelekea ndani ya kizazi kitaalam huitwa Endocervix. Chembe hai zilizopo katika sehemu ya nje huitwa Stratified Squamous Epithelium na zile za ndani kuelekea kwenye kizazi huitwa Simple Columnar Epithelium.

 

Tatizo hapa hutokea baada ya ile sehemu ya nje ya Stratified Squamous Epithelium kuotea juu ya ile sehemu ya ndani ya Simple Columnar Epithelium. Kwa kawaida ile sehemu ya ndani chembe hai zake zina tabia ya kutoa majimaji au ute mzito wa kawaida umtokao mwanamke kila siku ambao hauna harufu au muwasho.

 

Kitendo cha lile tabaka la nje kulalia la ndani, huziba njia ya kutolea uchafu au ute huo ziitwazo Crypts na kufungiwa uchafu huo kwa ndani na kusababisha uvimbe kujitokeza. Tatizo hili la mabadiliko ya chembe hai hizi husababishwa na mambo mbalimbali, mfano uzazi, kujifungua kwa njia ya kawaida na kuumia au kuchanika mlango wa kizazi.

 

Chanzo kingine ni maambukizi sugu ya mlango wa kizazi yaani Chronic Cervicitis ambao dalili zake ni kutoka na uchafu ukeni na harufu na maumivu wakati wa tendo la ndoa. Kwa hiyo mwanamke yeyote aliye katika umri wa kuzaa yupo hatarini kupata tatizo hili. Tatizo hili ukiwa nalo haliwezi kwisha lenyewe hadi litibiwe.

DALILI ZA TATIZO

Uvimbe wa Nabothian huwa hauna dalili za moja kwa moja, dalili hutegemea na chanzo ambapo kama ni maambukizi sugu ya kizazi, basi hali hii itaambatana na maumivu ya tendo la ndoa.

 

Wanawake wengi huwa hawagunduliki kirahisi kutokana na dalili zake kuchanganya. Wanawake wengi hugundulika wanapokwenda kupima saratani ya mlango wa kizazi, wengine wakati wanapotafuta mtoto ambapo anapochunguzwa mlango wa kizazi ndiyo tatizo linapojulikana.

 

Mara nyingi mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika kutoa uteute mwingi ukeni kila mara na hata damu ya hedhi huwa na uteute mwingi ukeni kila mara na hata damu ya hedhi huwa na uteute. Ute au majimaji haya ya kuvutika na huwa hayana vipindi maalum.

 

Kuanzia anapoona damu ya hedhi hadi anapoingia tena, wakati wa tendo la ndoa hujikuta analoa sana. Mwanamke pia hulalamika kusumbuliwa sana na tatizo la kutokwa na uchafu ukeni kila mara ambapo hauna harufu wala muwasho na hutumia dawa nyingi bila mafanikio, hupata nafuu na tatizo hujirudia.

UCHUNGUZI

Hufanyika katika kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama ambapo vipimo kama Colposcopy hufanyika. Vipimo kama Pap Smear, High Vaginal Smear na vingine ambavyo daktari anaona vitafaa hufanyika.

 

TIBA

Ingawa tiba ya tatizo hili ipo lakini wakati mwingine tatizo hili linaweza kuisha lenyewe endapo siyo la muda mrefu sana. Tiba kubwa ya tatizo hili ni kuondoa hizo sehemu zenye uvimbe au uvimbe wenyewe. Matibabu hupatikana katika vituo vyenye madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama ‘GYNECOLOGIST’.

Comments are closed.