The House of Favourite Newspapers

UWOYA, MOBETO SAWA! WENGINE JE?

Picha inayohusiana

LIKO wazi kwamba siku hizi imekuwa kama fasheni kwa mastaa Bongo hata wasio mastaa kupiga picha za utupu na kuposti katika mitandao ya kijamii.

Kwanza ya yote! Niwashukuru Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kufanikiwa kuwaita baadhi ya mastaa hao na kuwapa onyo kali. Julai 19, mwaka huu, kamati hiyo ya maudhui ilimuita staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya pamoja na mwanamitindo Hamisa Mobeto na kuwapa onyo kali baada ya kuwakuta na makosa ya kuposti picha za nusu utupu katika mitandao yao ya kijamii.

Kamati hiyo haikuishia kuwapa onyo tu, bali ilienda mbali zaidi na kuwaonesha kama mfano na kuwataka kila mmoja kuingia katika mitandao yao ya kijamii kuomba radhi sambamba na kuwa mabalozi wa kuwahamasisha wenzao wasifanye vitendo hivyo.

MOBETO

Ukiangalia kosa kubwa alilofanya Mobeto ni kitendo cha kuposti picha akionesha tumbo lake kipindi ana ujauzito wa mtoto wake, Abdul Nasibu ‘Daylan’. Mtoto huyo alizaliwa Agosti 8, mwaka jana, ukirudi nyuma kuanzia kipindi hicho alichoposti picha hiyo hadi leo hii, wapo mastaa wengi waliposti picha za utupu zaidi ya za kwake lakini hatujawasikia wakiitwa ama kuchukuliwa hatua, hilo tuwaachie wao!

UWOYA

Kwa upande wa dada huyu, aliweka picha ikimuonesha akiwa amevalia vazi la nusu utupu ufukweni, huenda kuvalia vazi hilo akiwa ufukweni bila kujua madhara ya kuposti mitandaoni wengine wangechukuliaje!

Ninachotaka kusema hapa, hatua iliyochukuliwa na TCRA ni nzuri sana lakini bado hawajamaliza yaani kama ni safari basi hii ni robo tu, hawajafika mwisho ama katikati wakaona kama suala limeshaisha, hapana! Bado wana kibarua kizito cha kukomesha tabia hii kwa sababu hao waliowaita ni ‘sample’ ndogo tu!

Wapo wadada wengi sana wa mjini ambao wamejiachia sana kwa kuposti picha za namna hiyo lakini bado hawajachukuliwa hatua hadi tunajiuliza hamuwaoni au? Kingine hata wengine hawajulikani kazi gani ambayo inawaweka mjini ila wao ni kuposti picha za utupu kama hawaishi nchini kumbe tupo nao, wapo wengi ni jambo la kufanya uchunguzi na kuwaibua kisha kuwapa adhabu ili matendo hayo yakome.

SANCHI

Mfano mdogo, kuna mdada ambaye amejipatia umaarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na kuposti picha zilizokosa maadili anayefahamika kwa jina la ‘Sanchoka ama Sanchi’.Kwa picha anazoposti kwa haraka unaweza kusema anaishi eneo ambalo hawana sheria juu ya picha hizo, ukiangalia kwa picha tofauti tangu kipindi Mobeto anaposti ile ya tumbo la ujauzito hazifai hata kulinganishwa kwa jinsi zilivyokosa maadili.

Hii maana yake nini? Maana yake ni TCRA bado wana kibarua kizito cha kudhibiti watu wa namna hii kwa kuweka sheria kali zaidi sio tu kuwaita ‘wachache sana’ na kuwaonya bali kuwaadhibisha vikali ili hata wengine wanaofikiria kupiga picha za namna hiyo waingiwe na woga na wasiweze hata kuthubutu kufanya kitendo cha namna hiyo.

KWA NINI WANAFANYA HIVYO?

Ipo dhana imejijenga katika vichwa vya wengi wao wanaotupia picha hizo kuwa inawasaidia kuendesha kazi zao. Wapo wanaodaiwa kudanga kupitia picha hizo kwamba wakiziweka wanapata wanaume wa ‘kumalizana nao’ na kupewa pesa ndefu, wapo wanaodaiwa kutengeneza kiki na wapo wanaotaka kuendelea kujiweka juu muda wote (kutochuja) na kupata followers wa kutosha kwenye akaunti zao.

ELIMU

Elimu inahitajika sio baada ya mtu kukosea ila kabla kwa watu wengi zaidi ili kila mtu awe balozi na iwe rahisi kulidhibiti suala hili na sio mmoja mmoja hiyo haitosaidia. Ukijaribu kuangalia, vijana wengi kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa ‘addicted’ kuona picha hizi na kuzishabikia bila kujua upande wa pili kuna madhara makubwa kwa anayeziachia.

Pia ni lazima kuhakikisha hata hawa mliowaita hawarudii tena kufanya kosa hilo isije ikawa onyo lenu ni kazi bure na halijabadilisha chochote, bado wanatakiwa kuwafuatilia maana kuna watu wengine bila kufuatiliwa hawawezi kubadilika kwa hiyo lazima wahakikishe hawa wawili wanakuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha watu wasiposti tena hizo.

 Makala: SHAMUMA AWADHI

Comments are closed.