Uwazi lachangisha sh. Milioni 14

Na Haruni Sanchawa

Gazeti hili la Uwazi limekuwa likiandika habari za  kijamii kwa lengo la kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali na kwa kushirikiana na wasomaji wake wanaochangia fedha, limefanikiwa kukusanya zaidi ya jumla ya shilingi milioni 14,600,000.

Baadhi ya wagonjwa waliosaidiwa kutokana na kuandikwa katika safu hii Agosti na Septemba mwaka huu na ambao wamewashukuru wasomaji wetu ni hawa wafuatao:

Feisa Masaka (28)

Mwanamke huyu mkazi wa Chanika Msumbiji, Ilala Dar alipatwa na uvimbe wa ajabu na habari yake kuandikwa na gazeti hili.

Kwa kuwa ni yatima, kilio chake alikitoa kupitia gazeti hili na akachangiwa zaidi ya sh. 1,000,000 hata hivyo, sasa anauguza kidonda na anahitaji msaada zaidi, namba yake ni 0717 260769.

 Revucatus Machanga (23)

Huyu ni mkazi wa Gongo la Mboto anayetatizwa na ugonjwa wa macho.

Baada ya habari ya kijana huyu ambaye ameshindwa kuendelea na chuo kutokana na kusumbuliwa na macho kuandikwa katika safu hii toleo namba 931, Septemba 18, mwaka huu, Watanzania wenye huruma walimchangia jumla ya sh. 11,000,000 na anaendelea na matibabu japokuwa lengo ni kupelekwa India hivyo michango zaidi inahitajika.

Aliyeguswa awasiliane naye kwa namba 0713 275740.

Feruzi Suleiman (27)

Huyu ni mgonjwa aliyekatwa miguu baada ya kupigwa shoti  ya umeme akiwa katika shughuli zake, Tegeta, Dar.

Baada ya habari yake kuandikwa na gazeti hili toleo namba 933 la Agosti 25, mwaka huu alipata msaada wa baiskeli yenye thamani ya sh. 2,100,000 ambayo  sasa inamsaidia  kutoka sehemu  mmoja kwenda nyingine.

 “Nawashukuru wote walionisaidia,” alisema akiwa kwao maeneo ya Changanyikeni jijini Dar.

Licha ya kupata usafiri huo bado anahitaji msaada kwa sababu hivi sasa hawezi kufanya kazi yoyote. Namba yake ni 0654 830584.

Emakulata John (28)

Bado mgonjwa, anasumbuliwa na ugonjwa wa uti wa mgongo uliosababisha kupooza. Hakuweza kutibiwa  kutokana na kukosa fedha hivyo kulala tu kitandani kwao Gongo la Mboto Dar.

Baada ya habari yake kuandikwa na gazeti hili kwenye toleo namba 937, Septemba 8, mwaka huu, wasomaji walimchangia sh. 510,000 za matibabu, hivyo kutoa shukrani kwa wote waliomsaidia.

Bado anahitaji msaada, wasiliana naye kwa simu namba 0719 464341.

Toa comment