The House of Favourite Newspapers

UWOYA: NAPENDA MWANANGU ANIRITHI UPENDO NA KUJALI WATU

MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu, mimi hapa niko mzima lakini pia najua wazi nawe msomaji wangu uko poa, spidi yangu ni ileile 120 hakuna kufunga breki ili wewe msomaji wangu upate kile unachostahili kila wiki. Leo tunaye staa wa filamu Bongo Muvi, Irene Uwoya ambaye ameyaweka wazi maisha yake halisi na mtoto wake Krish.

 

Staa huyo ameyafafanua mambo mengi kuhusu yeye na mwanaye huyo kama ifuatavyo;

Ijumaa Wikienda: Sio kawaida yako kuonekana mara kwa mara na mtoto wako, ni kwa nini?

Uwoya: Siwezi kuonekana na mtoto wangu kila sehemu zaidi ya nyumbani au sehemu ambayo ninastahili kuwa naye maana kuna wakati niko na kazi zangu.

Ijumaa Wikienda: Unaishi na Krish? Maana kipindi cha nyuma alikuwa anakaa na bibi yake.

Uwoya: Ninaishi na mwanangu, kwa bibi anaenda kusalimia japokuwa amemlea sana tangu akiwa mdogo.

 

Ijumaa Wikienda: Nini ambacho kinakupa furaha kwa mtoto wako?

Uwoya: Kwa kweli kila kitu cha Krish nakipenda sana, hakuna ambacho sikipendi, halafu simchoki sasa, hata kama nikikaa naye siku nzima siboreki.

Ijumaa Wikienda: Jina la Krish ulipewa na nani?

Uwoya: Mimi nilikuwa nampenda sana yule muigizaji wa filamu za Kihindi aitwaye Krish na ndio maana nilimpa jina hilo.

Ijumaa Wikienda: Hakusumbui kuhusu baba yake?

 

Uwoya: Ukweli ni kwamba Krish, anajua baba yake katangulia mbele ya haki lakini anamkumbuka kama binadamu kwa sababu alikuwa akimpenda.

Ijumaa Wikienda: Unapenda mtoto arithi nini kutoka kwako?

Uwoya: Achukue upendo wangu na kujali wengine, ndio kitu muhimu kitakachomsaidia maishani.

Ijumaa Wikienda: Kuna baadhi ya wamama wanadekeza sana watoto wao, vipi kwa upande wako?

Uwoya: Mimi sio kwamba nadekeza ila pale mtoto anapostahili kubembelezwa nafanya hivyo lakini akinikosea pia nakuwa mkali kama mama.

 

Ijumaa Wikienda: Kuna mabadiliko yoyote uliyopata baada ya kumzaa Krish?

Uwoya: Makubwa sana, amenifanya nijitambue zaidi na kila ninachofanya nakumbuka kuna yeye mbele yangu.

Ijumaa Wikienda: Vipi mpango wa kuongeza mtoto mwingine.

Uwoya: Kwa sasa bado kabisa, hiyo haiko kwenye ratiba zangu.

Ijumaa Wikienda: Haya asante kwa ushirikiano wako.

Uwoya: Asante na karibu tena.

Stori: Imelda Mtema, Dar

Comments are closed.