The House of Favourite Newspapers

Uzazi wa mpango unaoepuka, usioepuka kemikali

KUNA njia nyingi za kupanga uzazi salama kwa wanawake. Kwa ujumla kuna njia za aina mbili, ambazo kitaalamu huitwa ni barrier yaani vizuizi na hormonal, kwa Kiswahili ni dawa, utofauti wake ni jinsi zinavyofanya kazi. Vizuizi huzuia yai na mbegu za kiume zisikutane kabisa na yai la kike au kuzuia mimba isitunge bila kutumia dawa yoyote. Hapa mhusika anaweka kitanzi kisicho na dawa na njia za asili kama kuhesabu siku au kutumia kondomu. Njia hizi ni nzuri kwa kuwa hakuna kemikali yoyote inayoingia mwilini wala homoni hazibadilishwi ili kuzuia mimba.

Njia za dawa au hormonies, ni zile zinazobadilisha homoni za mwanamke au mwanamume kwa lengo la kuzuia mimba kutungwa na hivyo kutumia aina fulani ya dawa. Wataalamu wanashauri kuwa iwapo mtu ana mpango wa kuanza kupanga uzazi, ni vema akaonana nao kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu.

Faida ya kutumia njia hizo ni hizi zifuatazo, tukianza na zile zisizoingiza kemikali mwilini.

Kondomu: Njia hii ambayo ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 86, pia huzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono kama Ukimwi.

Kuhesabu siku: Njia ya kutumia kalenda au kuhesabu siku, ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 76. Katika njia hii, wahusika huamua kufanya mapenzi kutegemea siku za mzunguko wa hedhi ‘ovulation’ wa mwanamke kwa kutokutana siku za hatari.

Yai la mwanamke linapevuka (ovulate) kuanzia siku ya 10 hadi ya 18 tangu kuanza kwa hedhi yake. Hesabu yake si ngumu kwa mtu mwenye siku zinazoeleweka, labda kama mzunguko wa mwanamke ni siku 32 kila mwezi na haibadiliki, basi ni rahisi kuifuata njia hii. Kama siku zako hazibadilikibadiliki, unatakiwa uzigawe kwa tatu kuanzia siku ya kwanza ya hedhi. Tukitumia mfano wa siku 32 gawanya kwa tatu, ni siku 10 kasoro mbili.

Kwa hiyo, toka siku ya kwanza ya hedhi hadi ya 10 ni salama. Siku ya 11 hadi ya 22 ni hatari, siku ya 23 hadi 32 ni salama pia. Kama siku zinabadilika badilika, mwanamke anatakiwa kuhesabu siku ya kwanza ya hedhi hadi ya 10 ni salama, halafu siku 10 zinazofuata ni hatari, huku siku zilizobaki hadi hedhi inayofuata zinakuwa salama.

Njia zinazoingiza kemikali mwilini lakini zinazuia mimba ni hizi:

Vidonge: Vidonge huwa na dawa ambazo zina vichocheo vinavyozuia yai kutoka kwenye ‘ovary’ (ogani inayozalisha mayai ya mwanamke). Kwa kutumia njia hii, mwanamke anakuwa na uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 95.

Moja ya faida ya vidonge ni kufanya mzunguko wa hedhi kuwa unaoeleweka na kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya ‘ovary’ pamoja na maradhi ya shingo ya kizazi. Faida nyingine ni kupunguza maumivu ya tumbo na wingi wa damu ya hedhi na hata kupunguza chunusi.

Sindano: Njia hii ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99. Sindano huwa na dawa ambazo zina vichocheo vinavyozuia yai kutoka kwenye ogani inayozalisha mayai ya mwanamke. Wanawake wengi hupenda kutumia sindano katika kupanga uzazi ukilinganisha na njia nyingine.

Njia hii haina madhara, bali inaweza kugandisha damu kama ilivyo kwa dawa nyingine za kuzuia mimba au kwa wajawazito. Huweza kusababisha kichefuchefu, kutopata hamu ya kula, kunenepa au kukonda na kichwa kuuma.

Wakati mwingine inaweza kusababisha kuvurugika kwa hedhi au kupotea kabisa katika kipindi cha miezi ya mwanzo.

Vijiti (vipandikizi): Hivi ni vijiti vyembamba vidogo vinavyowekwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa mwanamke kwa njia ya upasuaji mdogo, ambapo vina kichocheo kinachozuia kupevuka kwa yai.

Kama ilivyo kwa sindano, kijiti pia kina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99. Husaidia kuzuia mimba kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano tangu kupandikizwa.

Kwa kutumia njia hii katika kupanga uzazi, mwanamke anaweza kuharibu mzunguko wake wa hedhi na kunyonyoka nywele.

Kitanzi: Hiki ni kitu kidogo kilichotengenezwa kwa aina maalumu ya plastiki ambacho huwekwa kwa utaalamu ndani

ya mfuko wa uzazi. Kinaweza kufanya kazi hadi miaka 10. Kitanzi kina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99, lakini ubaya wake ni kwamba kinasababisha ongezeko la damu ya hedhi na kuumwa tumbo. Wenza ni lazima wawe wametulia pindi wanapoamua kutumia njia hii kwa kuwa kina tabia ya kudaka maradhi. Nawashauri wahusika kutoitumia kama wanadhani bado wanajihusisha na ngono zembe.

Kufunga kizazi: Ni upasuaji wa kuziba mirija ya kupitisha mayai (kwa mwanamke) au kupita mbegu (kwa mwanamume), wahusika wanapaswa kuwa na uhakika na uamuzi wao kwa sababu ukishafanyiwa upasuaji, hutaweza kurudishiwa hali ya awali.

Vidonge vya dharura: Vidonge hivi kitaalamu huitwa The morning after pill. Mara nyingi hutumiwa pale mwanamke anapofanya tendo la ndoa katika siku za hatari bila kutumia kinga yoyote dhidi ya mimba.

Husaidia kuzuia mimba iwapo vitanywewa ndani ya saa 72 baada ya kufanya ngono zembe. Kadiri unavyochelewa kuvinywa, ndipo uwezekano wa kufanya kazi unapopungua kwa kuwa havitatoa mimba iliyokwishatungwa, vidonge hivi mara nyingi hutumiwa na watu waliobakwa.

USHAURI

Elimu ya uzazi wa mpango hutolewa katika vituo vya afya au zahanati, kama una tatizo lolote kuhusu uzazi unaweza kwenda huko au kutuona sisi. Tutaweza kukusaidia kwa namba hiyo hapo

Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta. Simu: 0713 252394.

Comments are closed.