Uzinduzi Kampeni: Shigongo Apania Kuisimamisha Buchosa Septemba 24

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, anatarajia kuzindua rasmi kampeni zake Alhamisi ya Septemba 24, 2020 katika uwanja wa mpira wa Nyakaliro na kuanza kuchanja mbuga katika maeneo mbalimbali ya vijiji na kata katika jimbo hilo kusaka kura kwa wananchi.

 

Shigongo amesema amejipanga kuzindua na kufanya kampeni zake kistaarabu huku akinadi mambo mazuri ambayo yeye na chama chake cha CCM wamepanga kuwafanyia wananchi wa Buchosa kwa miaka mitano ijayo.

 

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunafanya kampeni za kistaarabu, kunadi sera zetu na kuwaeleza yote tuliyopanga kuwafanyia wananchi wetu wa Buchosa, tunafahamu wana changamoto nyingi zikiwemo miundombinu ya barabara, maji, huduma za afya, elimu,  kilimo, biashara, uvuvi, ufugaji pamoja na ajira, kila sekta tumeiwekea mkakati madhubuti na tutahakikisha maeneo yote haya yanatatuliwa ili maendeleo ya Wanabuchosa yasonge mbele kwa haraka.

 

“Tayari Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofika hapa jimboni kwetu Septemba 8, alitupatia barabara ya lami ya Sengerema – Nyehunge yenye urefu wa kilomita 47, na kuagiza ianze kutengenezwa kabla ya kuisha kwa Desemba mwaka huu.  Tunamshukuru sana Mhe Rais, sasa limebaki deni kwetu kuhakikisha tunampa kura za kutosha ili akayakamilishe na mengine ambayo tumeshamuomba na tutaendelea kumuomba atufanyie.

 

“Tunafahamu wananchi wa Buchosa wanaipenda sana CCM kwa sababu ya mambo mengi na makubwa yaliyofanywa ya serikali yao ikiwemo hospitali kubwa ya wilaya yenye uwezo wa kufanya upasuaji.  Sisi tutapiga kampeni kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda ili kuhakikisha tunashinda kwa kishindo kuanzia kura za rais, mbunge, madiwani wa kata zote 21 na CCM inarejea madarakani kuendelea na kuchapa kazi,” alisema Shigongo.

 

Aidha, katika uzinduzi huo, Shigongo amesema patakuwa na burudani za kutosha kutoka kwa wasanii maarufu kibao wakiwemo H-Baba,  wasanii wa nyimbo za Injili, Joel Lwaga, Paul Clement, Jane Misso, wengine ni wasanii wa Buchosa ambao ni Ronna Max na Dox Fleva pamoja na sapraizi ya wasanii kibao kutoka ndani na nje ya mkoa wa Mwanza.
Toa comment