The House of Favourite Newspapers

Uvimbe katika sehemu za siri za mwanaume (SCROTAL MASSES)

ovariancystdiagramUvimbe katika sehemu za siri za mwanaume unaweza kusababishwa na matatizo mengi, mfano maambukizi katika kiwanda cha kuzalishia mbegu za kiume, Ngiri au Hernia, kuvimba kwa mishipa ya damu, kujaa maji au busha,  kuvimba  kwa mirija ya mbegu za  kiume,  saratani  ya  korodani, maambukizi sugu ya korodani, kujinyonga  kwa  korodani na matatizo mengine.

 

JINSI MATATIZO HAYA YANAVYOTOKEA

Maambukizi  katika  vifuko  vya  kutunzia mbegu au  kiwanda  cha  mbegu  na  maambukizi  sugu  ya njia ya mkojo  au  maambukizi  ya  tezi  dume  hasa endapo mwanaume atakuwa ameshawahi  kuumwa  ugonjwa  wa  kisonono  au  gono  ambao dalili  zake  ni  kutokwa  na  usaha  katika  njia  ya  mkojo.

Wengine  hupatwa  na  tatizo  hili  baada ya  kufanyiwa  upasuaji  wa  kuondoa  tezi  dume  au  endapo  mgonjwa  atakuwa  aliwekewa  mrija wa  mkojo kwa  muda  mrefu. Ugonjwa  wa kifua  kikuu pia huchangia tatizo hili kwa kiasi kikubwa.

Tatizo huanza ghafla, huambatana na homa na kutetemeka na maumivu makali ya korodani, ukipapasa kwa ndani ya korodani utagusa vivimbe kama goroli kwa ndani zaidi juu ya korodani. Ugonjwa  unaweza  tu  kutulia  baada  ya  kuanza  matibabu lakini madhara yake ni kuziba kwa njia  ya  kupitishia  mbegu  hivyo  kukufanya  uwe  mgumba.

Maambukizi ya korodani yote huwa makali na huanza ghafla au kwa kipindi kifupi, hutokea zaidi katika kipindi cha ujana na husababishwa na maambukizi mengine yoyote ya korodani. Mgonjwa hulalamika homa kwa vipindi, maumivu ya korodani na kuvimba upande ambao una maumivu.

Hali hii ikiendelea bila jitihada za haraka kuchukuliwa, korodani  hiyo husinyaa  na  kupotea  kabisa  na  kukufanya  uwe  na  korodani  moja, endapo  tatizo  litakuwa kwenye  pande  zote  mbili, basi  korodani  zote  mbili  zinaweza  kusinyaa  na  kupotea  na  kujikuta huna  korodani.

Endapo korodani itajinyonga  basi  itakufa kwa kutokuwepo  na  mzunguko  wa damu wa kutosha na  tiba  yake  ni  upasuaji  na  kuiondoa.

Mwanaume  ambaye  ana  korodani  moja, ni vema  akapime  mbegu  za  uzazi  kuona  kama  zipo za  kutosha  na yule  ambaye  hana  kabisa  korodani, uwezekano  wa  kuzaa  haupo. Saratani  ya korodani  huzalisha uvimbe ambao ni mgumu kwenye korodani na hauna maumivu. Kwa hiyo, endapo  una  uvimbe mgumu kwenye korodani na hauna  maumivu,  ni  vema  uondolewe  kwa upasuaji.

Ugonjwa  wa  ngiri  au hernia hutokana  na  uwepo  wa  uwazi  toka  juu tumboni  hadi   ndani  ya   mfuko  wa  korodani. Njia  hii  huwa  inakuwepo unapozaliwa  na  kuziba  taratibu  kutokana  na  kuendelea  kwa  misuli.

Kama  njia  ya  ngiri  itaendelea,  husababisha  matumbo  kuingia  humo  na kujaa  kwenye  mfuko  wa  korodani.  Ugonjwa  huu  wa  ngiri  ni  tofauti  na busha. Busha  ni  hali  ya  kujaa  maji  katika  mfuko  wa  korodani  na husababishwa  na  maambukizo  ya  vimelea  viitwavyo  filaria  na huenezwa  na  mbu.

Ugonjwa  wa  ngiri  pia  huwatokea  watoto,  vijana na watu wazima.  Ugonjwa  wa  busha  na  ngiri hutibika kwa upasuaji. Kinga ya mabusha ni matumizi ya dawa za kinga ya mabusha na matende ambayo kila mwaka hutolewa  bure na serikali  kwa  wananchi  wote, huwa  kunakuwa na kampeni maalumu.

Ugonjwa wa ngiri hutokana na  kasoro  katika  njia zake, ili  kuepuka  ni kutofanya  kazi  ngumu  kama  utagundulika  una tatizo  hilo.

USHAURI

Matatizo  haya  ya  korodani  husababisha  matatizo  makubwa  ya  uzazi  kwa  mwanaume kwa hiyo  ni  vizuri  kuwahi hospitali kama una matatizo sehemu hiyo, usipuuze  hata  maumivu kidogo  kwani athari zake ni kubwa.

Matatizo au maambukizi  katika  njia  ya  mkojo  pia ni shida kubwa kwa mwanaume. Epuka  kuumia  korodani, joto kali kwenye korodani, uvutaji  wa sigara, bangi  na  matumizi  mengine  ya  madawa  ya  kulevya.

Epuka  ngono  zembe, vyote  hivi  huhatarisha afya  yako  ya  uzazi.

Wahi  katika  hospitali  ya  mkoa  kwa  uchunguzi  na  matibabu.

Comments are closed.